Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhamasishaji dhidi ya Ebola unatusaidia – Asema mkazi wa Bunia, DRC

Mfanyakazi wa misaada aliyevaa fulana nyekundu anazungumza na kundi la watu wanne, wakiwemo wanawake wawili na watoto wawili, katika mazingira ya vijijini yenye miti ya ndizi nyuma.
© OCHA Mfanyakazi wa misaada wa OCHA aendesha kampeni ya uhamasishaji kuhusu Ebola na jamii ya wenyeji nchini DRC.

Uhamasishaji dhidi ya Ebola unatusaidia – Asema mkazi wa Bunia, DRC

Afya
  • Timu ya Mratibu Mkuu wa UN dhidi ya Ebola yapiga kambi Bunia
  • Waelimishaji wa kujitolea watoa elimu mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba
  • Wataka wananchi waache ‘kupapasa’ maiti

Habari njema kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) kuhusu Ebola ya virusi vya Bundibugyo ni kwamba watu zaidi ya 500 waliokuwa wameambukizwa ugonjwa huo wamepona.

Mfanyakazi wa Msalaba Mwekundu akizungumza na wanaume wawili katika jamii ya vijijini nchini DRC.
© OCHA Mfanyakazi wa Msalaba Mwekundu anajadili uelewa wa Ebola na wanajamii huko Ituri, DRC.

Ingawa Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la afya duniani, WHO, unasema bado hali ni tete hususan mjini Bunia, jimboni Ituri ambako ndio kitovu cha mlipuko wa sasa uliotangazwa mwezi Mei mwaka huu, harakati za kuelimisha umma, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa zinazaa matunda.

Mathalani katika mtaa wa Ujio wa Heri ulioko kitongoji cha Kasegwa mjini Bunia, wahudumu wa afya wa kujitolea wanaofanya kazi chini ya shirika la Msalaba Mwekundu wamefanya kazi ambayo hata wakazi wake wanakiri kuwa imesaidia.

Mkazi mmoja wa eneo hilo, Monique Fambwe amemweleza Priscilla Lecomte aliye kwenye timu ya Mratibu Mkuu wa Ebola wa Umoja wa Mataifa, Julien Harneis iliyoko Bunia kwamba “sasa tunapata kuelewa jinsi maambukizi yanavyofanyika na jinsi ya kujikinga.”

Mwanamke mwenye tabasamu katika mazingira ya vijijini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati wa kampeni ya uhamasishaji kuhusu Ebola huko Ituri.
© OCHA Monique Fambwe akizungumza na Priscilla Lecompte kuhusu Ebola.

Watoa huduma hao wa kujitolea ni pamoja na Alphonce Lukana ambaye ameieleza timu hiyo kuwa “tunatembelea watu kwenye nyumba zao na kuwahimiza jinsi ya kukabiliana na Ebola. Tunagundua kuwa tangu Ebola itangazwe hapa nchini mwetu watu wengi hawajui. Kuna watu wanajiuliza uliza unaweza kuwa ugonjwa gani? Sawa, dalili ya ule ugonjwa inakuwa sawa na dalili ya malaria. Watu hawaelewi vizuri, hawafahamu. Inabidi sisi sasa sisi kuwatembelea na kuwaelimisha kuhusu maambukizi na jinsi ya kutambua.”

Kisa cha familia iliyopata maambukizi bila kufahamu

Bwana Lukana ananukuu kisa kimoja kilichosimuliwa na Bi. Fambwe kwamba, “jirani yao familia yote ilifariki dunia bila kufahamu ni ugonjwa gani. Ilikuwa ni mwanzoni waliambukizwa, mmoja akafariki dunia na mwingine vivyo hivyo mpaka familia imeisha.”

Hiyo imesababisha uoga na ndio maana “huyo mama ametueleza kuwa anakataza wajukuu zake wasitoke nje.”

Amezungumzia changamoto za baadhi ya watu kuwafukuza wahudumu wa afya akisema, “Kuna familia fulani fulani pale ambapo tunapita watu wanatafuta kutuzuia. Lakini tunajikaza tu kwa sababu najua katika jamii ni lazima tuweze tu kufundisha watu zaidi. Watu waweze kujua kama ugonjwa ule ni Ebola ni nini unaambukizwa namna gani wanaweza kutambua namna gani? Na zaidi tunatia mkazo kuhusu matibabu hospitalini. Mtu yeyote akipata homa asijifiche nyumbani. Lazima aondoke, aende hospitali apate matibabu kwani huko ndio kuna wataalamu.”

Mwanamume aliyevaa fulana nyeupe yenye nembo ya 'CROIX-ROUGE' amesimama nje katika mazingira ya vijijini, pengine wakati wa kampeni ya uhamasishaji kuhusu Ebola huko Ituri, DRC.
© OCHA Alphonce Lukana, Mfanyakazi wa kujitolea wa Msalaba Mwekundu amesimama wakati wa kampeni ya uhamasishaji kuhusu Ebola katika jamii ya vijijini huko Ituri, DRC.

Hofu ya Bwana Lukana ni kwenye mazishi ya wanaofariki dunia hivyo akisema, “Tunafundisha jamii ziache kupapasa maiti. Mtu akifariki katika familia tuogope kwa sababu hii ndio inatoa virusi sana sana. Ndio maana tunajua watu wanafariki katika familia moja. Unasikia watu wanakufa watano, hadi saba.”

Tukirejea kwa Bi. Fambwe yeye baada ya kupata elimu kutoka kwa wahudumu wa afya anasema, “tunashukuru mafundisho ya kila namna. Wametupatia mafundisho ya jinsi ya ujikinga. Tunashukuru.”

Ana matumaini kuwa Ebola itatokomezwa akisema, “kwa msaada wa Mungu atuwezeshe ili tuishi katika yetu.”