Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atamatisha ziara yake Syria, ataka vikwazo vyote dhidi ya taifa hilo viondolewe

Katibu Mkuu UN akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus, huku bendera UN ikiwa nyuma na maikrofoni nyingi kutoka kwa mashirika mbalimbali ya habari.
UN/ Ali Haj Sulieman Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus nchini Syria, mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili Julai 26, 2026

Guterres atamatisha ziara yake Syria, ataka vikwazo vyote dhidi ya taifa hilo viondolewe

Amani na Usalama
  • Apongeza hatua za kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Syria
  • Ataka vikwazo vyote viondelewe ili Syria iweze kujinasua kiuchumi na kimaendeleo
  • Akutana na Rais Al-Sharaa na kusisitiza ushirikishwaji wa makundi yote kwenye michakato yote
Tweet URL

Mwishoni mwa ziara yake ya mshikamano nchini Syria, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amekaribisha hatua zilizochukuliwa ambazo zimesababisha kulegezwa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Syria, akibainisha kwamba hatua hizo zimefungua fursa mpya za kufufua uchumi wa nchi hiyo. Hata hivyo, amesisitiza kwamba, "vikwazo hivi vyote vinapaswa kuondolewa mara moja."

Pia ameitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za kisiasa zinazoendelea, ushirikiano wa kiuchumi, na msaada wa vitendo ili kuisaidia Syria kujijenga upya baada ya miaka ya migogoro.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo mwishoni mwa ziara yake ya siku mbili nchini Syria—ikiwa ni ziara ya kwanza ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo katika kipindi cha miaka 17—Guterres ameeleza kipindi cha mpito kuwa ni "wakati wa kipekee katika historia ya watu," na fursa ya kufungua "ukurasa mpya" ambapo Wasyria wote wanaweza kujiona kuwa sehemu ya mustakabali wa nchi yao.

Mkutano wake na Rais Al-Sharaa wa Syria

Jana Jumamosi Julai 25, Katibu Mkuu wa alikutana na Rais wa Syria, Ahmad Al-Sharaa, mjini Damascus, ambapo viongozi hao walijadili hatua zilizopigwa katika kipindi cha mpito wa kisiasa na namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Syria.

Katika mkutano huo Guterres amekaribisha maendeleo yaliyofikiwa katika mchakato wa mpito wa kisiasa nchini Syria na kusisitiza "umuhimu wa kuendeleza kasi hiyo kupitia ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii."

Guterres amesema "ushiriki jumuishi ni muhimu ili kujenga Syria yenye amani, utulivu na ustawi kwa manufaa ya wananchi wote wa Syria."

Ushirikiano wa Syria na Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu na Rais Al-Sharaa pia wamejadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Syria ili kusaidia mchakato wa mpito wa kisiasa, pamoja na juhudi za kuokoa uchumi na kujenga upya nchi baada ya miaka ya mgogoro.

Aidha, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza tena dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kuheshimu na kuunga mkono mamlaka kamili ya Syria, uhuru wake, umoja wa taifa na mipaka yake inayotambuliwa kimataifa.

Pia ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu ukiukwaji unaofanywa na Israel wa Makubaliano ya Kutenganisha Vikosi ya mwaka 1974, akisisitiza umuhimu wa kulinda utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati.

Katibu Mkuu alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa mshirika wa karibu wa wananchi wa Syria na mamlaka za nchi hiyo katika kipindi hiki muhimu cha mpito kuelekea amani na maendeleo endelevu.

Mwanamume mwenye ndevu na upara aliyevaa miwani anaelekeza juu huku akizungumza na mwanamume mzee mwenye nywele za kijivu katika suti na tai nyekundu, mbele ya ukuta mweupe wenye picha na maandishi ya Kiarabu.
UN/ Ali Haj Sulieman Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres (kulia), akipatiwa maelezo wakati wa ziara yake katika eneo la Saydnaya, lilipo gereza la kijeshi lenye sifa mbaya lililokuwa likiendeshwa na utawala wa zamani wa Assad.

Ziara kwenye gereza la Sednaya

Wakati wa ziara hiyo ametembelea maeneo kadhaa ikiwemo gereza la Sednaya ambako Guterres amesema kwamba wakati wa ziara yake, ameshuhudia "maendeleo ya kipekee katika mpito wa kisiasa", licha ya mateso ambayo nchi imepitia.

Amesema kuwa alishtushwa sana alipotembelea gereza hilo ambako amesema "makumi ya maelfu ya watu wameuawa na kuteswa."

"Lakini pia niliona ustahimilivu, ujasiri na azma... Nilihisi matumaini makubwa ya kuwepo kwa usalama na utulivu kwa wote."

Amesema kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono juhudi za kuimarisha uwajibikaji, haki ya mpito, haki za binadamu, maridhiano, kujenga imani kati ya jamii mbalimbali, na kuhakikisha ushiriki wa maana wa Wasyria wote, wakiwemo wanawake na vijana.

Kulaani ukiukaji wa Israel

Guterres amesisitiza tena kulaani kwake ukiukaji unaoendelea wa Israel dhidi ya Makubaliano ya Kutenganisha Vikosi ya mwaka 1974. "Naulaani vikali ukiukaji unaoendelea wa Israel dhidi ya Makubaliano ya kutofanya mashambulizi ya mwaka 1974, pamoja na ukweli kwamba Milima ya Golan kwa asili ni eneo la Syria," amesema.

Ziara kwenye msikiti wa Umayyad mjini Damascus

Jana, Katibu Mkuu ametembea msikiti wa Umayyad mjini Damascus. Katika video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, amesema, "nyuma yangu kuna msikiti wa Umayyad mjini Damascus. Si mahali pa ibada pekee, bali pia ni alama ya Syria kama njia panda ya ustaarabu mbalimbali. Sitaisahau kamwe kwamba mmoja wa wanazuoni wa dola ya Umayyad alichangia kuanzishwa kwa dola ya Córdoba, ambao ulikuwa na nafasi muhimu katika kusambaza ustaarabu na maarifa hadi bara la Ulaya."