Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wazinduliwa kulinda haki ya kusaka hifadhi

Mwanamke wa Sudan Kusini mwenye tabasamu amebeba mtoto mgongoni, amesimama mbele ya hema la UNHCR katika kambi ya wakimbizi.
© UNHCR/Blaise Sanyila Joelle, mkimbizi wa Sudan Kusini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, anatumai elimu itampatia mwanawe mustakabali bora, huku familia za wakimbizi zikijitahidi kujitegemea kwa usaidizi kutoka kwa UNHCR na wadau wake.

Mpango wazinduliwa kulinda haki ya kusaka hifadhi

Wahamiaji na Wakimbizi
  • Sauti 75 zashirikiana na UNHCR kuzindua “The Promise” kwa ajili ya wakimbizi
  • Ni pamoja na washindi wa tuzo ya amani ya Nobel
  • Ahadi yao ni pamoja na kulinda haki ya kusaka hifadhi

Watu mashuhuri 75 kutoka sekta mbalimbali duniani wameungana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kuzindua mpango unaoitwa “The Promise”, au AHADI kwa lugha ya Kiswahili ambalo ni tamko la kimataifa la mshikamano kwa wakimbizi na haki ya watu kutafuta hifadhi salama.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo Geneva, Uswisi inasema uzinduzi huo unafanyika wakati Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi wa mwaka 1951 unatimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake. Lengo kuu ni kujenga muungano mpana wa kimataifa wa kuimarisha ulinzi wa wakimbizi kuelekea Jukwaa la Kimataifa la Wakimbizi mwaka 2027

Tweet URL

Nani wanahusika?

Miongoni mwa watu 75 wa kwanza waliotia saini tamko hilo ni:

  • Waigizaji na watengenezaji filamu Cate Blanchett, Angelina Jolie na Ben Stiller
  • Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) Kirsty Coventry
  • Wafanyabiashara Mo Ibrahim, Hamdi Ulukaya na Tadashi Yanai
  • Washindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel akiwemo Malala Yousafzai, Nadia Murad, Denis Mukwege na Ellen Johnson Sirleaf
  • Sarah Mullaly, Askofu Mkuu wa Kanisa la kianglikana huko Canterbury, Uingereza

“The Promise” “Ahadi” inasisitiza nini?

Waliotia saini tamko hilo wameahidi:

  • Kulinda haki ya kutafuta hifadhi
  • Kuwajumuisha wakimbizi katika jamii zinazowapokea
  • Kuanza kutafuta majawabu mapema katika migogoro inayosababisha watu kukimbia
  • Kuimarisha msaada kwa nchi na jamii zinazowahifadhi wakimbizi
  • Kukuza huruma, mshikamano na hatua za vitendo kwa wakimbizi

Kaulimbiu ya tamko hilo ni:

“Hatua, huruma na mshikamano hadi kila mtu awe salama.”

Kwa nini mpango huu umezinduliwa?

UNHCR imesema dunia inakabiliwa na viwango vya juu vya watu waliolazimika kukimbia makazi yao kutokana na: vita; ghasia, mateso na ukandamizaji

Kwa sasa, zaidi ya wakimbizi milioni 41 duniani bado wamekimbia makazi yao, huku nchi zinazowapokea zikibeba mzigo mkubwa na mifumo ya hifadhi ikikabiliwa na changamoto za rasilimali.

Maafisa katika Palais des Nations huko Geneva wanasaini Mkataba Unaohusiana na Hali ya Wakimbizi mwaka wa 1951. Walioketi mezani ni, kutoka kushoto kwenda kulia, Margaret Kitchen, John Humphrey, Knud Larsen, na Dkt. GJ Van Heuven Goedhart, huku wajumbe na waangalizi wengine wakiwa wamesimama nyuma yao.
Picha ya UN/ES Mataifa kumi na mawili yalitia saini Mkataba wa Wakimbizi huko Geneva mnamo Julai 1951.

Kauli ya Mkuu wa UNHCR

Kamishna Mkuu wa UNHCR, Barham Salih, akizungumzia miaka 75 ya Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi amesema umeokoa mamilioni ya maisha kwa miongo kadhaa.

“Miaka 75 iliyopita dunia ilitoa ahadi ya kulinda watu wanaolazimika kukimbia makazi yao. Wajibu wetu sasa ni kuhakikisha ahadi hiyo inaendelea kuishi kwa vizazi vijavyo,” amesema Salih.

Ameongeza kuwa mataifa yanapaswa kushirikiana katika kutekeleza mkataba huo ili kulinda wakimbizi huku yakidumisha usalama na utulivu wa jamii.

Muendelezo wa kampeni

UNHCR imesema itaendelea kuwakaribisha watu binafsi na mashirika mbalimbali kujiunga na “The Promise” katika kipindi cha maandalizi kuelekea Jukwaa la Kimataifa la Wakimbizi 2027.