Njaa duniani yapungua, lakini Afrika bado inaongoza kwa idadi kubwa ya watu wenye njaa
- Mwelekeo wa sasa si sahihi kufanikisha SDGs ifikapo 2030
- Afrika sasa ni bara lenye idadi kubwa zaidi ya watu wenye njaa duniani.
- Ukosefu wa lishe bora husababisha utapiamlo na utipwatipwa
Njaa duniani imepungua kwa mwaka wa tatu mfululizo mwaka 2025, ishara kwamba hatua za kukabiliana na tatizo hilo zinaanza kuzaa matunda. Hata hivyo, maendeleo hayo bado ni madogo, hayajasambaa kwa usawa kati ya maeneo mbalimbali ya dunia, na hayatoshi kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uhakika wa Chakula na Lishe Duniani 2026 (SOFI 2026) iliyotolewa leo Roma, nchini Italia, na mashirika matano ya Umoja wa Mataifa hii leo ikisema, takribani watu milioni 645 walikabiliwa na njaa mwaka 2025. Hii ni punguzo la karibu watu milioni 14 ikilinganishwa na mwaka 2024, na milioni 43 chini ya kiwango cha mwaka 2022.
Mashirika hayo matano ni; lile la Chakula na Kilimo, (FAO), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), la kuhudumia watoto, (UNICEF), Mpango wa Chakula (WFP), na la Afya Duniani (WHO).
Afrika bado hali ni tete
Ingawa hali imeimarika katika maeneo kama Asia pamoja na Amerika ya Kusini na Karibea, Afrika bado ndiyo eneo lenye idadi kubwa zaidi ya watu wenye njaa.
Ripoti inaonesha kuwa:
- Takribani watu milioni 309 barani Afrika walikuwa wanakabiliwa na njaa mwaka 2025.
- Idadi hiyo imeizidi Asia, ambayo sasa ina watu milioni 292 wenye njaa.
- Sehemu ya watu wanaokabiliwa na njaa Afrika imepungua kidogo kutoka asilimia 20.3 mwaka 2024 hadi asilimia 20.0 mwaka 2025, jambo linaloonesha dalili za kuimarika.
- Hata hivyo, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu, Afrika sasa ndiyo bara lenye idadi kubwa zaidi ya watu wenye njaa duniani.
Changamoto bado zipo
Akizugumzia ripoti hiyo, Mchumi Mkuu wa FAO, Máximo Torero, ametaja visababishi vya njaa kuwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya nishati na mbolea kutokana na migogoro ya kimataifa na matukio ya hali mbaya ya hewa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, akisema “Mambo haya yanaweza kusababisha zaidi hali ya uhaba wa chakula katika miaka ijayo.”
Ripoti pia inaonya kuwa lishe bora bado haiwezi kumudiwa na mabilioni ya watu duniani, hali inayochangia kuongezeka kwa uzito kupita kiasi na unene uliokithiri sambamba na tatizo la utapiamlo.
Kwa kule kwenye mafanikio, Maximo anasema, “mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kulindwa kwani bado yako katika hatari ya kurudishwa nyuma na migogoro pamoja na mishtuko ya kiuchumi na tabianchi.”
Nini kinapendekezwa?
FAO inapendekeza hatua kadhaa za kuimarisha uhakika wa chakula, zikiwemo:
- Kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya kilimo, ikiwemo maghala, mifumo ya kuhifadhi kwa ubaridi, usafirishaji na barabara za kufikisha mazao sokoni.
- Kupunguza upotevu wa mazao, hasa matunda, mboga na vyakula vingine vyenye thamani kubwa ya lishe.
- Kuweka sera zinazosaidia uzalishaji na upatikanaji wa vyakula vyenye lishe bora badala ya kuelekeza ruzuku kwenye vyakula vya wanga pekee.
- Kuongeza kasi ya hatua za kukabiliana na athari za migogoro na mabadiliko ya tabianchi ili kulinda uzalishaji wa chakula na maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa FAO, mchanganyiko wa uwekezaji katika miundombinu na sera zinazopunguza gharama za vyakula vyenye lishe bora ni muhimu ili kupunguza njaa, utapiamlo pamoja na ongezeko la uzito kupita kiasi duniani, hususan barani Afrika.
Soma ripoti nzima SOFI 2026 hapa
Bofya hapa kupata takwimu za SOFI2025