Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vitendo vya walowezi wa kiyahudi huko Ukingo wa Magharibi vyakwamisha huduma muhimu kwa Wapalestina - OHCHR

Mwanamume Mpalestina amesimama katikati ya magofu kufuatia uharibifu wa nyumba yake huko Al Jiftlik-Abu al 'Ajaj, jimbo la Jericho, kutokana na ukosefu wa vibali vya ujenzi.
© UNOCHA Wapalestina wengi katika jumuiya tisa kwenye Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel wamefurushwa 2026 kutokana na mashambulizi ya sasa.

Vitendo vya walowezi wa kiyahudi huko Ukingo wa Magharibi vyakwamisha huduma muhimu kwa Wapalestina - OHCHR

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) imesema hali ya usalama katika Ukingo wa Magharibi, eneo la Palestina linaokaliwa kwa mabavu na Israel inaendelea kuzorota, ikieleza wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mashambulizi ya walowezi wa Israel dhidi ya Wapalestina, upanuzi wa makazi ya walowezi na hatua zinazozidi kuzuia raia kupata huduma muhimu.

Akizungumza leo Jumatano Julai 29 mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa OHCHR Ravina Shamdasani amesema hali hiyo inajiri miaka miwili baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutoa uamuzi wa ushauri kwamba uwepo wa Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria na unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo.

"Miaka miwili baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwamba uwepo wa Israel katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu ni kinyume cha sheria na unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo, ghasia zinazofanywa na walowezi na kuendelea kutwaliwa kwa ardhi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi vinazidi kuwa vibaya," amesema Shamdasani.

Kwa mujibu wa OHCHR, tangu Alhamisi iliyopita yaani Julai 23, Wapalestina wanane, akiwemo mtoto wa kiume mmoja, pamoja na wanajeshi wawili wa Israel wameuawa katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Vikosi vinashambulia wananchi

Shamdasani amesema walowezi na vikosi vya usalama vya Israel, ambavyo mara nyingi hufanya operesheni pamoja, vimeshambulia jamii za Wapalestina, vikiwashambulia wananchi, kuharibu na kutaifisha mali zao pamoja na kuchoma misikiti. Ameongeza kuwa vizuizi vya usafiri vimeongezwa na sasa vinawazuia Wapalestina kufika kwenye huduma muhimu.

Pia amesema ofisi hiyo ina wasiwasi mkubwa kufuatia tangazo la Serikali ya Israel la kuongeza idadi ya makazi na vituo vipya vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi.

"Tunasikitishwa na tangazo la Serikali ya Israel la kuongeza zaidi makazi ya walowezi na vituo vya walowezi, pamoja na wito wa wazi kutoka kwa viongozi wa Israel wa kulipiza kisasi na kutoa adhabu ya pamoja kwa jamii za Wapalestina, ukiambatana na vitisho vya kuugeuza Ukingo wa Magharibi kuwa Gaza nyingine," amesema.

Wito kwa mataifa

OHCHR imezitaka nchi nyingine kuchukua hatua za haraka na kwa mshikamano ili kusitisha mashambulizi hayo na kukomesha kunyang'anywa kwa Wapalestina ardhi yao.

"Mashambulizi ya walowezi wa Israel pamoja na kuanzishwa kwa makazi na vituo vipya vya walowezi vimefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa. Nchi nyingine lazima zichukue hatua za haraka na kwa umoja kusitisha mauaji yanayoendelea na kunyang'anywa kwa Wapalestina ardhi yao, na kuhitimisha ukaliaji wa Israel," amesisitiza Shamdasani.