Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wataka ukiukwaji wa mamlaka ya Syria ukome

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa mkutano, huku bendera UN ikionekana nyuma.
UN Syria Katibu Mkuu UN António Guterres akihutubia waandishi wa habari mjini Damascus, Syria.

Umoja wa Mataifa wataka ukiukwaji wa mamlaka ya Syria ukome

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema Umoja wa Mataifa unasimamia kwa msimamo thabiti kuheshimiwa kwa mamlaka, uhuru, umoja na ukamilifu wa eneo la Syria, akisisitiza kuwa uvamizi wa kijeshi ndani ya eneo la Syria na ukiukwaji wa mipaka yake haukubaliki na unapaswa kukoma.

Akizungumza jijini Damascus, Syria, Guterres amesema vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyoko katika eneo la Golan vinaendelea kutekeleza wajibu wake wa kupunguza athari za hali hiyo kwa wananchi na kusaidia jamii zilizoathirika, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kuhakikisha sheria za kimataifa zinaheshimiwa.

Amesema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina jukumu la msingi la kulinda amani na usalama duniani, lakini limeendelea kukabiliwa na mgawanyiko wa kisiasa pamoja na matumizi ya kura ya turufu ambayo mara nyingi yamezuia hatua zinazohitajika kutekeleza sheria za kimataifa.

Gari jeupe la kivita UMOJA WA MATAIFA liko katika kituo cha ukaguzi katika Milima ya Golan.
UNDOF/Wolfgang Grebien Kituo UNDOF huko Golan mnamo 2013. (faili)

Miinuko ya Golan ni sehemu ya Syria

Katibu Mkuu amesema msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Miinuko ya Golan haujabadilika, akisisitiza kuwa eneo hilo linatambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa sehemu ya Syria.

Amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kutetea msimamo huo katika vyombo vyake na kuhimiza jumuiya ya kimataifa kuheshimu sheria za kimataifa na mipaka inayotambuliwa kimataifa.

Aidha amesema, “kile ambacho ni cha Syria ni cha Syria na hakiwezi kuchukuliwa”

Ujenzi wa Syria unahitaji mshikamano wa kimataifa

Katibu Mkuu amesema hakuna nchi inayotoka katika zaidi ya muongo mmoja wa vita inaweza kujijenga peke yake, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za Syria za kujijenga upya.

Amesema msaada huo unapaswa kusaidia kufufua uchumi, kurejesha huduma muhimu na miundombinu, kupanua fursa za ajira na kuwezesha wakimbizi pamoja na watu waliokimbia makazi yao kurejea kwa hiari, kwa usalama na kwa heshima.

Katibu Mkuu Guterres amesema kuwa “kuisaidia Syria kujijenga upya si suala la kibinadamu pekee, bali pia ni uwekezaji katika maendeleo, amani na utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati,”

Amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuendelea kuunga mkono mchakato wa mpito wa kisiasa, uandishi wa katiba ya kudumu na kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki kulingana na vipaumbele vya wananchi na serikali ya Syria.