Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mafunzo ya STEM yawezesha vijana Zanzibar kuongezea thamani zao la mwani

Kundi la wasichana wadogo darasani katika mradi wa STEM UNICEF Tanzania, wakikusanya kitambuzi cha kielektroniki kwa ajili ya kiwanda.
© UNICEF Tanzania Kupitia ushirikiano kati ya serikali ya Canada na UNICEF Tanzania, ProjektInspire na vituo vya STEM vinawapa vijana ujuzi wa uandishi wa programu za kompyuta (coding), masomo ya kidijitali na STEM ili kujiandaa kwa fursa za siku zijazo.

Mafunzo ya STEM yawezesha vijana Zanzibar kuongezea thamani zao la mwani

Utamaduni na Elimu

Je, ingekuwaje kama kila kijana kutoka visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania angeweza kugeuza zao la mwani kuwa suluhisho la kiuchumi la kesho yake? Hilo ndilo lengo mradi wa shirika la kiraia la ProjeKt Inspire kupitia programu yake ya Girls in STEM, au Wasichana kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati, unaoungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa ufadhili wa  Canada.

Kupitia warsha wa siku tatu ya  masomo ya  STEM, wanafunzi wamejifunza kutumia masomo hayo kuongeza thamani ya zao la mwani na kuendeleza Uchumi wa buluu.

Mwanamke aliyevaa shati la bluu na kofia ya umbo la koni akivuna mwani katika maji ya kina kifupi kwenye kisiwa cha Zanzibar.
© Courtesy of Vincent Doumeizel Kwenye kisiwa cha Zanzibar, ongezeko la biashara ya mwani lilianza baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya viambato vya kuboresha chakula vinavyotengenezwa kwa mwani. Wajane na wanawake wasio na waume waliingia haraka katika sekta hiyo.

Kwanza utajiuliza Uchumi wa buluu ni nini? Huu ni uchumi utokanao na mazao ya baharini ambalo mwani ni mojawapo. Sasa tuendelee na video iliyoandaliwa na UNICEF inayoanza kwa kuwaonesha wanafunzi wakivuna mwani baharini kabla ya kurejea katika maabara kuuchakata na kutoa biopolima asilia.  Hizi ni molekuli zinazofanana na plastiki.

Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea vijana uwezo wa kutumia sayansi kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wa mwani na kuongeza thamani ya zao hilo. Max George ni meneja wa Projekt Inspire, anaeleza umuhimu wa mradi huu.

"Mwani ni zao muhimu sana Zanzibar. Vijana wengi wanajishughulisha na kilimo hiki, lakini pia ni zao linalowanufaisha zaidi wanawake kwani wengi wa wanaolima mwani ni wanawake. Ndio maana tumeona umuhimu wa kuwafundisha vijana wetu, na asilimia kubwa ya washiriki wa kambi hii ni mabinti."

Wavulana wawili wadogo darasani wanafanya kazi pamoja katika mradi mdogo wa kielektroniki unaohusisha waya na vipengele kwenye dawati la mbao.
© UNICEF Tanzania Kupitia ushirikiano kati ya serikali ya Canada na UNICEF Tanzania, ProjektInspire na vituo vya STEM vinawapa vijana ujuzi wa uandishi wa programu za kompyuta (coding), masomo ya kidijitali na STEM ili kujiandaa kwa fursa za siku zijazo.

Kutokana na mafunzo hayo, wanafunzi walitumia utafiti na majaribio kubuni bidhaa mbalimbali zinazotokana na mwani, wakigeuza maarifa ya darasani kuwa majawabu ya changamoto za maisha ya kila siku. Aifat K. Mwalimu ni mwanafunzi wa Sayansi ambaye ni mshiriki wa mradi huu..

"Katika darasa letu la sayansi tumetengeneza bidhaa mbili kutokana na unga wa mwani. Tulitengeneza sabuni na shampoo. Hivyo tunaweza kujiita wajasiriamali na wanasayansi kwa sababu tumegundua namna ya kutengeneza bidhaa zinazoweza kutumika majumbani na katika jamii."

Mbali na kutengeneza bidhaa, baadhi ya washiriki walibuni majawabu ya kidijitali ya kuwasaidia wakulima wa mwani kupata taarifa muhimu na masoko kwa urahisi zaidi. Sofia S. Suleiman ni mwanafunzi wa teknolojia, anaeleza jinsi wanavyotumia akili mnemba kuendesha shughuli za utafiti wa kilimo cha mwani. 

"Tumebahatika kutengeneza programu tunayoiita Seaweed Farming Chatbot App, ambayo inalenga kuwasaidia wakulima wa mwani kupata taarifa za kilimo, kuboresha uzalishaji wao, pamoja na kupata masoko na wateja."

Mtu amesimama kwenye maji yasiyo na kina kirefu kwenye kisiwa cha Zanzibar, akiwa ameshika kamba ya mwani uliovunwa.
© Kwa hisani ya Vincent Doumeizel Katika kisiwa cha Zanzibar, mwani sasa ni rasilimali ya tatu kwa ukubwa.

Changamoto ya ukaushaji wa mwani baada ya mavuno pia lilipata jawabu kupitia ubunifu wa kiteknolojia ulioanzishwa na wanafunzi hao. Ilham F. Bakari, Mwanafunzi wa uhandisi anaeleza zaidi.

"Tumeona wakulima wa mwani wanapata changamoto kubwa baada ya kuvuna kwa sababu hali ya hewa hubadilika mara kwa mara. Kwa hiyo tumetengeneza kifaa kinachoitwa Smart seaweed dry Machine kitakachosaidia kukausha mwani kwa ufanisi."

Washiriki wengine walitumia maarifa ya hisabati na uchambuzi wa takwimu kubaini vipindi vinavyofaa zaidi kwa kilimo cha mwani ili kuongeza uzalishaji mwaka mzima kama anavyoeleza Mwanafunzi huyu wa somo la hisabati Raudhat J. Said..

Katika miezi 12 ya mwaka, kila mwezi una hali ya hewa tofauti. Kwa hiyo, tumetumia hisabati ili kubaini ni mwezi gani kati ya miezi hiyo unafaa zaidi kwa ajili ya kulima na kuvuna zao la mwani."

Kupitia mradi huu, vijana wamejifunza kufikiri kwa ubunifu, kufanya kazi kwa ushirikiano na kutumia sayansi kutatua changamoto za jamii.