Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka lithiamu hadi nikeli: Jinsi Umoja wa Mataifa unavyosaidia nchi kunufaika zaidi na madini ya kimkakati

Mchimbaji wa kiume aliyevaa kofia ngumu amesimama kati ya safu za vifaa vya umeme katika mgodi wa chini ya ardhi.
© UN Kazakistani Mchimbaji madini akijiandaa kwa kazi huko Kazakhstan.

Kutoka lithiamu hadi nikeli: Jinsi Umoja wa Mataifa unavyosaidia nchi kunufaika zaidi na madini ya kimkakati

Amani na Usalama
  • Argentina na lithiamu
  • DRC na utajiri wa madini lukuki kama kobalti
  • Kazakhstani na madini ya kimkakati
  • Zambia jamii za wenyeji nazo zinashirikishwa ili nazo zinufaike na madini

Mwelekeo wa dunia kuelekea matumizi ya nishati safi unasababisha ongezeko kubwa la mahitaji ya madini muhimu kama vile lithiamu, nikeli, kobalti na shaba.

Hata hivyo, uchimbaji wa madini hayo ni hatua ya mwanzo tu. Duniani kote, Umoja wa Mataifa unasaidia nchi kuhakikisha kuwa rasilimali hizi zinachangia kuunda ajira zenye staha, kulinda mazingira na kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika, badala ya kunufaisha minyororo ya usambazaji ya kimataifa pekee.

Argentina: Kuweka jamii katikati ya maendeleo ya sekta ya lithiamu

Argentina ina mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi duniani za lithiamu, jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa wasambazaji muhimu wa malighafi kwa utengenezaji wa betri za magari ya umeme na mifumo ya nishati mbadala.

Umoja wa Mataifa unasaidia kuhakikisha kuwa wananchi wa maeneo yanayozalisha lithiamu wanashiriki kikamilifu katika maamuzi kuhusu maendeleo ya sekta hiyo. Unaratibu majadiliano kati ya serikali, makampuni, wafanyakazi na jamii za asili ili kwa pamoja kushughulikia masuala kama ulinzi wa mazingira na upatikanaji wa fursa za kiuchumi.

Aidha, Umoja wa Mataifa unasaidia serikali za majimbo kuboresha mipango ya kifedha ili sehemu kubwa ya mapato yatokanayo na lithiamu ibaki katika jamii za wenyeji. Pia unasaidia kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali na kuhamasisha ushiriki mkubwa wa wanawake katika sekta hiyo.

Wachimbaji madini wa kienyeji hubeba magunia makubwa ya madini kwenye kilima chenye miamba katika mgodi wa Mudere katika eneo la Kivu Kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© Adobe Stock/Erberto Zani Kobalti inachimbwa huko Rubaya, mashariki mwa Congo, eneo linalodhibitiwa na wanamgambo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo: Kubadilisha utajiri wa madini kuwa maendeleo ya kiuchumi

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huzalisha takriban asilimia 70 ya kobalti yote duniani, madini muhimu katika utengenezaji wa betri nyingi zinazoweza kuchajiwa tena kwa ajili ya magari ya umeme na mifumo ya kuhifadhi nishati.

Umoja wa Mataifa unasaidia kuhakikisha kuwa utajiri huo wa madini unachochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi. Msaada huo unahusisha kuimarisha sera za umma, kukuza biashara zinazowajibika, na kuwezesha biashara za wenyeji kushiriki katika minyororo ya thamani ya betri na magari ya umeme inayozidi kukua.

Indonesia: Kuongeza thamani ya nikeli ndani ya nchi

Indonesia ni mzalishaji mkubwa wa nikeli duniani, madini muhimu kwa utengenezaji wa betri nyingi za magari ya umeme.

Badala ya kutegemea zaidi usafirishaji wa malighafi nje ya nchi, Indonesia inawekeza katika kuongeza uzalishaji wa bidhaa zenye thamani zaidi ndani ya nchi.

Lori kubwa la kubeba mizigo la manjano linasafirisha vifaa kwenye barabara ya vumbi katika eneo la mgodi wa nikeli, huku vifaa vingine vya uchimbaji madini na udongo uliochimbwa ukionekana nyuma.
© Adobe Stock/Mirwanto Lori linasafirisha vifaa kwenye mgodi wa nikeli nchini Indonesia.

Umoja wa Mataifa unaunga mkono juhudi hizo kwa kusaidia kuboresha viwango vya uzalishaji viwandani, kuhimiza matumizi ya teknolojia safi zaidi, na kuongeza uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi.

Pia unasaidia kuimarisha usalama na afya kazini katika sekta ya madini, kukuza stadi za kijani  au zisizoharibu mazingira ambazo zinahitajika katika uchumi unaobadilika, na kuwezesha Indonesia kubadilishana uzoefu na nchi nyingine zinazozalisha madini kupitia ushirikiano wa Kusini-Kusini kuhusu uchimbaji endelevu na usimamizi wenye uwajibikaji wa rasilimali.

Kazakhstan: Kufanya uchimbaji madini kuwa safi na wenye uwajibikaji zaidi

Kazakhstan inaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta yake ya madini muhimu huku mahitaji ya kimataifa ya rasilimali hizo yakiongezeka.

Umoja wa Mataifa unasaidia kuboresha usimamizi wa minyororo ya usambazaji wa madini muhimu kwa kusaidia kuoanisha mifumo ya kitaifa na viwango vya kimataifa, pamoja na kutambua na kudhibiti hatari zinazotokana na uhalifu, rushwa na ukosefu wa uwajibikaji.

Msaada huo pia unajumuisha kuboresha usalama migodini na mazingira ya kazi, kuhimiza biashara kuwajibika kwa kuzingatia Kanuni Elekezi za Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu, na kuchunguza njia za kurejesha madini yenye thamani kutoka kwenye taka za vifaa vya kielektroniki ili kupunguza hitaji la uchimbaji mpya.

Zambia: Kuchimba fursa mpya za ajira kwa wananchi

Rasilimali nyingi za madini za Zambia zina mchango mkubwa katika mpito kuelekea matumizi ya nishati safi. Umoja wa Mataifa unasaidia kuhakikisha kuwa sekta ya madini pia inaleta ajira mpya, kuimarisha biashara za wenyeji na kuinufaisha jamii.

Msaada huo unahusisha kuandaa mkakati wa kitaifa wa maendeleo ya stadi katika sekta ya madini, kuwaandaa wafanyakazi kwa ajira katika minyororo ya thamani ya madini na betri, na kusaidia biashara ndogo na za kati kushiriki katika minyororo mipya ya usambazaji wa magari ya umeme.

Aidha, Umoja wa Mataifa unafanya kazi na wachimbaji wadogo ili kuboresha usalama kazini, kuimarisha ulinzi wa mazingira na kusaidia urasimishaji wa shughuli zao.

Jamii za wenyeji pia zinashirikishwa katika kufuatilia athari za kimazingira za shughuli za uchimbaji madini kwa kushirikiana na serikali, vyuo vikuu na makampuni ya uchimbaji. Ushirikiano huo unasaidia kujenga imani na kuongeza uwazi katika utekelezaji wa miradi ya uchimbaji madini.

Maudhui ya makala hii yameandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Maendeleo