Aliyekuwa mkimbizi, Wenyen Gabriel, awa mchezaji wa kwanza wa mpira wa kikapu wa kulipwa kuteuliwa kuwa Balozi-Mwema wa UNHCR
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) leo limetangaza kumteua mchezaji wa mpira wa kikapu wa kulipwa Msudan Kusini, Wenyen Gabriel, mwenye umri wa miaka 29 kuwa Balozi-Mwema. Gabriel ndiye mchezaji wa kwanza wa mpira wa kikapu kuteuliwa kuwa Balozi-Mwema wa UNHCR.
Alizaliwa Khartoum, Sudan, na wazazi waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vinaendelea nchini mwao Sudan Kusini. Baadaye yeye na familia yake walikimbilia Misri kabla ya kuhamishiwa nchini Marekani alipokuwa na umri wa miaka miwili.
Baadaye, Gabriel alipata ufadhili wa masomo ya mpira wa kikapu katika Chuo Kikuu cha Kentucky na akaendelea kucheza katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA), akizichezea timu zikiwemo Los Angeles Lakers na Portland Trail Blazers. Mwaka 2024 aliwakilisha Sudan Kusini katika Michezo ya Olimpiki ya Paris, ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kushiriki Olimpiki. Huo ulikuwa wakati wa kipekee kwa mtu aliyeanza maisha akiwa mkimbizi baada ya wazazi wake kulazimika kuikimbia nchi yao.
Amekuwa akiunga mkono UNHCR
Gabriel amekuwa akiunga mkono wakimbizi na UNHCR tangu mwaka 2022, aliporejea kwa mara ya kwanza Sudan Kusini kushuhudia hali ya kibinadamu na kutetea haki za watu waliolazimika kukimbia makazi yao. Tangu wakati huo, ameendelea kutumia umaarufu wake na uzoefu wake wa zamani kama mkimbizi kuongeza uelewa na kuunda fursa kwa jamii zilizolazimika kuhama duniani kote, hasa kwa vijana kupitia michezo.
Akikubali jukumu lake jipya, Gabriel amesema, “familia yangu ililazimika kukimbia vita na migogoro. Maisha yetu yalibadilika kwa sababu tulipata usalama. Niliweza kwenda shule, kucheza michezo na kuota kuhusu mustakabali wangu. Sasa, kama Balozi wa Nia Njema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, ninaweza kutetea haki za watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao na kuikumbusha dunia kwamba hakuna anayechagua kuwa mkimbizi. Kuwa mkimbizi kunapaswa kuwa sura moja tu ya maisha, na kamwe si mwisho wa simulizi lako.”
UNHCR yajivunia
Akimkaribisha Gabriel kama Balozi-Mwema, Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi, amesema, “tunapoadhimisha miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi wiki hii, simulizi ya Wenyen ni ukumbusho wenye nguvu wa umuhimu wa ulinzi kwa wakimbizi. Anaonesha uthabiti na uwezo mkubwa wa watu wanaolazimika kukimbia makazi yao wanapopata usalama na fursa ya kujenga upya maisha yao. Kupitia kazi yake ya kibinadamu na kujitolea kwake kwa vijana kupitia michezo, Wenyen tayari analeta mabadiliko. Tunajivunia kumkaribisha katika familia ya UNHCR.”
Kabla ya kutangazwa rasmi katika nafasi hiyo, Gabriel alirejea Maban, Sudan Kusini, ambako alikutana na wakimbizi waliokimbia mzozo nchini Sudan. Alisikiliza simulizi za familia zilizokimbia ghasia na changamoto wanazoendelea kukabiliana nazo. Zaidi ya wakimbizi 220,000 kutoka Sudan wanaishi pamoja na jamii zinazowahifadhi katika eneo la Maban.
Wakati wa ziara hiyo, Gabriel alizindua uwanja mpya wa mpira wa kikapu katika Kambi ya Wakimbizi ya Doro na kuendesha mafunzo ya mpira wa kikapu kwa vijana wakimbizi na wa jamii zinazowahifadhi, akisisitiza nafasi ya michezo katika kuleta matumaini, ushirikishwaji na fursa.
Akikumbuka ziara yake, Gabriel anasema, “nchini Sudan Kusini nilikutana na akina mama waliokimbia mabomu nchini Sudan na kuendelea kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine wakitafuta tu usalama. Mama mmoja aliniambia kwamba sasa anatamani tu kulala kwa amani, bila hofu na bila kusikia sauti za ndege zisizo na rubani angani. Pembeni yake alikuwa binti yake mwenye umri wa miaka minane ambaye bado ana ndoto ya kuwa daktari. Nyakati kama hizi zinanikumbusha kwa nini kazi ya UNHCR ni muhimu na kwa nini hatupaswi kamwe kuacha kuwasaidia watu waliolazimika kukimbia makazi yao.”
Uteuzi wa Gabriel unakuja wakati UNHCR na wadau wake duniani kote wanaadhimisha miaka 75 ya Mkataba wa Wakimbizi tarehe 28 Julai, wakithibitisha upya ahadi yake ya kudumu ya kulinda watu waliolazimika kukimbia makazi yao na kuwasaidia kujenga upya maisha yao.
Gabriel anasema, “kuwa Balozi-Mwema wa UNHCR wakati dunia inaadhimisha kumbukumbu hii ni jambo lenye maana kubwa kwangu. Mimi ni ushahidi hai kwamba ahadi ya Mkataba wa Usalam kwa Wakimbizi inaweza kubadilisha maisha. Ilibadilisha maisha yangu. Katika wakati ambapo ahadi hiyo inakabiliwa na vitisho, ninajitolea kusimama pamoja na wakimbizi na watu wote waliolazimika kukimbia makazi yao hadi kila mmoja atakapokuwa salama.”