Maji, nishati, ubunifu, ubia na miji endelevu vyapatiwa kipaumbele kwenye mkutano wa UN
Maji, nishati, ubunifu, ubia na miji endelevu vyapatiwa kipaumbele kwenye mkutano wa UN
- Maji bado ni changamoto kubwa
- Nishati jadidifu yashika kasi
- Tanzania miongoni mwa nchi zilizowasilisha tathmini ya hiari (VNR)
- Mwakilishi wa Watoto na Vijana asema hayo ni makundi yasiyo na uwakilishi wa kutosha kwenye vikao muhimu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema dunia inapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), akionya kuwa maendeleo yaliyopatikana tangu kupitishwa kwa Ajenda ya 2030 yanakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa rasilimali za kifedha.
Akifungua Kikao cha Mawaziri cha Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo Endelevu (HLPF) jijiin New York, Marekani, Guterres amesema dunia imepiga hatua katika kupunguza vifo vya watoto na wajawazito, kuongeza upatikanaji wa maji safi, usafi wa mazingira, umeme na intaneti, pamoja na kukuza matumizi ya nishati jadidifu.
Hata hivyo, amesema kasi ya maendeleo bado haitoshi kufikia malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2030.
“Ni asilimia 36 pekee ya malengo ya SDGs yanayopimika ambayo yako kwenye mwelekeo sahihi au yanapiga hatua za wastani, huku asilimia 15 yakiwa yamerudi nyuma,” amesema Guterres.
Ameeleza kuwa hadi sasa nchi wanachama zimewasilisha tathmini 401 za hiari kuhusu maendeleo, na tathmini nyingine 36 zinatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha mwaka huu, zikionesha kuwa pale kunapokuwa na utashi wa kisiasa, maendeleo yanawezekana.
1. Maji bado ni changamoto kubwa
Kuhusu Lengo la 6 la Maendeleo Endelevu linalohusu maji safi na usafi wa mazingira, Katibu Mkuu amesema mamia ya mamilioni ya watu zaidi sasa wanapata huduma hizo ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.
Hata hivyo, amesema watu bilioni 2.2 bado hawapati maji ya kunywa yanayosimamiwa kwa usalama, huku bilioni 3.5 wakikosa huduma salama za usafi wa mazingira.
Ameonya kuwa matumizi makubwa ya maji, uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi vinafanya dunia kutumia maji safi kwa kiwango kisicho endelevu, hali inayohatarisha mito, maziwa, chemichemi za chini ya ardhi na mifumo ya ikolojia ya maji.
2. Nishati safi yaendelea kukua
Katika eneo la nishati safi na nafuu, Guterres amesema nishati jadidifu sasa ndiyo chanzo cha bei nafuu zaidi na kinachokua kwa kasi zaidi katika uzalishaji wa umeme duniani.
Amesema mwaka uliopita kwa mara ya kwanza uzalishaji wa umeme kutoka upepo na jua ulizidi ongezeko lote la mahitaji mapya ya umeme duniani. Aidha, zaidi ya asilimia 90 ya uwezo mpya wa nishati jadidifu ulioongezwa duniani tayari ni nafuu kuliko mbadala wa chini kabisa wa mafuta ya kisukuku.
Pamoja na hayo, amesema “uwekezaji mwingi wa nishati safi unaelekezwa katika nchi zilizoendelea na China, huku Afrika ikipata asilimia 2 tu ya uwekezaji huo wa kimataifa licha ya kuwa na asilimia 60 ya uwezo bora wa nishati ya jua duniani.
3. Teknolojia na ubunifu kwa maendeleo
Akizungumzia viwanda, ubunifu na miundombinu, Guterres amesema teknolojia za kidijitali na akili mnemba (AI) zinaweza kusaidia kuharakisha maendeleo, kuunda ajira na kupanua huduma za umma.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watu wote wanapata teknolojia na mtandao wa intaneti, huku akitaka AI itumike kupunguza pengo la maendeleo na si kuliongeza.
4. Miji endelevu na makazi bora
Kwa upande wa miji na jamii endelevu, Katibu Mkuu huyo amesema dunia inapaswa kukabiliana na ongezeko la uhaba wa makazi na kuwekeza katika miundombinu ya mijini inayoweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametaka serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia kushirikiana katika kugharamia huduma za mijini, makazi nafuu na nafasi za kijani kwa wananchi wote.
5. Wito wa ushirikiano na ufadhili zaidi
Guterres amesema mafanikio ya SDGs hayawezi kupatikana bila ushirikiano mpana kati ya serikali, benki za maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia na vijana.
Ameonya kuwa pengo la ufadhili wa Malengo ya Maendeleo Endelevu sasa limefikia zaidi ya dola trilioni 4 kwa mwaka, huku nchi nyingi zinazoendelea zikikabiliwa na madeni makubwa na gharama za juu za mikopo.
Akihitimisha, amesema mkutano wa mwaka ujao wa kuhusu SDGs utakuwa fursa muhimu ya kuhamasisha uongozi, mshikamano na uwekezaji unaohitajika ili kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya 2030.
“Tuendelee kuifanya dira ya Ajenda ya 2030 kuwa hai, na tuhakikishe miaka iliyobaki inaleta matokeo kwa watu na sayari,” amesema Guterres.
Tathmini za kitaifa, (VNR) zawasilishwa- Tanzania yazungumza
Baada ya ufunguzi nchi zilianza kuwasilisha Tathmini ya Hiari ya Kitaifa (VNR) kuhusu utekelezaji wa SDGs, ambapo Tanzania imewasilisha tathmini ya Tatu.
Akiwasilisha tathmini hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema taifa hilo la Afrika Mashariki limeendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa SDGs licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi, msukosuko wa uchumi duniani na mvutano wa kisiasa wa kimataifa.
Ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira, kuimarika kwa huduma za afya, kuongezeka kwa fursa za elimu bora nakuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kidijitali na mageuzi ya kidijitali.
Amezungumzia jinsi mzigo wa madeni na pengo la ufadhili vinavyokwamisha SDGs akisema, "pengo la ufadhili linaloongezeka na mzigo wa madeni vinazidi kudhoofisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, kwani nchi nyingi zinazoendelea zinalazimika kuelekeza rasilimali chache zilizopo katika kulipa madeni badala ya kuwekeza katika afya, elimu, miundombinu na mahitaji mengine muhimu ya maendeleo."
Hivyo amesema “kuna haja ya mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa ili kuzipatia nchi hizo nafasi bora ya kufadhili maendeleo endelevu.”
Kuelekea mbele, Profesa Mkumbo amesema Tanzania inalenga kuunda ajira zenye tija, kuongeza kipato cha kaya, kukuza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuboresha maisha ya wananchi wote bila kumuacha mtu nyuma.