Fahamu kuhusu ugonjwa wa Homa ya ini unaoweza kukaa mwilini kwa miaka bila dalili
Virusi vya Homa ya ini vinaweza kukaa mwilini kwa muda mrefu bila kuonesha dalili, huku vikiendelea kuliharibu ini na kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa saratani.
Onyo hilo limetolewa na Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, nchini Tanzania Dkt. Swalehe Kitabu Pazi, katika siku hii ya maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani tarehe 28 Julai inayolenga kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa huo.
Homa ya ini B na C yaweza kusababisha saratani
Katika mahojiano maalum na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Dkt. Pazi amesema homa ya ini husababishwa na virusi vya aina mbalimbali, lakini virusi vya homa ya ini B na C ni miongoni mwa vinavyoweza kusababisha madhara makubwa visipotibiwa.
“Unaweza ukahisi kwamba uko salama, lakini ugonjwa unaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika mwili,” amesema.
Ameeleza kuwa kugundua ugonjwa mapema humwezesha mgonjwa kuanza kufuatiliwa na kupata matibabu kabla ini halijapata madhara makubwa.
Saratani ya ini inapogunduliwa katika hatua za mwanzo inaweza kutibiwa, lakini mgonjwa akichelewa kufika hospitalini huenda akabaki na tiba za kupunguza makali ya ugonjwa na kurefusha maisha pekee.
Jinsi ya kulinda afya ya ini
Dkt. Pazi amewataka wananchi kujikinga dhidi ya maambukizi ya homa ya ini kwa kufanya ngono salama na kuepuka matumizi ya vifaa vinavyoweza kuwa na damu ya mtu mwingine.
Pia amesisitiza umuhimu wa wanawake wajawazito kupima, kwa kuwa virusi vya homa ya ini B vinaweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Kupunguza au kuacha matumizi ya pombe na sigara pia kunaweza kusaidia kulinda ini dhidi ya madhara.
Chanjo inapatikana kwa ajili ya kuzuia homa ya ini B, huku homa ya ini C ikiwa na dawa zinazoweza kuitibu.
Wananchi wahimizwa kwenda kupima
Hospitali ya Taifa Muhimbili inaungana na Umoja wa Mataifa kayika kuadhimisha Siku ya Homa ya Ini Duniani hii leo, tarehe 28 Julai, katika hospitali hiyo jijini Dar es Salaam.
Wananchi wamehimizwa kutumia fursa hiyo kupima na kufahamu afya ya ini, hata kama hawana dalili zozote.
“Kupima kunasaidia kugundua tatizo katika hatua za mwanzo. Ukijua afya yako, inakuwa rahisi kupata matibabu yanayofaa,” amesema Dkt. Pazi.