Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SUDAN: Kilichobainika El Fasher kinaashiria mauaji ya kimbari; Uchunguzi wa dharura waanza El Obeid

Watu waliokimbia makazi yao hukusanyika katika kambi ya misaada nchini Sudan, huku wafanyakazi wa misaada na magari UN yakionekana nyuma.
© UNOCHA Watu waliokimbia El Fasher wanapokelewa na kupatiwa msaada wa kibinadamu Tawila Kaskazini mwa Darfur, Sudan.

SUDAN: Kilichobainika El Fasher kinaashiria mauaji ya kimbari; Uchunguzi wa dharura waanza El Obeid

Haki za binadamu

Tume huru ya Umoja wa Mataifa ya  Kuchunguza Ukweli kuhusu mzozo unaoendelea Sudan imesema mauaji ya halaiki, ubakaji wa makundi na utekaji wa kimfumo wa wanawake na wasichana unaodaiwa kufanywa na vikosi vya  Msaada wa Haraka (RSF) mjini El Fasher vinaonesha viashiria vya uhalifu wa mauaji ya kimbari. Wakati huo huo, Tume hiyo imetangaza uchunguzi wa dharura kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu mjini El Obeid, ambako kuna hofu ya kurudiwa kwa mtindo huo wa ukatili.

UN yaonya dalili za El Fasher zinajitokeza El Obeid

Ripoti mpya ya uchunguzi iliyotolewa leo mjini Geneva uswisi, imebainisha ushahidi wa mauaji, mateso, kutoweka, kuwazuilia raia kinyume cha sheria na kuwashikilia kwa lengo la kudai fidia. 

Mwenyekiti wa Tume hiyo ya uchunguzi, Mohamed Chande Othman, amesema, "Mifumo tuliyoibaini El Fasher, ikiwemo kuzingirwa kwa mji, mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia, vizuizi vya misaada ya kibinadamu na ukiukwaji mkubwa dhidi ya raia, ni onyo kali. Jumuiya ya kimataifa lazima izingatie mafunzo haya na ichukue hatua kuzuia janga jingine."

Wito wa hatua za haraka kulinda raia

Tume hiyo imeeleza kuwa zaidi ya wakazi nusu milioni pamoja na zaidi ya watu 100,000 waliokimbia makazi yao wako hatarini El Obeid kutokana na mashambulizi na kuzorota kwa hali ya usalama. Mjumbe mtaalamu Mona Rishmawi amesema, "Mafunzo ya El Fasher hayapaswi kupuuzwa... Jumuiya ya kimataifa bado ina nafasi ya kuzuia uhalifu mwingine mkubwa. El Obeid haipaswi kuwa eneo jingine la uhalifu."

Imesisitiza umuhimu wa uwajibikaji kupitia ushirikiano na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), huku ikiendelea na uchunguzi wake na kuahidi kuwasilisha matokeo kwa Baraza la Haki za Binadamu na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.