Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za SDGs zimeboresha maisha ya mabilioni ya watu, lakini dunia iko hatarini kukosa kufikia malengo ya mwaka 2030

Watu hupita kwenye onyesho kubwa la magurudumu lenye rangi mbalimbali linaloonyesha Malengo ya Maendeleo Endelevu UMOJA WA MATAIFA (SDGs) katika ukumbi wa kisasa wa majengo.
UN News/Daniel Dickinson Malengo ya Maendeleo Endelevu yanaunda msingi wa haki ya kijamii.

Hatua za SDGs zimeboresha maisha ya mabilioni ya watu, lakini dunia iko hatarini kukosa kufikia malengo ya mwaka 2030

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa ingawa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yameboresha maisha ya mabilioni ya watu duniani, kasi ya maendeleo bado haitoshi kufikia malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2030.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, karibu watu bilioni moja wamepata maji salama ya kunywa, bilioni 1.2 huduma bora za usafi wa mazingira, maambukizi mapya ya VVU yamepungua kwa asilimia 30, huku asilimia 92 ya watu duniani sasa wakipata umeme.

Pamoja na hayo

Hata hivyo, mtu mmoja kati ya kumi bado anaishi katika umaskini uliokithiri, watu bilioni 2.3 wanakabiliwa na uhaba wa chakula, watoto na vijana milioni 273 hawapo shuleni, na maendeleo katika karibu nusu ya malengo 139 yanayofuatiliwa ni ya polepole mno.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo Endelevu, HLPF, jijini New York, Marekani Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed ametoa wito wa mageuzi katika mfumo wa fedha duniani ili kusaidia nchi kupata nafuu ya madeni na ufadhili wa muda mrefu kwa miradi ya maendeleo.

Naye Rais wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Uchumi na Jamii (ECOSOC), Lok Bahadur Thapa, amesema Ajenda ya 2030 bado ni ahadi ya pamoja kwa dunia, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa kubadili ahadi kuwa vitendo.

Malengo matano katika HLPF ya mwaka huu

Wakati muda wa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030 ukizidi kuyoyoma, Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu (HLPF) la mwaka huu 2026 linaangazia hatua za mageuzi, usawa, ubunifu na uratibu ili kuharakisha utekelezaji wa malengo hayo.

Kila mwaka, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hufanya tathmini ya kina ya baadhi ya malengo badala ya yote 17. Lengo la 17, linalohusu ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wa malengo, hujadiliwa kila mwaka.

Mwaka huu, pamoja na Lengo la 17, jukwaa linajadili pia Lengo la 6 (maji safi na usafi wa mazingira), Lengo la 7 (nishati nafuu na safi), Lengo la 9 (viwanda, ubunifu na miundombinu), na Lengo la 11 (miji na jamii endelevu).

Ili kuhakikisha uwajibikaji katika utekelezaji wa SDGs, Umoja wa Mataifa unazitaka nchi kuwasilisha mara kwa mara Tathmini za Hiari za Kitaifa (VNRs) kuhusu maendeleo yao. Tangu mwaka 2016, karibu kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa imewasilisha angalau tathmini moja.

Mwaka huu, nchi 36, kuanzia Albania hadi Uruguay, zinawasilisha tathmini zao katika jukwaa hilo.

Soma zaidi hapa.