Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lajadili ukatili wa kingono wakati wa migogoro duniani

Msichana aliyenusurika ukatili wa kingono akipokea huduma ya baada ya kujifungua akiwa na mtoto wake katika hospitali moja huko Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNFPA DRC/Junior Mayindu Msichana aliyenusurika ukatili wa kingono akipokea huduma ya baada ya kujifungua akiwa na mtoto wake katika hospitali moja huko Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Baraza la Usalama lajadili ukatili wa kingono wakati wa migogoro duniani

Wanawake

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya mjadala wa wazi leo Alhamisi Julai 8 kwa lengo la kutimiza ahadi ya sheria za kimataifa kwa manusura wa ukatili wa kingono wakati wa migogoro, huku ripoti zaidi zikionesha kuwa pande zinazopigana zinaendelea kutumia ubakaji kama silaha ya vita; vitendo vinavyoweza kuwa uhalifu wa kivita.

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono katika Migogoro, Pramila Patten,ndani ya Baraza amesema ripoti ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu imethibitisha matukio 9,788 vya ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro mwaka 2025, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya idadi iliyorekodiwa mwaka uliotangulia. Hata hivyo amesisitiza kuwa "idadi halisi ni kubwa zaidi." Amesema matukio mengi yalithibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Haiti, Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), akiongeza kuwa, "Kila tukio linaeleza simulizi mbili: kushindwa kwa mifumo kulinda raia walio hatarini na hali ya kutoadhibiwa kwa wahalifu inayowatia moyo kuendelea kutenda uhalifu huo."

Haiti

Carine Jocelyn Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Haitian Women's Collective amesema ukatili wa kingono nchini Haiti uliongezeka kwa asilimia 163 mwaka 2025. Amesema, "wanawake na wasichana wanabakwa, wanasafirishwa na kunyonywa kingono kwa utaratibu na magenge ya uhalifu," akilitaka Baraza kuimarisha utekelezaji wa vikwazo vya silaha, kuongeza msaada kwa mashirika ya wanawake ya ndani na kuwalinda manusura.

DRC

Akizungumza kwa niaba ya nchi yake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi ambayo ndio Rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu wa Julai, Judith Suminwa Tuluka, amesema ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro "si athari ya pembeni ya vita. Mara nyingi ni mbinu ya vita."

Kwamba ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro si tu janga la mtu binafsi; ni lugha ya vita yenyewe, inayotumiwa “kutisha, kudhalilisha, kuwahamisha watu, kutawala, kuvunja familia na kuharibu jamii.”

Ameeleza hatua zinazochukuliwa kukomesha kutoadhibiwa kwa wahalifu na kutoa wito wa kuimarishwa kwa ulinzi na msaada kwa watoto wanaozaliwa kutokana na ukatili huo.