Migogoro na kusitasita kuchanja vyakwamisha upatiaji watoto chanjo muhimu
Migogoro na kusitasita kuchanja vyakwamisha upatiaji watoto chanjo muhimu
- Bila chanjo kwa watoto dunia inaweza kushuhudia mlipuko wa magonjwa yanayozuilika
- Watoto walikosa mwendelezo wa chanjo kama ya surua
- Mataifa 57 yaliripoti mlipuko wa surua 2025
Utoaji wa chanjo kwa watoto duniani umeongezeka kidogo mwaka 2025, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia watoto, UNICEF na lile la Afya, WHO. Licha ya ongezeko hilo dogo, mashirika hayo yanasema mamilioni ya watoto bado hawapati kinga muhimu kwa sababu ya migogoro, umaskini, kuhama kwa lazima na jamii kusitasita kuchanja.
Changamoto kubwa: watoto kutomaliza ratiba ya chanjo
Takwimu zinaonesha kuwa watoto milioni 13.5 hawakupata chanjo yoyote katika mwaka wao wa kwanza wa maisha. Aidha, watoto milioni 7.3 walipata chanjo ya kwanza dhidi ya Kifaduro, Dondakoo na Pepopunda (DTP) lakini hawakupata chanjo ya surua.
- Asilimia 84 pekee walipata dozi ya kwanza ya chanjo ya surua.
- Asilimia 77 walipata dozi ya pili.
- Nchi 57 ziliripoti milipuko mikubwa ya surua mwaka 2025.
Migogoro na taarifa potofu vyakwamisha chanjo
Zaidi ya nusu ya watoto ambao hawajapatiwa chanjo wanaishi katika nchi zilizoathiriwa na migogoro.
Mifano:
- Syria: Chanjo ya DTP ilishuka kwa pointi 6, huku chanjo ya surua ikishuka kwa pointi 12.
- Sudan: Ilirekodi ongezeko kubwa duniani, ambapo chanjo ya DTP iliongezeka kwa pointi 35 na chanjo ya surua kwa pointi 22.
Katika baadhi ya nchi zenye kipato cha kati na cha juu, changamoto ni kusitasita kuchanja na taarifa potofu kuhusu chanjo.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema, "Serikali na wahudumu wa afya wamechangia kurejesha viwango vya chanjo duniani baada ya kushuka kwa kiwango kikubwa wakati wa janga la coronavirus">COVID-19,"
Hata hivyo amesema, "mamilioni ya watoto walio katika mazingira hatarishi bado hawapati kinga kutokana na migogoro, kulazimishwa kuhama na umaskini. Ni lazima tuwafikie watoto wote, na turejeshe imani katika maeneo ambako imeanza kuyumba. Hakuna mtoto anayepaswa kuugua ugonjwa ambao unaweza kuzuilika kwa chanjo rahisi."
Kwa Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, "kila mtoto, awe amezaliwa katika familia tajiri au maskini, katika mazingira ya amani au ya migogoro, anastahili kupata ulinzi unaookoa maisha unaotolewa na chanjo. Chanjo ni mojawapo ya hatua zenye gharama nafuu zaidi, zinazotoa usawa zaidi na zinazotegemewa zaidi katika kulinda afya na ustawi wa watoto.”
Amekumbusha kuwa, "usalama wetu mkubwa unaanzia katika kuhakikisha kwamba kila mtu, popote anapoishi, analindwa dhidi ya magonjwa hatari ambayo yanaweza kuzuilika kupitia chanjo."
Mapendekezo
UNICEF na WHO wanatoa wito kwa serikali na wadau:
- Kuimarisha huduma za chanjo katika maeneo yenye migogoro.
- Kupambana na taarifa za uongo kuhusu chanjo.
- Kuongeza ufadhili wa programu za chanjo.
- Kuboresha mifumo ya takwimu na ufuatiliaji wa magonjwa.
Mashirika hayo yanaonya kuwa bila hatua za haraka, dunia inaweza kushuhudia ongezeko la milipuko ya magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika kwa chanjo.