Hali ya kibinadamu Gaza ina unafuu, lakini maendeleo ya binadamu yanasuasua – UN
- Kuna matumaini lakini kasi ni ndogo
- Bado mbinu za kujipatia kipato hazijashamiri
- Palestina yadai Israeli inachochea vurugu kwa maslahi ya 'uchaguzi'
- Israeli yadai Hamas lazima iweke silaha chini ili mashambulizi yakome
Hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, eneo la kipalestina linalokaliwa kimabavu na Israeli imeanza kuimarika, lakini maendeleo hayo yanaenda kwa kasi ndogo ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya wakazi.
Amesema Ramaz Alakbarov, Naibu Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Mchakato wa Amani Mashariki ya Kati, wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hii leo jijini New York, Marekani kutokea Yerusalem, huko Mashariki ya Kati.
“Ziara yangu ya hivi karibuni Gaza ilibaini hatua chanya katika kuondoa taka ngumu na kuruhusu vifaa muhimu vya usafi kuingia. Aidha, hali ya uhakika wa kupata chakula na lishe imeonesha nafuu, ingawa familia nyingi bado zinategemea misaada ya kibinadamu ili kuishi,” amefafanua afisa huyo.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa maendeleo hayo hayatoshi kutokana na kuendelea kwa watu kuhama makazi yao, msongamano mkubwa katika maeneo ya hifadhi, uharibifu wa miundombinu na vifo vinavyotokana na operesheni za kijeshi zinazoendelea licha ya mkataba wa kusitisha mapigano wa Oktoba 2025.
Bofya hapa kufahamu azimio namba 2803 (2025) lililopitishwa baada ya makubaliano hayo na kuridhia mpango wa vipengele 20 vya ujenzi mpya wa Gaza uliowasilishwa na Rais wa MArekani Donald Trump na pia jeshi la kimataifa la kuimarisha ulinzi kwenye eneo hilo lililozingirwa.
Matumaini aliyoshuhudia Gaza
Mfano wa matumaini ulioshuhudiwa ni juhudi za wahudumu wa afya wanaoendelea kutibu wagonjwa na kukarabati vituo vya afya licha ya mazingira magumu. Vilevile, mashirika ya kijamii yanaendelea kusaidia familia zilizohamishwa kupata makazi ya muda, elimu na huduma za afya.
Misaada pekee haitoshi
Alakbarov amesema misaada ya kibinadamu pekee haiwezi kuijenga upya Gaza. “Ni muhimu kuharakisha urejeshaji wa huduma muhimu, kujenga upya miundombinu, kurejesha fursa za ajira na kujipatia kipato, kuhakikisha upatikanaji wa makazi salama na kuongeza usambazaji wa vifaa muhimu vya ujenzi na huduma za msingi.”
Pia ametoa wito kwa pande zote ambazo ni Israeli na wanamgambo wa Hamas kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu kwa kulinda raia, wafanyakazi wa misaada na miundombinu ya kibinadamu ili kurahisisha utoaji wa misaada.
Nini kifanyike?
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, ili maisha ya kila mkazi wa Gaza yawe bora, kunahitajika ushirikiano wa karibu wa kimataifa na kisiasa utakaowezesha ujenzi wa kudumu, kuimarisha taasisi za Kipalestina, kurejesha huduma za msingi na kuanzisha mchakato wa kisiasa utakaosaidia kuleta amani ya kudumu pamoja na mazingira salama kwa wananchi wote.
Kauli ya Palestina
"Israel inatafuta kuchochea mvutano katika Ukingo wa Magharibi," amesisitiza Riyad Mansour, Mwakilishi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa akiwa na hadhi ya uangalizi akiongeza kuwa walowezi wa kiyahudi lazima wapokonywe silaha.
Amedai kuwa Israeli inachochea mvutano ili kuhalalisha ukandamizaji zaidi na hatimaye kurahisisha unyakuzi wa ardhi na kuwahamisha Wapalestina, au kufanikisha malengo ya kisiasa yanayohusiana na uchaguzi.
"Ndiyo, akiwa anakabiliwa na uwezekano wa kushindwa katika uchaguzi ujao, Netanyahu anatafuta faida za kisiasa kupitia umwagaji damu wa Wapalestina na hata Waisraeli," amesisitiza akiongeza kuwa, "hali hii inahitaji mwitikio madhubuti kutoka kwa jumuiya ya kimataifa."
Kauli ya Israeli
Mwakilishiw a Israeli kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Danny Danon, amesema Hamas imekataa kuweka chini silaha huku akilishutumu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutolishinikiza kundi hilo wala kulitangaza rasmi kuwa shirika la kigaidi.
“Hali hii imesababisha kuendelea kwa mateso ya wananchi Gaza” amesema, akiongeza kuwa taarifa ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu mashambulizi katika kituo cha usambazaji wa chakula Jabalya ilishindwa kulitaja Hamas moja kwa moja.
Amekataa madai kwamba Israel inazuia misaada ya kibinadamu au inawanyima raia chakula, akisema hali ya kibinadamu Gaza ni thabiti.
“Zaidi ya malori 600 ya misaada yanaingia Gaza kila siku na tangu kusitishwa kwa mapigano, zaidi ya tani milioni 1.8 za chakula zimefikishwa katika eneo hilo, kiwango ambacho, kinazidi mahitaji ya kila mwezi yaliyowekwa na shirika la Umoja wa MAtaifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).