Maambukizi ya VVU yanaongezeka, janga la UKIMWI latishia kurejea
Kupungua kwa ufadhili wa kimataifa, kudhoofika kwa huduma za kinga na kuongezeka kwa sheria zinazobagua makundi yaliyo hatarini kunahatarisha mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI -VVU. Bila hatua za haraka, zaidi ya watu milioni tatu wanaweza kuambukizwa kufikia mwaka 2030.
Dunia ipo katika hatari ya kushuhudia kurejea kwa kasi kwa janga la UKIMWI, huku maambukizi mapya ya VVU yakiongezeka katika baadhi ya maeneo na mamilioni ya watu wakikosa matibabu.
Onyo hilo limetolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI, UNAIDS, katika ripoti maalumu iliyozinduliwa hii leo wakati wa Mkutano wa 26 wa Kimataifa kuhusu UKIMWI unaofanyika Rio de Janeiro, Brazil, kuanzia tarehe 27 hadi 31 Julai 2026.
Ripoti inaonesha kuwa mwaka 2025 pekee, watu milioni 1.2 waliambukizwa VVU na wengine 570,000 walifariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI.
Ingawa idadi hiyo ni miongoni mwa viwango vya chini zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka 30, UNAIDS inaonya kuwa mafanikio yaliyopatikana ni dhaifu na yanaweza kupotea haraka.
Maambukizi yaongezeka katika nchi 21
Kwa mujibu wa ripoti hiyo maambukizi mapya ya VVU yaliongezeka katika kanda tatu na nchi 21 mwaka 2025.
Kati ya watu milioni 41 wanaoishi na VVU duniani, takribani milioni tisa hawakuwa wanapata matibabu. Karibu nusu ya watoto wote wanaoishi na VVU pia hawakuweza kupata dawa za kufubaza virusi.
Bila hatua za haraka kufikia malengo ya mwaka 2030, zaidi ya watu milioni tatu wanaweza kuambukizwa VVU katika kipindi cha miaka minne ijayo.
Hata hivyo, mafanikio katika baadhi ya maeneo yanaonesha kuwa janga hilo linaweza kudhibitiwa. Nchi saba ambazo ni Benin, Eswatini, Kenya, Lesotho, Nepal, Rwanda na Zimbabwe zimepunguza maambukizi mapya kwa karibu asilimia 80 tangu mwaka 2010.
Nchi nyingine 11 zimefikia malengo ya matibabu ya 95-95-95.
Dawa mpya zaja, lakini wengi hawawezi kuzifikia
Sayansi imeleta matumaini mapya kupitia dawa za kuzuia VVU zinazotumiwa kwa sindano kila mwezi au kila baada ya miezi sita. Vidonge vinavyotumiwa kila mwezi pia vipo katika hatua za mwisho za majaribio.
Lakini changamoto kubwa ni gharama na kutopatikana kwa dawa hizo kwa watu wengi wanaozihitaji.
“Mafanikio ya kisayansi yanatupatia nyenzo ambazo vizazi vilivyopita vingeweza kuziota tu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Winnie Byanyima
Hata hivyo Mkuu huyo wa UNAIDS ametahadharisha kuwa“Ubunifu usiofikiwa na watu si ubunifu, ni ukosefu wa haki. Kipimo cha mafanikio si kama dawa zipo, bali kama watu wanaozihitaji wanaweza kuzipata kwa bei wanayoweza kumudu.”
UNAIDS inakadiria kuwa watu milioni 20 wanahitaji dawa za kuzuia maambukizi ili kuleta athari kubwa katika kudhibiti VVU. Hata hivyo, dawa ya sindano ya lenacapavir kwa sasa inawafikia watu elfu chache tu.
Ufadhili wa VVU washuka kwa kiwango kikubwa
Misaada ya maendeleo kutoka nchi mbalimbali ilipungua kwa asilimia 23 mwaka 2025 hili ni anguko kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa.
Ufadhili wa kimataifa kwa ajili ya VVU ulipungua kwa dola bilioni 1.5, kutoka dola bilioni 8.8 mwaka 2024 hadi dola bilioni 7.3 mwaka 2025. Hicho ni kiwango cha chini zaidi katika karibu miaka 20.
Nchi nyingi maskini zenye mzigo mkubwa wa VVU barani Afrika zilikuwa zinategemea misaada ya nje kwa zaidi ya asilimia 90 kuendesha programu zao.
“Enzi ya kutegemea misaada ya kimataifa imekwisha,” amesema Byanyima. “Nchi haziwezi kusubiri wala kurudi nyuma. Dunia lazima irekebishe haraka mfumo wa fedha uliovunjika na kuharakisha marekebisho ya madeni ili serikali ziweze kuwekeza katika mambo muhimu zaidi ambayo ni afya, elimu na mustakabali wa watu wao.”
Katika baadhi ya nchi, ufadhili wa kondomu umepunguzwa kwa zaidi ya asilimia 90. Huduma zinazoongozwa na jamii pia zimepungua kwa kiasi kikubwa, zikiwemo zinazowahudumia wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao, wafanyakazi wa ngono na manusura wa ukatili wa kijinsia.
Ubaguzi na sheria kandamizi zahatarisha mapambano
UNAIDS pia imeonya kuwa kuongezeka kwa sheria zinazoharamisha au kubagua makundi yaliyo katika hatari kubwa ya kupata VVU kunawafanya watu waogope kutafuta huduma.
Mwaka 2026, nchi 168 ziliharamisha biashara ya ngono, 152 ziliharamisha umiliki wa kiasi kidogo cha dawa za kulevya, 66 ziliharamisha mahusiano ya watu wa jinsia moja na 14 ziliharamisha watu waliobadili utambulisho wa kijinsia.
“Huwezi kumaliza UKIMWI huku ukiwafanya wahalifu watu wanaoishi na VVU na wale walio katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa,” amesema Byanyima.
“Watu wanapoogopa kukamatwa, kufanyiwa ukatili au kubaguliwa, wanakaa mbali na huduma za VVU. Haki za binadamu si jambo lililo tofauti na mapambano dhidi ya VVU ni msingi wa mafanikio yake.”
Byanyima amesema kumaliza UKIMWI bado kunawezekana, lakini kutahitaji mshikamano mpya wa kimataifa, ufadhili endelevu na kulindwa kwa haki za binadamu.
“Chaguo lililo mbele yetu ni wazi: kurudi nyuma na kuhatarisha kurejea kwa janga, au kufikiri upya, kujenga upya na kusimama pamoja kumaliza UKIMWI kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030.”