Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM: Waliofungwa kwenye vituo vya utapeli mtandaoni ni waathirika, si wahalifu

Mchoro wa mikono miwili ikiwa imeshikwa pingu ikiandika kwenye simu nyingi za mkononi zinazoonyesha aikoni za mawasiliano na barua pepe, zinazowakilisha uhalifu wa kulazimishwa na ulaghai mtandaoni.
© UNODC Mamia ya maelfu ya watu duniani kote wamesafirishwa kinyume cha sheria na mitandao ya uhalifu na kulazimishwa kushiriki katika ulaghai wa mtandaoni.

IOM: Waliofungwa kwenye vituo vya utapeli mtandaoni ni waathirika, si wahalifu

Wahamiaji na Wakimbizi

Baada ya ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na dawa za kulevya na uhalifu UNODC kuonesha hapo jana jinsi biashara ya utapeli mtandaoni inavyozidi kukua duniani, sasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, limefafanua kuwa nyuma ya biashara hiyo kuna maelfu ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu wanaolazimishwa kufanya uhalifu kwa vitisho na ukatili.

IOM inasema wahanga hao mara nyingi huvutwa kupitia matangazo ya fursa za ajira yanayoonekana halali, yakiahidi ajira nzuri nje ya nchi. Wakifika huko, hunyang’anywa nyaraka zao, hufungiwa katika maeneo yenye ulinzi mkali na kulazimishwa kuendesha utapeli mtandaoni kwa kutumia vitisho, madeni ya kulazimishwa na ukatili. Walioponea katika mazingira hayo wameeleza kukumbwa na mateso, unyanyasaji wa kingono, njaa na kufungiwa peke yao.

Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope, amesema watu wanaofungiwa katika vituo hivyo ni waathirika wa biashara haramu ya binadamu na si wahalifu. “Watu waliokwama katika vituo vya utapeli ni waathirika wa biashara haramu ya binadamu wanaolazimishwa kufanya uhalifu kwa ukatili, vitisho na shinikizo. Wanastahili kulindwa, si kuadhibiwa,” amesema.

Ameongeza kuwa kukabiliana na biashara hiyo kunahitaji ushirikiano wa kimataifa. “Ni lazima tushirikiane kuwasaidia manusura, kuwazuia walanguzi na kuziba mianya inayotumiwa na mitandao hii ya uhalifu. Hakuna nchi inayoweza kukabiliana na tatizo hili peke yake,” amesema Pope.

Dawati lenye karatasi, SIM kadi kwenye trei, kebo ya USB iliyozungushwa, na daftari lililoandikwa kwa mkono.
© UNODC/Laura Gil Meza katika kituo cha ulaghai na utapeli imesalia tupu baada ya mamlaka nchini Ufilipino kukivamia.

Kwa mujibu wa takwimu mpya za UNODC, hasara zinazotokana na utapeli mtandaoni katika maeneo ya Asia Mashariki, Kusini-Mashariki mwa Asia, Australia na New Zealand pekee zilifikia kati ya dola bilioni 88.3 na 114.1 mwaka 2025. 

IOM inaeleza kuwa mamia ya maelfu ya watu bado wanaaminika kushikiliwa katika vituo vya utapeli katika eneo hilo wakilazimishwa kufanya kazi kwa niaba ya makundi ya uhalifu wa kupangwa.

Kati ya mwaka 2022 na 2025, IOM imetoa msaada kwa zaidi ya waathirika 3,500 wa biashara hiyo kutoka nchi 39, wengi wao wakitoka Indonesia, India, Sri Lanka, Ethiopia, Kenya na Bangladesh. Kwa kutambua ongezeko la tatizo hilo, shirika hilo pia limezindua mkakati mpya wa Asia na Pasifiki wa miaka 2026–2030, unaolenga kuimarisha ulinzi wa waathirika, kuzuia biashara haramu ya binadamu, kuimarisha ushirikiano wa mipakani na kuvunja mitandao ya wahalifu.

Kuelekea Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu tarehe 30 Julai, IOM imesisitiza kuwa kuwaokoa waathirika ni hatua ya kwanza tu. Wengi wao huhitaji msaada wa muda mrefu wa kurejea nyumbani kwa usalama, kupata huduma za afya ya akili, kurejeshewa nyaraka zao na kujenga upya maisha yao, huku shirika hilo likitoa wito kwa serikali na wadau kuongeza ulinzi kwa waathirika na kuelimisha umma kuhusu mbinu zinazotumiwa na walanguzi wa ajira.