Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiswahili kwa asili yake ni lugha ya amani na biashara – Balozi Togolani Mavura

Mwanamume mwenye suti na miwani ameketi kwenye kiti wakati wa mkutano wa waandishi wa habari nchini Tanzania.
UN News/Feissal Kirwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Togolani Idriss Mavura akizungumza na Flora Nducha wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa ya Kiswahili.

Kiswahili kwa asili yake ni lugha ya amani na biashara – Balozi Togolani Mavura

Utamaduni na Elimu
  • Kiswahili asili yake ni lugha ya amani
  • Ni vigumu kugombana na lugha ya Kiswahili
  • Wazungumzao hawagombani

Ikiwa leo ni  maadhimisho ya tano ya Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili chini ya Kaulimbiu "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Dunia", Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Togolani Mavura anafafanua zaidi ni kwa namna gani lugha ya Kiswahili inaweza kuyafanikisha hayo.

Balozi Mavura anasema, “Kiswahili kwa asili yake ni lugha ya amani. Ni vigumu kugombana na lugha ya Kiswahili.”

Anaendelea kufafanua kuwa lugha ya Kiswahili ina maneno machache ya kugombana lakini ina maneno mengi ya maridhiano na anaongeza akisema, “kwa ajili hiyo ni lugha ambayo imetsaidia sana katika eneo letu la Aftika Mashariki kwa sababu (pia) ni lugha ya biashara kwa asili yake. Ni lugha ya watu waliokutana kutoka katika maeneo mbalimbali. Ilikuwa lugha ya kuwaunganisha watu. Kwa hiyo Kiswahili ni lugha daraja na si lugha ya kutenganisha watu.

Bwana Togolani anasema katika jumuiya za kiuchumi ambazo zimefanikiwa sana barani Afrika ni Jumuiya ya Afrika Mashariki, “na moja ya siri yake ni kwa sababu inatumia lugha ya Kiswahili.”

Wazungumzao hawagombani

Balozi Togolani Mavura anaamini katika msemo wa Waswahili usemao ‘Wazungumzao hawagombani’ na kwa hivyo anasema, “kwa hiyo tunaamini kwamba kadiri Kiswahili kitakavyopanuka kwenda kwenye maeneo mengine ndivyo amani itapanuka kwenda kwenye maeneo mengi na ndio maana lugha ya Kiswahili inatumika katika majeshi ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani.”