Umoja wa Mataifa waonya kuhusu kuimarika kwa mgogoro wa kibinadamu nchini Ukraine
- Wataka ulinzi zaidi kwa raia kwani wanakumbwa zaidi na madhara
- Huduma za kiutu zaendelea licha ya mashambulizi yanayoendelea
- Mnepo wa mashirika ya kiutu usitafsiriwe ni kukubali hali ilivyo
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa raia kote nchini Ukraine wanaendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita iliyoanza Februari 2022 baada ya Urusi kuvamia taifa hilo, huku mashambulizi ya mara kwa mara yakisababisha vifo na majeruhi, kuharibu makazi, kuvuruga huduma muhimu, na kuathiri miundombinu ya misaada ya kibinadamu.
Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Misaada ya Dharura, (OCHA) Tom Fletcher, Kaimu Naibu Mkuu wa ofisi hiyo, Indrika Ratwatte, amesema mashirika ya kibinadamu yanaendelea kujitolea kuwasaidia mamilioni ya watu licha ya mazingira yanayozidi kuwa magumu na hatari.
Raia wanaendelea kuathirika zaidi
Ametaja mashambulizi ya hivi karibuni ambayo yamekuwa na madhara kwa jamii katika maeneo mbalimbali ya Ukraine, ikiwemo Odesa, Mykolaiv, Kharkiv, Dnipro, Sumy, Zaporizhzhia, Kyiv, Donetsk, na Kherson, ambako raia wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi ya makombora, ndege zisizo na rubani au droni, na mashambulizi ya angani.
Kwa mujibu wa Ratwatte, nyumba zimeharibiwa, huduma za umeme na maji zimekatizwa, na maghala ya misaada ya kibinadamu yameharibiwa, hali inayopunguza upatikanaji wa misaada inayookoa maisha.
“Tuna wasiwasi kuhusu taarifa za vifo na majeruhi kwa raia nchini Urusi, ingawa amesisitiza kuwa bado hatujaweza kuthibitisha taarifa hizo kwa njia huru.”
Mwitikio wa kibinadamu unaendelea kukabiliana na changamoto zinazoongezeka
Kadri hali ya usalama inavyobadilika, mashirika ya kibinadamu yanaendelea kurekebisha shughuli zake ili yaweze kuwafikia watu wanaohitaji msaada.
Juhudi zinazoendelea ni pamoja na:
- Kuhamisha maghala na vifaa vya misaada katika maeneo salama.
- Kurekebisha njia za misafara ya misaada ili kuongeza usalama.
- Kusambaza chakula, makazi ya dharura, huduma za afya, msaada wa fedha taslimu, na huduma za msaada wa kisaikolojia na kijamii.
- Kushirikiana kwa karibu na wahudumu wa ndani ili kuwafikia wananchi walio katika mazingira hatarishi.
Umoja wa Mataifa pia umesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mipango ya kibinadamu inayowezesha raia kuhamishwa kwa usalama na kuruhusu misaada ya kuokoa maisha kuwafikia wanaohitaji zaidi.
Maandalizi kwa majira ya baridi kali
Wakati mashirika ya kibinadamu yakiendelea kushughulikia dharura za kila siku, pia yanafanya maandalizi kwa ajili ya majira ya baridi yanayokuja.
Umoja wa Mataifa umezindua Mpango wake wa Kila Mwaka wa Mwitikio wa Majira ya Baridi, unaojumuisha:
- Kuhifadhi mapema vifaa vya dharura.
- Kusaidia ukarabati wa nyumba zilizoharibiwa.
- Kurejesha miundombinu muhimu.
- Kusaidia jamii zilizo katika mazingira magumu kujiandaa kwa kipindi cha baridi.
Ratwatte ameonya kuwa jamii ambazo tayari zimechoshwa na miaka ya mzozo haziwezi kuachwa zikabiliane na majira mengine ya baridi bila msaada.
Kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu
Afisa huyo amesisitiza tena kwamba pande zote zinazohusika katika mzozo huo zinapaswa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu kwa kuwalinda raia na wahudumu wa misaada ya kibinadamu, kulinda miundombinu ya kiraia, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia watu wote wanaohitaji.
Ratwatte ametamatisha akisema ingawa mashirika ya kibinadamu yataendelea kubadilisha utendaji wao kulingana na mazingira na kutoa misaada ya kuokoa maisha, hayawezi kuchukua nafasi ya wajibu wa pande zinazohusika katika mzozo wa kuwalinda raia.
"Dhamira na ustahimilivu wa wahudumu wa misaada ya kibinadamu haupaswi kutafsiriwa kama kukubaliana na hali hizi," amesema, akisisitiza kuwa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu si jambo la hiari.