Madini ya kimkakati: Je ni nini?
- Kwa nini muhimu hivi sasa ?
- Rasilimali zilizojificha zinazoendesha mustakabali wa nishati safi
- Kwa nini madini ya kimkakati yamekuwa kitovu cha siasa za dunia?
Kila gari la umeme, mtambo wa kuzalisha umeme kwa upepo, paneli ya nishati ya jua au sola na simu janja hutegemea madini yanayochimbwa ardhini.
Kadri mataifa yanavyoharakisha mpito kuelekea matumizi ya nishati safi isiyotegemea nishati ya kisukuku, yaani mafuta yanayochimbwa ardhini kwa kupasua miamba, mahitaji ya madini kama vile lithiamu, kobalti, nikeli, shaba na grafaiti yanaongezeka kwa kasi.
Kwa nchi nyingi, hali hii inaleta fursa kubwa ya kukuza uchumi.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo ushindani wa kumiliki rasilimali hizo umechochea migogoro, rushwa, uharibifu wa mazingira na ukiukaji wa haki za binadamu.
Wiki hii Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linauliza swali hili la msingi:
Je, madini yanayoendesha mpito wa nishati ya kijani yanaweza pia kuwa msingi wa amani na maendeleo endelevu?
Kwa Muhtasari
Kwa nini sasa?
Mahitaji ya madini muhimu yanaongezeka kwa kasi kubwa huku nchi zikiongeza matumizi ya nishati jadidifu na teknolojia za betri.
Kwa nini yana umuhimu?
Bila madini haya, dunia haiwezi kufanikisha mpito wa kuelekea nishati safi na kuachana na matumizi ya mafuta ya kisukuku yanayochochea mabadiliko ya tabianchi.
Changamoto ni ipi?
Usimamizi dhaifu unaweza kuyageuza madini haya kuwa chanzo cha migogoro, rushwa na uharibifu wa mazingira.
Umoja wa Mataifa unalenga nini?
Kuhakikisha utajiri unaotokana na madini unawanufaisha wananchi badala ya kufadhili migogoro na vurugu.
Maswali matano muhimu
1. Madini ya kimkakati ni nini?
Madini muhimu ni malighafi zinazohitajika katika teknolojia nyingi za kisasa, zikiwemo:
- Betri za magari ya umeme
- Mitambo ya kuzalisha umeme kwa upepo
- Paneli za nishati ya jua
- Mifumo ya usambazaji wa umeme
- Simu janja na vifaa vya kielektroniki
Bila madini haya, teknolojia nyingi za nishati safi zisingewezekana.
2. Yanapatikana wapi?
Akiba kubwa ya madini muhimu ipo katika maeneo mbalimbali ya Afrika, Amerika ya Kusini na sehemu za Asia.
Kwa nchi zinazozalisha madini hayo, ni fursa kubwa ya:
- Kuzalisha ajira
- Kupanua uchumi
- Kuongeza mapato ya serikali
Hata hivyo, mafanikio yanategemea jinsi rasilimali hizo zinavyosimamiwa.
3. Kwa nini mahitaji yanaongezeka kwa kasi?
Mpito wa dunia kuelekea nishati safi unaendelea kuimarika.
- Gari la umeme linahitaji takribani madini mara sita zaidi kuliko gari la kawaida.
- Mitambo ya upepo iliyoko baharini hutumia madini karibu mara 13 zaidi kuliko mitambo ya kuzalisha umeme inayotumia gesi.
- Mahitaji ya madini mengi muhimu yanatarajiwa kuongezeka hadi mara tatu ifikapo mwaka 2030.
Wachambuzi wengi sasa wanalinganisha umuhimu wake wa kimkakati na nafasi ambayo mafuta ya kisukuku yalikuwa nayo katika karne ya ishirini.
4. Je, uchimbaji wa madini si hatari kwa mazingira?
Uchimbaji wa madini ni muhimu, lakini usiposimamiwa ipasavyo unaweza kuwa na athari kubwa kwa mazingira.
Uchimbaji usiodhibitiwa unaweza kusababisha:
- Ukataji holela wa misitu
- Uchafuzi wa maji
- Kupotea kwa bioanuwai
- Uharibifu wa ardhi
- Kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi
Aidha, maeneo mengi yenye madini hayo yapo karibu na jamii za Wenyeji na mifumo ikolojia iliyo katika hatari.
Changamoto si kama madini yachimbwe au la, bali ni jinsi ya kuyachimba kwa uwajibikaji na uendelevu.
5. Kwa nini Baraza la Usalama linajadili suala hili?
Kwa muda mrefu, rasilimali za asili zimekuwa zikihusishwa na migogoro.
Baraza la Usalama linachunguza wasiwasi kwamba:
- Makundi yenye silaha yanadhibiti migodi yenye madini yenye thamani.
- Uchimbaji haramu unafadhili migogoro.
- Mitandao ya uhalifu inanufaika kupitia biashara ya magendo ya madini.
- Utawala dhaifu unachochea ukosefu wa utulivu.
Swali kubwa ni iwapo ongezeko la mahitaji ya madini muhimu duniani litaongeza mvutano wa kisiasa kati ya mataifa, au litakuwa chachu ya amani na maendeleo.
Ujumbe muhimu wa Umoja wa Mataifa
"Dunia inayotumia nishati jadidifu ni dunia yenye mahitaji makubwa ya madini ya kimkakati." Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres