Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madini ya kimkakati Afrika yanufaishe kwanza waafrika – Bi. Mohammed

Mchimbaji madini aliyevaa shati la bluu na kofia amebeba beseni la kijani begani mwake katika eneo la mgodi wa wazi nchini DRC.
© UNDP Mwanamume mmoja akifanya kazi katika mgodi wa uchimbaji madini huko DR Congo.

Madini ya kimkakati Afrika yanufaishe kwanza waafrika – Bi. Mohammed

Tabianchi na mazingira

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, ametoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya haraka ili kuhakikisha nchi zinazoendelea ikiwemo za bara la Afrika zenye utajiri wa madini ya kimkakati (Critical Minerals), zinapata manufaa ya haki kutokana na ongezeko la mahitaji ya madini hayo, ambayo ni msingi wa mpito wa dunia kuelekea matumizi ya nishati safi.

Akizungumza katika Mkutano wa Kwanza wa Ngazi ya Juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Madini ya Kimkakati katika kipindi cha Mpito kuelekea Nishati Safi uliofanyika Jumanne, kwenye Makao Makuu ya UN jijini New York, Marekani, Bi. Mohammed amesema kuwa licha ya Afrika kuwa na baadhi ya akiba kubwa zaidi duniani za madini yanayohitajika katika teknolojia za nishati jadidifu, bara hilo bado linapata uwekezaji mdogo na manufaa finyu ya kiuchumi.

Afrika ina madini mengi, lakini haipati manufaa yanayostahili

Naibu Katibu Mkkuu amesema Afrika inamiliki takribani asilimia 30 ya akiba ya madini ya kimkakati duniani, yakiwemo shaba, lithiamu, kobalti, nikeli na madini adimu  ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa magari ya umeme, paneli za sola, mitambo ya kuzalisha umeme kwa upepo na betri kubwa za kuhifadhi nishati.

Hata hivyo, amesema bara hilo hupokea asilimia 2 tu ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi, hali inayodhoofisha maendeleo ya miundombinu, ukuzaji wa wataalamu wenye ujuzi, viwanda vya uchakataji wa madini na uwezo wa kufikia masoko ya kimataifa.

Aidha, amesema kuwa ushindani unaoongezeka duniani wa kupata madini ya Afrika unachangia kuongezeka kwa migogoro, kuwahamisha wananchi kutoka makazi yao na kuzusha machafuko katika baadhi ya maeneo ya bara hilo.

Mahitaji yanaongezeka kwa kasi

  • Mahitaji kuongezeka zaidi ya maradufu ifikapo mwaka 2040 kutokana na ukuaji wa teknolojia za nishati jadidifu, magari ya umeme, akili mnemba na vituo vya kuhifadhi na kuchakata data.
  • Madini hayo ndiyo msingi wa dunia kuachana na matumizi ya nishati ya kisukuku, huku yakizidi kuwa muhimu pia katika sekta za viwanda, teknolojia za kidijitali, afya na ulinzi.

Afrika isiendelee kusafirisha malighafi pekee

Nchi zinazoendelea zenye utajiri wa madini zinapoteza fursa ya kipekee ya maendeleo kwa kuendelea kuuza madini ghafi wakati uchakataji, uongezaji thamani na faida kubwa hupatikana katika nchi nyingine.

“Jamii zinazozunguka migodi, ambazo zinapaswa kuwa wanufaika wa kwanza wa shughuli za uchimbaji na uchakataji wa madini, bado zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo, uUharibifu wa mazingira, maendeleo duni ya kiuchumi na fursa chache za ajira nje ya shughuli za uchimbaji madini,” amesema Bi. Mohammed

"Mpito wa nishati safi haupaswi kurudia dhuluma na ukosefu wa haki ulioshuhudiwa huko nyuma," amesema akipendekeza yafuatayo:

Mapendekezo

1. Kuhakikisha uchimbaji wa madini unakuwa wa haki na endelevu

2. Kujenga ushirikiano wa haki kimataifa

3. Kulinda haki za binadamu na mazingira

Soma hotuba yake hapa

Tazama video hapa