Jinsi UNHCR inavyotumia AI kusaidia wakimbizi na kuboresha shughuli zake
Jinsi UNHCR inavyotumia AI kusaidia wakimbizi na kuboresha shughuli zake
Kwa kuwa duniani kuna takriban wakimbizi milioni 42 na shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) zinafanyika katika maeneo mbalimbali duniani, (UNHCR) hukusanya na kutumia kiasi kikubwa cha data kutoka vyanzo mbalimbali.
Mbali na vyanzo hivyo, UNHCR pia hutegemea taarifa kutoka vyanzo vingi vya nje. Kuchambua na kuelewa taarifa hizi zote kunahitaji muda na utaalamu mkubwa, hata kwa wataalamu wanaozifahamu hifadhidata na zana za uchambuzi. Hata hivyo, maarifa yanayotokana na data yana uwezo mkubwa wa kuboresha ufanisi wa shughuli za shirika na kuimarisha huduma kwa watu waliolazimika kuyahama makazi yao.
Hapo ndipo teknolojia ya Akili Mnemba (AI) inapokuwa na mchango muhimu.
“Data bora inaweza kusaidia kutambua mapema hatari zinazohusiana na ulinzi, kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na dharura na kuboresha maamuzi ya kiutendaji,” anasema Mkuu wa UNHCR, Barham Salih, katika hotuba yake ya hivi karibuni kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Anaongeza kuwa, “AI ikitumika kwa uwajibikaji na kwa kuzingatia ulinzi madhubuti wa taarifa, inaweza kupunguza mzigo wa kazi za kiutawala, kuboresha uchanganuzi wa data, kuharakisha utoaji wa maamuzi na kuwapa wafanyakazi muda zaidi wa kuwalinda watu waliolazimika kukimbia makazi yao na kusaidia kupata suluhisho la kudumu.”
UNHCR inatumiaje AI?
Kama ilivyo kwa mashirika mengi duniani, matumizi ya Akili Mnemba (AI) yanaendelea kuongezeka katika shughuli za kila siku za UNHCR, yakisaidia katika kuandaa na kuboresha ripoti, kufupisha nyaraka ndefu, kutafsiri, kuandaa kumbukumbu za mikutano na kazi nyingine mbalimbali.
Hata hivyo, kinachoitofautisha UNHCR ni SHAPE, msaidizi wa akili mnemba anayefanya kazi kama jukwaa salama la ndani la shirika. SHAPE inaweza kutafuta na kuchanganua taarifa kutoka hifadhidata, miongozo na nyaraka maalum za nchi.
Mbali na uwezo wa kuchambua nyaraka ndefu, kutoa takwimu na kupendekeza viashiria pamoja na mada muhimu, SHAPE pia inaweza kuchanganua data ya kimaelezo, ikiwemo ripoti, tathmini za uwandani, simulizi za watu na taarifa nyingine zisizo na muundo maalum lakini zenye thamani kubwa katika kufanya maamuzi.
SHAPE ilitumika kusaidia uandaaji wa Mkakati wa Miaka Mingi wa UNHCR wa 2026–2029 nchini Bangladesh, ambako kuna kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, Cox’s Bazar, na ambako shughuli za kibinadamu ni miongoni mwa zilizo ngumu zaidi duniani. Ingawa taarifa zote na matokeo yaliyopatikana yalipitiwa na kuthibitishwa na wataalamu, muda uliookolewa katika mchakato wa kuandaa mkakati huo ulikuwa mkubwa.
“AI ya uzalishaji haikuharakisha tu mchakato wetu wa kuandaa nyaraka; pia ilitupatia muda tuliouhitaji zaidi wa kukutana na wakimbizi na wanajamii wenyeji, kuthibitisha mawazo yetu na kuboresha suluhisho,” anasema Hiroshi Miyauchi, Afisa Mwandamizi wa Ulinzi aliyekuwa akifanya kazi Cox’s Bazar wakati huo.
Sambamba na SHAPE, UNHCR pia inatumia zana nyingine za Akili Mnemba, kama vile Msaidizi wa Usimamizi wa Hatari, unaosaidia kutambua, kuchambua na kuonyesha hatari zinazohusiana na shughuli muhimu za shirika.
Zana hiyo inaweza kusaidia katika kupanga misheni za uwandani, kuongoza mchakato wa uteuzi wa washirika wa kusambaza msaada wa kifedha, pamoja na kusimamia minyororo ya ugavi wakati wa majanga na dharura.
Inaonekana ni nzuri kwa UNHCR. Je, kwa wakimbizi?
UNHCR tayari ina tovuti au kwa usahihi zaidi, mtandao mpana wa tovuti chini ya jukwaa la help.unhcr.org, unaowapatia wakimbizi, waomba hifadhi na watu wengine taarifa mahususi kulingana na nchi kuhusu huduma mbalimbali, kuanzia usajili na uamuzi wa hadhi ya ukimbizi, hadi makazi mapya, msaada wa kisheria, huduma za afya na elimu, makazi, pamoja na msaada kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na huduma nyinginezo.
Hatua inayofuata ni kuunganisha zana ya Akili Mnemba (AI) itakayokusanya taarifa za msingi kutoka kwa watumiaji, kama vile nchi wanayotoka na nchi wanakoomba hifadhi, kisha kuwaelekeza moja kwa moja kwenye taarifa zinazowahusu zaidi kwa lugha yao wenyewe.
Bidhaa nyingine inayotengenezwa ni 'Digital Gateway', jukwaa la kidijitali linalolenga kubadilisha namna wakimbizi wanavyopata huduma kama usajili, taarifa za kesi zao, msaada wa kifedha, pamoja na miadi na UNHCR, washirika wake na mamlaka za nchi mwenyeji.
Jukwaa hilo limekusudiwa kufanya kazi kama mfumo wa serikali mtandao, likiwa na msaidizi wa AI atakayewaongoza watumiaji kuelewa huduma zinazopatikana, haki zao na taratibu mbalimbali kwa lugha rahisi. Pia litakuwa na uwezo wa kutumia sauti na kufanya kazi katika mazingira yenye matumizi madogo ya data, ili kuongeza ufikivu kwa watu wengi zaidi.
Mfumo huo unaweza kuokoa muda kwa wakimbizi, kupunguza safari zisizo za lazima na kuwawezesha wafanyakazi wa UNHCR kuelekeza nguvu zao katika kushughulikia mahitaji magumu zaidi ya ulinzi yanayohitaji mawasiliano ya ana kwa ana.
Mbali na zana hizi za kimataifa, UNHCR pia inaendeleza mifano ya bidhaa za AI zinazobuniwa kulingana na mahitaji ya mazingira maalum. Mfano mmoja ni msaidizi wa biashara wa AI ulioundwa kuwasaidia wakimbizi na waomba hifadhi nchini Paraguay.
Kwa kuchanganua mwenendo wa soko, sheria na kanuni husika, zana hiyo inaweza kusaidia kuandaa mipango ya biashara yenye uwezekano wa kuvutia mtaji wa kuanzia, pamoja na kubuni mikakati ya biashara inayozingatia makadirio ya mapato na uendelevu wa muda mrefu.
Msaidizi huyo wa AI tayari umewasaidia wakimbizi wanaoendesha biashara mbalimbali, zikiwemo za ushonaji nguo, utengenezaji wa mishumaa na ukarabati wa vifaa vya michezo. Ofisi ya Nchi Nyingi ya UNHCR sasa inapanga kupanua matumizi ya zana hiyo katika nchi nyingine za eneo hilo.
Iwapo itafanikiwa, mfumo huo unaweza kutumika katika maeneo mengine duniani ambako wakimbizi wanapata fursa ya kuanzisha na kuendeleza biashara zao.
Nini kingine kinachotarajiwa siku zijazo?
Kutoa msaada unaofaa kwa haraka iwezekanavyo kwa wakimbizi na watu wengine waliolazimika kuyahama makazi yao wakati wa dharura ni miongoni mwa majukumu makuu ya UNHCR.
Katika siku zijazo, akili mnemba (AI) inaweza kusaidia UNHCR kutabiri migogoro inayoweza kuzuka au kurejea tena, pamoja na kutabiri matukio yanayohusiana na tabianchi kama mafuriko, ukame na majanga mengine — ikiwemo ukubwa wake na athari zinazoweza kuwapata watu. Hilo linaweza kuiwezesha taasisi kuwa tayari zaidi kuchukua hatua kwa wakati na kuelekeza rasilimali katika maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi.
Kwa mfano, fikiria zana ya UNHCR ya Country 360, ambayo ni mkusanyiko wa dashibodi zinazojumuisha zaidi ya seti 40 za data zinazosasishwa mara kwa mara. Taarifa hizo zinahusisha takwimu za idadi ya watu, uwepo wa ofisi za UNHCR, maghala ya misaada, wafanyakazi, pamoja na taarifa kuhusu upatikanaji wa hifadhi, nyaraka na viashiria vingine muhimu.
Sasa fikiria ikiwa taarifa hizo zingeweza kuunganishwa na data huria kuhusu watu na nchi kuanzia viashiria vya maendeleo ya binadamu, hali za kijamii na kiuchumi, hadi maeneo yenye migogoro.
Kwa kuongeza mifumo ya kutabiri hatari za tabianchi, taarifa za kijasusi kutoka vyanzo huria kama picha za setilaiti, pamoja na uchanganuzi wa maudhui ya mitandao ya kijamii, inawezekana kubaini mapema dalili kama uharibifu wa mazao, kupanda kwa bei za chakula, mvua zisizo za kawaida au vipindi virefu vya ukame.
Vilevile, kwa kutumia AI kubaini taarifa potofu, upotoshaji na matamshi ya chuki kwenye mitandao ya kijamii, UNHCR inaweza kutambua mapema dalili za kuongezeka kwa mivutano ya kijamii au shughuli za makundi yenye silaha.
Iwapo AI itaweza kuchakata na kuchanganua aina hizi zote za data kwa kasi na usahihi, inaweza kusaidia kujenga mifumo ya tahadhari ya mapema inayoweza kutabiri uhamishaji wa watu unaosababishwa na migogoro au mishtuko ya tabianchi kabla haujatokea.
Hilo linaweza kufungua njia kwa enzi mpya ya hatua za mapema, ambapo rasilimali za dharura na ufadhili vinaelekezwa katika maeneo sahihi kabla ya majanga kutokea, huku pia ikiimarisha uwezo wa kutabiri ukubwa unaoweza kufikiwa na migogoro ya uhamishaji wa watu.
Yote haya yanasikika vizuri. Tunasubiri nini?
Ingawa UNHCR inaendelea kubuni na kuendeleza zana mpya za akili mnemba (AI) ili kusaidia shughuli zake na kuboresha huduma kwa watu wanaowahudumia, shirika hilo linatambua umuhimu wa kuchukua tahadhari kubwa ili kuhakikisha usalama na ulinzi wa watu waliolazimika kukimbia makazi yao pamoja na watu wasio na uraia, hasa wale walio katika mazingira hatarishi zaidi ya kutengwa au kudhurika.
Kwa mfano, ni muhimu kuhakikisha kuwa kuipa AI ufikiaji wa mifumo ya ndani ya shirika hakutasababisha uvujaji wa data au taarifa nyeti zinazoweza kuhatarisha maisha, usalama au ustawi wa watu wanaohudumiwa. Taarifa hizo zinaweza kuhusisha asili ya kikabila, dini, hadhi ya kisheria, ulemavu, uanachama wa makundi fulani ya kijamii, sababu za kuomba hifadhi au sifa nyingine binafsi zinazohitaji ulinzi mkubwa.
UNHCR inaendelea kuwa makini kuhusu changamoto zinazojulikana za AI, ikiwemo uzushi wa taarifa (hallucination) hali ambapo mifumo ya AI huzalisha taarifa zisizo sahihi kama vile ukweli, takwimu, vyanzo au sheria ambazo hazipo pamoja na hatari ya mifumo hiyo kuakisi au kuimarisha upendeleo uliopo katika data iliyotumika kuifundisha, maagizo yanayopewa na hata majibu inayotoa.
Hatari hizi zinaonyesha umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya ulinzi, ikiwemo viwango vya ndani vya uwajibikaji na usimamizi endelevu wa binadamu, ambavyo vitaendelea kuwa nguzo kuu katika matumizi yote ya AI ndani ya UNHCR.
Aidha, UNHCR inashirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, serikali na kampuni za teknolojia ili kuhakikisha maendeleo na usimamizi wa AI vinaendana na kanuni za ulinzi wa wakimbizi na sheria za kimataifa za haki za binadamu. Lengo ni kuhakikisha kuwa AI inakuwa nyenzo ya kuimarisha, na si kudhoofisha, haki na ustawi wa watu wanaohudumiwa na shirika.
Mbali na kulinda watu dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyowajibika ya AI, UNHCR pia inatetea wakimbizi na watu wasio na uraia wanufaike kikamilifu na fursa zinazotokana na teknolojia hiyo. Hii ni pamoja na kupata huduma zenye ufanisi na mwitikio zaidi, pamoja na fursa za kujenga ujuzi wa kidijitali na kutumia teknolojia zinazowawezesha.
Esther Ruharara, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ni miongoni mwa wabunifu vijana watano wakimbizi waliosaidiwa na UNHCR kushiriki katika Mkutano wa AI Everything Kenya uliofanyika jijini Nairobi mwezi Mei 2026. “Kila suluhisho linalohusisha AI linapaswa kubuniwa likiwa limejikita kwa watu watakaolitumia iwe ni wakimbizi, watu wanaohusika katika minyororo yetu ya ugavi, wafanyakazi wa UNHCR katika maeneo ya operesheni au mtu mwingine yeyote,” alisema Rebeca Moreno Jimenez, Afisa wa Ubunifu wa UNHCR. “Endapo suluhisho linafanya kazi kwa watu wachache tu, halitaweza kupanuka. Watumiaji ndio wanaoelewa vyema zaidi kile kinachohitajika,” aliongeza.
Hatimaye, wakati UNHCR ikitumia uzoefu wake wa miaka 75 wa kulinda na kusaidia wakimbizi kutumia uwezo wa AI kukabiliana na changamoto za uhamishaji wa lazima, kuendeleza teknolojia na zana zitakazowezesha maono hayo kutimia kutahitaji ushirikiano mpana.
UNHCR itahitaji utaalamu, maarifa na rasilimali kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwemo kampuni za teknolojia, taasisi za utafiti, mashirika yanayoongozwa na wakimbizi, taasisi za hisani na serikali, ili kubadili uwezo wa AI kuwa suluhisho halisi na kuhakikisha teknolojia hiyo inaleta manufaa kwa mamilioni ya wakimbizi na watu wasio na uraia duniani kote.