Wavamizi wote waondoke DRC ili sisi ‘wakongomani’ tuendeleze nchi yetu – Bi. Kibuya
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasiaya Congo, DRC, shirika la kiraia la Congo Notre Avenir, yaani kwa kiswahili, Congo Mustakabali wetu linapigania haki ya amani kwa wanawake ili hatimaye waweze kushiriki katika kuendeleza familia zao kwa kushirikiana na familia zao, wakati huu ambapo mapigano mashariki mwa nchi yamesababisha ukatili ikiwemo ubakaji, na hata wanaume kuacha familia zao na kwenda msituni kupigana.
Pauline Farini Kibuya, Muasisi na Mkurugenzi wa shirika hilo amefafanua kazi za shirika hilo alipohojiwa na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa jijiini New York, Marekani ambako Bi. Kibuya alifika kwa ajili ya mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70.
“Tulianzisha shirika hili baada ya kuona kuwa wanawake wengi ndio wanateseka na vita, wanashindwa kwenda kazini, wanashindwa kufanya biashara, wanashindwa kuangalia familia zao. Wengine wamebaki wajane kwa kuwa waume zao wameuawa kwenye mapigano,” amesema Bi. Kibuya.
Awali alikuwa anaishi Goma, uliokuwa mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, kabla ya kutwaliwa na waasi wa M23 na makao makuu ya muda kuhamishiwa Beni. Hivi sasa Bi. Kibuya anaishi mji mkuu wa DRC, Kinshasa.
Amezungumzia makubaliano ya amani yaliyotiwa saini jijini Washington DC nchini Marekani kati ya Rwanda na DRC kwa uratibu wa serikali ya Marekani, akisema ni matumaini yake kuwa wavamizi wanaosaidia waasi wataondoka nchini mwao, ili vita ikome.
Alipoulizwa anataka nini kifanyike ili amani ya kudumu irejee DRC, Bi, Kibuya amesema, “tunataka wavamizi waondoke, ili sisi wananchi wa DRC tubakie wenyewe na tuendeleze nchi yetu.”
Sikiliza mahojiano yote hapa: