Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Umoja wa Afrika Kujengwa Uganda

Mwanamume aliyevaa suti akizungumza kwenye maikrofoni wakati wa hafla ya Siku ya Kiswahili, akiwa amezungukwa na watu wengine wawili.
UN News Makamishina wa Kamisheni ya Kiswahili wakiongea na wandishi wa habari jijini Kampala, Uganda.

Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Umoja wa Afrika Kujengwa Uganda

Utamaduni na Elimu

"Yeyote atakayesema kwamba Kiswahili kilifia Uganda, basi aongeze kwamba pia kilifufuliwa tena Uganda,” amesema Profesa Pacifique Malonga kutoka Rwanda, ambaye ni Kamishna katika Kamisheni ya Kiswahili ya Muungano wa Afrika, (AU) kwa kifupi ACALAN-Kiswahili

Prof. Malonga amesema kauli hiyo baada ya hafla ya kutambulisha Kamisheni hiyo mpya ya Kiswahili ya Muungano wa Afrika iliyofanyika jijini Kampala nchini Uganda.

Sasa ifahamike Kiswahili ‘kinafufukia’ Uganda

Kwa mujibu wa Prof. Malonga, mipango ya kujenga makao makuu ya ACALAN Kiswahili nchini Uganda ni ishara kuwa lugha ya Kiswahili itaendelea kukua na kuenea zaidi barani Afrika na duniani.

"Nakumbuka miaka 15 iliyopita tulipopitisha ACALAN Kiswahili, nilikuwa bado kijana mjini Nairobi. Leo ni siku ya furaha kuona Kiswahili kikiendelea kuenea," amesema.

Katibu Mkuu wa ACALAN Kiswahili, Dkt. Ronex Kisembo Tendo, amesema Makao Makuu ya kamisheni hiyo yanatarajiwa kujengwa jijini Kampala ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa kamisheni mpya.

"Natumaini kwamba Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, atawashawishi marais wenzake kuunga mkono ujenzi wa makao makuu ya ACALAN Kiswahili hapa Uganda," amesema Dkt. Kisembo.

Mvulana mdogo wa Kiafrika ameketi kwenye jukwaa akiwa na kipaza sauti wakati wa hafla katika UMOJA WA MATAIFA.
UN /Manuel Elias Mshiriki kijana kwenye maadhimisho ya pili ya siku ya kiswahili duniani mwaka 2023.

Vijana jifunzeni lugha ya Kiswahili 

Kwa upande wake, Prof. Aldin Mutembei wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye ni Mratibu wa ACALAN Kiswahili, amesema huu ni wakati wa vijana kujifunza Kiswahili kwa mkakati ili wanufaike na fursa zinazozidi kuongezeka barani Afrika na duniani.

"SADC, inayoundwa na nchi 16, ilipitisha Kiswahili kuwa lugha rasmi na lugha ya kazi. Hii ina maana kwamba kijana anaweza kwenda kufundisha Kiswahili Botswana, Namibia na nchi nyingine za ukanda huo," amesema Prof. Mutembei.

Alipoulizwa kwa nini makao makuu ya kamisheni hiyo yanajengwa Uganda badala ya nchi nyingine, Prof. Mutembei amesema viongozi wa kamisheni wanaamini Rais Museveni ameonyesha dhamira ya dhati ya kukuza Kiswahili, jambo linalowapa matumaini ya mafanikio makubwa.

"Tunakwenda mahali penye mbolea," amesema.

Ameongeza kuwa kama makao hayo yangejengwa Rwanda au Burundi, swali hilo hilo lingeulizwa. Kwa hiyo walichagua eneo ambalo wanaamini litatoa matokeo makubwa zaidi.

Kwa mujibu wa Prof. Mutembei, ingawa Tanzania ni kitovu muhimu cha Kiswahili, tayari Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo Zanzibar.

"Rais Samia Suluhu Hassan ni mswahili halisi, hivyo tunaona ni muhimu kupata pia kinara mwingine wa kuendeleza Kiswahili katika nchi nyingine kama Uganda," amesisitiza.

Kikundi cha watu, ikiwa ni pamoja na mwanamume aliyevaa mavazi ya Kiswahili ya jadi nyekundu akiwa ameshika fimbo, wakijipiga picha huko Havana, Cuba, wakati wa hafla ya elimu au utamaduni iliyozingatia lugha ya Kiswahili.
UN News Barbara Batte Guevara (kulia) akiwa na wanafunzi wa lugha ya Kiswahili jijini Havana, Cuba. (Maktaba)

Kamisheni itafundisha Kiswahili kwa mbinu mbalimbali

Naye Dkt. Aidah Mutenyo, Kamishna anayehusika na Elimu na Uhamasishaji, amesema kamisheni hiyo itatoa mafunzo kwa watu katika nyanja mbalimbali sambamba na kuhamasisha ufundishaji wa Kiswahili mashuleni.

"Mpango wetu ni kueneza Kiswahili kila mahali. Sisi ni kama wamisionari, na Biblia yetu ni Kiswahili," amesema Dkt. Mutenyo.

Kila mwaka tarehe 7 Julai huadhimishwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili, iliyoanzishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) mwaka 2021 kwa kutambua mchango wa lugha hiyo katika kuimarisha mshikamano, mawasiliano na kuhifadhi pamoja na kubadilishana tamaduni duniani.