Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP yatumia mafunzo ya ufundi stadi kudumisha amani nchini Tanzania

Kundi la vijana wakisherehekea wakiwa na vyeti katika hafla ya uwezeshaji wa UNDP nchini Tanzania.
© UNDP Tanzania Vijana washiriki mafunzo ya UNDP ya ufundi stadi kudumisha amani nchini Tanzania.

UNDP yatumia mafunzo ya ufundi stadi kudumisha amani nchini Tanzania

Na Rashid Malekela
Amani na Usalama
  • Kazi ninayoifanya ina uhusiano mkubwa na amani, kwa sababu bila amani siwezi kufanya kazi yangu kwa uhuru
  • Kabla ya kuja hapa nilikuwa mama wa nyumbani tu lakini sasa nimejua kupika vyakula mbalimbali, nafurahia pia mapishi.

Hizi ni kauli za vijana nchini Tanzania walionufaika na mafunzo kupitia Mradi wa Dumisha Amani kwa Maendeleo Endelevu unaopatia vijana mafunzo ya stadi za kazi sambamba na amani. Makala hii inafafanua zaidi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP, nchini Tanzania kupitia mradi wake wa Dumisha Amani kwa Maendeleo Endelevu awamu ya pili, unaotekelezwa kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo kupitia Ofisi ya Rais -Maendeleo ya Vijana, limeendelea kutumia mafunzo ya ufundi stadi kama njia ya kudumisha amani na kuwajengea uwezo vijana kiuchumi. Rashid Malekela, balozi kijana wa UNDP Tanzania alihudhuria mafunzo hayo na kutuandalia mada hii kwa kina.

Kutoka mkoani Kigoma, Magharibi mwa Tanzania, jumla ya vijana 60 wakiwemo wakike 38 na wakiume 22, wamehitimu mafunzo ya siku 14 ya ufundi stadi na ujasiriamali yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kujiajiri, kuongeza tija kwenye shughuli zao za kila siku na muhimu zaidi kuwa mabalozi wa utatuzi wa migogoro, ujenzi wa amani na maadili katika jamii.

Mpishi wa kike jikoni la kitaalamu anaonyesha keki mbalimbali zilizopambwa kwenye kaunta ya chuma cha pua.
© UNDP Tanzania Ebiphina Paul, Mpishi kijana ambaye ni mmoja wa vijana washiriki wa mafunzo ya UNDP Tanzania ya stadi kwa vijana.

Ndani ya mafunzo hayo yaliyohitimishwa Julai 18 mwaka huu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi, VETA, mkoani Kigoma, vijana hao 15 kwa kila fani, wamepatiwa ujuzi kwenye fani za ubunifu wa mitindo na ushonaji wa mavazi, ufundi bomba, mapishi, na umeme wa majumbani.

Baada ya shamrashamra za hafla ya ugawaji vyeti kwa wahitimu, nini mtazamo wa wanufaika wa mafunzo haya? Mmoja wa wahitimu wa fani ya mapishi ni Baby Robert.

"Kabla ya kuja hapa nilikuwa mama wa nyumbani tu. Baada ya kupata mafunzo, cha kwanza kabisa nimejua kupika vyakula mbalimbali, nafurahia pia mapishi. Cha pili, nimefungua mgahawa tayari nyumbani, baada ya kushiriki mafunzo namshukuru Mungu, nimeongeza wateja. Nimekuwa napika chakula kizuri kinachovutia, chenye radha. Mimi kama mwanamke najivunia nimepata kazi inaniingizia kipato kinakidhi mahitaji yangu mimi na mwanangu."

Ernest Mussa ni mhitimu wa fani ya ubunifu wa mitindo na ushonaji wa mavazi, kazi yake ina uhusiano gani na amani katika jamii? 

"Kazi ninayoifanya ina mahusiano makubwa na amani, kwa sababu ninapokuwa nafanya shughuli zangu kwa kuwepo na amani na mimi nafanya kwa uhuru Zaidi, ila kama hakuna amani, nitakuwa nafanya kazi kwa mashaka na hofu kubwa. Kwa sababu bila amani kwangu mimi ni changamoto na sitoweza kuelewana kabisa na wateja. Kupitia Dumisha Amani nimejifunza mengi, kwanza nimeboresha ufundi wangu niliyokuwa nao, pia nimejifunza kudarizi, kuweka maua kwenye vitambaa."

Vijana nchini Tanzania wanashiriki katika warsha ya mafunzo ya ujuzi UNDP inayolenga ushonaji na utengenezaji wa nguo.
© UNDP Tanzania Vijana wa Tanzania washiriki katika warsha ya mafunzo ya ujuzi wa kushona yanayofadhiliwa na UNDP.

Kwa upande wake, Mabisi Yusuph, ambaye pia amejifunza ubunifu wa mitindo na ushonaji wa mavazi, anasisitiza umuhimu wa elimu kwa vijana.

"Kikubwa sana ambacho nimejifunza kwanza kabisa kuhusiana na neno amani, nimejifunza kwamba kumbe amani ni kitu kikubwa sana mtu anachotakiwa awe nayo. Mwanzo nilipokuwa sijafundishwa kuhusiana na neno amani, nilikuwa nachukulia jambo la kawaida tu. Kumbe ni jambo la muhimu sana ili niweze kufanya hata shughuli zangu kama mimi fundi wa nguo. Changamoto ambazo nahisi zinasababisha vijana wanakosa amani: kwanza hawana elimu. Kwa hiyo kukosekana kwa elimu ndiyo kunasababisha vijana wanaingia kwenye hiyo migogoro na kukosekana kwa amani."

Katika fani ya ufundi bomba, Jackson Thobias amedhamiria kuwa balozi wa amani mitaani.

"Moja ya faida ambayo nitatoka nayo hapa ni kuwafundisha vijana wenzangu ambao wapo mtaani kuhusu suala la amani. Kwanza tunatakiwa tuwe na amani ya moyo na kila kitu katika utendaji wako wa kazi. Hivyo inakupelekea kuaminika kwa jamii yako ambayo inakuzunguka, ni namna gani watu wanaweza kukupa kazi. Ukiwa na amani, hata kazi zako zinakuwa zinanyooka."

Msajili na Mratibu wa mafunzo ya ufundi stadi kutoka VETA Kigoma, Edward Elias, anafafanua mchakato wa kuwapata vijana hao.

"Programu hii imewagusa vijana, vijana ambao walikuwa wameshahitimu mwaka mmoja, miwili, mitatu nyuma, lakini tumewaita tena baada ya kuona kwamba baada ya kuhitimu bado wengine hawajaweza kujishikiza, hawajaweza kuajiriwa, lakini wako wengine ambao walikuwa wanafanya shughuli zao tu binafsi. Kwa hiyo tumewaita ili kuja kuongezea tena maarifa katika ujuzi wao, katika fani zao. Tunaamini kabisa kwa sasa hivi haya mafunzo yamekuwa chachu kiasi ya kwamba wamehamasika. Baada ya mafunzo haya sasa kila mmoja anaweza kwenda kuendeleza tena hiyo fani yake vizuri kabisa."

Mwokaji katika jikoni la kitaalamu hupanga mikate iliyookwa hivi karibuni kwenye kaunta ya chuma.
© UNDP Tanzania Godwin Otieno, Kijana Mwokaji mtaalamu wa mikate ambaye ni mmoja wa vijana washiriki wa mafunzo ya UNDP Tanzania ya stadi kwa vijana.

Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano na shirika la Global Peace Foundation Tanzania, kampuni ya Uhandisi ya Mafuta ya China, CPP, na VETA kupitia ufadhili wa Mfuko wa Amani na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, UNPDF, unalenga pia kujenga miundombinu endelevu ya kusaidia vijana. Afisa Mradi kutoka UNDP Tanzania, Josephine Sepeku, anaeleza.

"Moja ya hatua inayochukuliwa kwa ajili ya uimara huo ni utengenezaji wa ‘Youth Center’ (Kituo cha Vijana), ambapo tayari uongozi wa VETA hapa Kigoma umeshachagua eneo ambalo kituo hicho kitawekwa ili kuwasaidia hawa vijana 60 pamoja na wengine ambao hawajashiriki mafunzo. Watapatiwa vifaa mbalimbali ambavyo VETA wenyewe wameviainisha, ikiwemo upatikanaji wa kompyuta pamoja na gharama mbalimbali kulingana na kozi zilizotolewa."

Amesema kwa hiyo, "UNDP tutaendelea kusaidia kupitia ufadhili wa Serikali ya China kupitia UNPDF katika kuendelea na suala hili la kudumisha amani kwa maendeleo endelevu nchini Tanzania. Sababu ya kuunganisha amani na mafunzo ya amali ni kwamba wanaweza wakawa na ajira na ujuzi, ila bila kuwa na amani ya ndani kama nidhamu ya kuweza kuhudumia wateja vizuri, inaweza ikasababisha migogoro na migongano."

Hadi sasa mradi huu umewafikia vijana 240 kutoka Tanzania bara, katika mikoa ya Kigoma, Lindi, Mtwara na Ruvuma, ambapo kwa kila mkoa vijana 60 wamepatiwa mafunzo ya ufundi stadi na kudumisha amani kwa Maendeleo Endelevu.