Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malezi kwa watoto: Jinsi ya kuzungumza na wavulana kuhusu ‘manosphere’ na ushawishi wa mitandao ya kijamii

Mchoro wa mzazi na kijana wakijadili maudhui mtandaoni kwenye simu mahiri, huku mandhari mbalimbali za kidijitali zikiwa nyuma.
© UN Women/Poompat Watanasiriku Kuzungumza na vijana kuhusu ulimwengu wa ndani na usalama wa mtandao - mwongozo kwa wazazi na walezi.

Malezi kwa watoto: Jinsi ya kuzungumza na wavulana kuhusu ‘manosphere’ na ushawishi wa mitandao ya kijamii

Utamaduni na Elimu

Wavulana wengi katika dunia ya leo wanatumia saa nyingi mtandaoni wakitafuta ushauri kuhusu maisha, kujiamini, mahusiano na mafanikio. Lakini ndani ya safari hiyo ya kidigitali, baadhi hukutana na kile kinachoitwa kwa lugha ya kiingereza manosphere yani mtandao wa maudhui na washawishi wa mitandaoni (influencers) wanaoweza kuathiri namna wanavyoelewa uanaume wao, wanawake na mahusiano.

Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women inaonya kuwa si kila maudhui mtandaoni ni mabaya, lakini baadhi ya maudhui hujificha kama ushauri wa kawaida huku yakikuza chuki dhidi ya wanawake, shinikizo la “kuwa mwanaume kamili”, au mtazamo wa ushindani usio na afya.

Dalili za kuangalia

Mzazi au mlezi anaweza kuona mabadiliko haya kwa mvulana:

• Kujitenga zaidi na familia au marafiki
• Kutumia muda mwingi kupita kiasi mtandaoni
• Kutumia maneno kama mimi ni “alpha”, “beta”, au “red pill”
• Kuonesha hasira au mtazamo hasi dhidi ya wanawake

Mchoro wa vijana wawili wakiangalia simu janja inayoonyesha umbo la mtu aliyevaa miwani ya jua, akiwa amezungukwa na viputo vya usemi vyenye alama mbalimbali zinazowakilisha jamii za mtandaoni.
© UN Women/Poompat Watanasiriku Kuzungumza na vijana kuhusu hali ya maisha na usalama mtandaoni - mwongozo kwa wazazi na walezi.

Wazazi/ Walezi wafanye nini?

1. Anza kwa mazungumzo, si hukumu
Muulize kwa utulivu:

  • Unapenda nini kuhusu maudhui hayo?
  • Kitu gani kinakuvutia hapa?

2. Msaidie kufikiri kwa kina
Mfundishe kujiuliza:

  • Ujumbe gani umepata kutoka katika maudhui hayo?
  • Je maudhui hayo ni kweli au ni propaganda?
  • Mtengeneza maudhui huyu anafaidika vipi?

3. Tengeneza mazingira salama ya kuzungumza
Wavulana wengi hufundishwa kuficha hisia zao. Wasaidie kuona kuwa kuomba msaada si udhaifu.

4. Wape njia mbadala nzuri
Michezo, Nafasi ya kuwa mbunifu , Washauri ( Mentors), Watu ambaye ni mfano wa kuigwa (role models) wazuri, hii inaweza kuwasaidia kujenga kujiamini kwa njia yenye afya.

Mchoro unaoonyesha kijana kwenye simu ya mkononi akiwa amezungukwa na picha za watangazaji mtandaoni na watu wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii, ukionyesha athari za maudhui ya kidijitali.
© UN Women/Poompat Watanasiriku Kuzungumza na vijana kuhusu hali ya maisha ulimwenguni na usalama mtandaoni - mwongozo kwa wazazi na walezi.

Kwa nini hii ni muhimu?

UN Women inasisitiza kuwa maudhui mabaya  mtandaoni hayaishii kwenye rununu pekee. Yanaweza kuathiri namna vijana wanavyoongea, kufikiri na kuwatendea wengine katika maisha halisi.

Ujumbe mkubwa ni huu: mazungumzo ya wazi nyumbani yanaweza kuwa kinga muhimu zaidi dhidi ya ushawishi hasi wa mtandaoni.

Soma zaidi kuhusu makala hiyo hapa: UN Women Explainer on the Manosphere