Mikopo midogo yaimarisha mnepo kwa wanawake jimboni White Nile, nchini Sudan
- Ni kupitia ubia wa UNHCR na Wakfu wa Mastercard
- Shuhuda asema sasa analipa karo za shule ya watoto bila shida
- Mwingine aweza kulipia masomo yake ya Chuo Kikuu
- Kando ya mkopo, mradi unapatia wanawake mafunzo ya usimamizi wa fedha
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kwa ushirikiano na Wakfu wa Mastercard, linaendelea kuwawezesha wanawake wakimbizi wa ndani na wenyeji katika Jimbo la White Nile nchini Sudan kujijengea uwezo wa kiuchumi kupitia Vikundi vya Kuweka na Kukopa Vijijini (VSLA).
Kupitia mikopo midogo, mafunzo ya usimamizi wa fedha na utunzaji wa akiba, wanawake hao wanaanzisha biashara ndogo, kuongeza kipato na kujenga maisha ya kujitegemea licha ya athari za vita vinavyoendelea nchini humo.
Hanan Mohammed ni shuhuda
Katika kijiji cha Mahada, wilayani Al Jabalain, Hanan Mohammed anasema kujiunga na kikundi cha VSLA kumebadilisha maisha yake.
Kabla ya hapo alitegemea vibarua vya muda visivyo na uhakika, hali iliyomlazimu kuchagua kati ya kununua chakula au kulipia karo na mahitaji ya shule ya watoto wake.
Baada ya kupata mkopo wake wa kwanza, aliweza kulipa ada na kununua sare za watoto wake. Mkopo wa pili ulimwezesha kuanzisha kibanda cha kuuza chai na kahawa kandokando ya barabara. Leo hii, mapato ya biashara hiyo yanamwezesha kukidhi mahitaji ya familia, kurejesha mkopo na kuendelea kuweka akiba.
"Watoto wangu wanapoenda shule ninapata nguvu zaidi. Sasa ninategemea kazi yangu mwenyewe, na hilo limeleta tofauti kubwa katika maisha yangu," amesema Hanan.
Mikopo midogo yamwezesha Halima kurejea Chuo Kikuu
Kwa upande wake, Halima, aliyekimbia Khartoum mji mkuu wa Sudan, baada ya vita kuzuka mwezi Aprili 2023, anasema alipoteza karibu kila kitu, ikiwemo ndoto yake ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu.
Baada ya kujiunga na kikundi cha VSLA, alipata mkopo uliomwezesha kufungua duka la kuuza nguo, bidhaa za urembo na mahitaji mengine ya kila siku.
Biashara hiyo ilikua hatua kwa hatua na sasa amemshirikisha kaka yake katika kuiendesha, huku mapato yake yakimwezesha kurejea chuoni kusomea Shahada ya Utawala wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Wad Madani, Jimbo la Al Jazirah.
"Nilikuwa na ndoto ya kurejea chuoni lakini sikuwa na uwezo wa kifedha. Sasa ninaweza kusoma na nina matumaini ya kuikuza biashara yangu zaidi siku zijazo," amesema Halima.
Vikundi vya VSLA vyajenga mnepo na mshikamano
· Vikundi vya VSLA havitoi mikopo pekee, bali huwajengea wanachama uwezo wa kusimamia fedha, kuweka akiba na kuimarisha mshikamano kati ya wakimbizi wa ndani na jamii zinazowahifadhi.
· Jimbo la White Nile linahifadhi zaidi ya wakimbizi wa ndani 480,000.
- Takribani watu milioni 13 wameyakimbia makazi yao nchini Sudan tangu vita vilipoanza Aprili 2023.
· Kupitia ushirikiano wa UNHCR na Wakfu wa Mastercard, familia zinaanzisha biashara ndogo, kuongeza kipato na kujenga upya maisha, huku wanawake kama Hanan na Halima wakijitegemea kupitia mikopo midogo.