Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katikati ya vifusi vya Gaza: Jinsi vita inavyohatarisha maisha ya watu wenye ulemavu

Mwanamume anayeitwa Moayad anamsukuma baba yake, Saeed Bakroun, kwenye kiti cha magurudumu kupitia kifusi huko Gaza.
Habari za UN Moayad anamtembeza baba yake, Saeed Bakroun, kwenye kiti chake cha magurudumu.

Katikati ya vifusi vya Gaza: Jinsi vita inavyohatarisha maisha ya watu wenye ulemavu

Msaada wa Kibinadamu

Huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli ambapo video ya Umoja wa Mataifa inaangazia mtaa mmoja uliosheheni vijibanda vya makazi vilivyofunikwa na vitambaa. Ni matokeo ya mashambulizi  kutoka Israeli. Mtoto Muayyad Bakroun anaonekana akimsukuma baba yake Saeed Bakroun kwenye kitimwendo. Wanapita kwenye mashimo, vifusi, na mahema ya watu waliofurushwa makazi yao. Barabara iliyokuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya kila siku sasa imekuwa mtihani mkali kwa mzee huyu mwenye ulemavu wa sio tu kuona bali pia wa viungo.

Taswira inaendelea kuonesha jinsi barabara hiyo ilivyoharibika kwa kiwango kikubwa baada ya vita na mahema yaliyosongamana pande zote mbili za njia, huku Saeed akijaribu kufika kwenye mabaki ya nyumba yake yenye kuta zilizomomonyoka.

Mwanamume kipofu anaegemea begani mwa mwanawe anapomsaidia kupanda ngazi katika jengo lililoharibika.
Habari za UN Said Bakroun, ambaye ana ulemavu wa kutoona au kipofu, anaegemea mabegani mwa mwanawe, Moayad, ili kupanda hadi nyumbani kwao kwenye ghorofa ya pili ya jengo lililobomoka wanakoishi.

Wakiwasili nyumbani hapo, Muayyad anapambana kuvuta kitimwendo ili kupita rundo la vifusi vilivyoziba njia, kisha Saeed anaegemea mabega ya mwanae ili kupanda ngazi zenye nyufa hatari kuelekea ghorofa ya pili. Akiwa ameketi kwenye kiti chake chakavu kilichoshika kutu, Saeed kwa masikitiko anasema.

“Kabla ya vita, niliishi mahali hapa kwa amani ya fikra na usalama. Niliweza kutembea kwenye kitimwendo hiki kwa urahisi na kwa utulivu kwa sababu kuta zilikuwa zikinilinda na kunisafirisha. Lakini baada ya vita, kama unavyoona, kuta zimeporomoka, na ugumu wa kutembea umejidhihirisha, hakika, naushuhudia ugumu huo kiukweli. Sikuwa na njia mbadala ya nyumba hii isipokuwa hema, na hema, kama unavyojua, si salama zaidi kuliko nyumba, na kukodisha nyumba nyingine ni gharama kubwa sana, ambayo iko nje ya uwezo wangu.”

Kamera inamwonesha Saeed akisoma Kitabu Kitukufu cha Qur’ani kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu ambayo ni maalum ya watu wasioona, huku kwa nje kupitia madirisha yaliyovunjika yakionekana mahema na nyumba zilizobomolewa zilizozunguka makazi yake.

Hali ya Saeed inaonesha upande usioonekana kwa urahisi wa janga la kibinadamu huko Gaza, unaohusu maisha ya watu wenye ulemavu wa kuona, viziwi, au ulemavu zaidi ya mmoja wakati huu wa uharibifu mkubwa na kuporomoka kwa huduma za afya. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameeleza kuwa vita vimeongeza hatari kwa kundi hili ambalo haliwezi kusikia amri za kuhama au kuona njia wakati hali ya hatari ikibadilika ghafla. Saeed anakumbuka kazi aliyokuwa nayo kabla ya vita vya sasa vilivyoanza Oktoba 7, 2023.

“Kabla ya vita, nilikuwa mtangazaji katika kituo cha redio cha hapa Gaza. Niliweza kwenda na kurudi kituoni kwa urahisi kwa sababu barabara ilikuwa inapitika. Lakini sasa, baada ya vita, barabara hazina lami, na nyumba, kama unavyoona, iko katika hatari ya kuporomoka.”

Mikono ya karibu ya Said Bakroun ikisoma kitabu cha Braille.
Habari za UN Said Bakroun anasoma moja ya vitabu viwili vilivyosalia baada ya maktaba yake kuungua kutokana na vita, akitumia Braille.

Mzee Saeed anaonekana akifungua kurasa za kitabu chenye maandishi ya nukta nundu. Kusoma, kwake sio mchezo wa kupitisha muda tu, bali ni nafasi ya kiroho ya kumsaidia kuhimili maisha, ingawa moto uliounguza nyumba yake umemwachia vitabu viwili pekee.

“Kitabu hiki mkononi mwangu, pamoja na kitabu kingine kilichochapishwa kwa njia ya kawaida inayotumiwa na watu wanaoona, ndivyo vitabu viwili pekee vilivyookoka kwenye moto ulioteketeza nyumba yangu wakati wa mashambulizi. Ndiyo maana sasa ninahisi upweke na uchovu mkubwa, baada ya kupoteza kitu kilichonipa furaha yangu muhimu na kitu nilichotumia muda wangu mwingi kukifanya; kusoma.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, linakadiria kuwa hadi watu 43,000 kati ya 172,000 waliojeruhiwa Gaza tangu Oktoba 2023 wamepata majeraha yaliyobadili kabisa mfumo wa maisha yao, huku robo yao wakiwa ni watoto.

Licha ya mahitaji hayo makubwa, huduma za utengamao zimebaki kuwa duni sana, huku kukiwa hakuna kituo hata kimoja kinachofanya kazi kikamilifu, na zaidi ya wagonjwa 400 wapo kwenye orodha ya kusubiri vitanda vya matibabu hayo maalum.

Wakati huohuo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA, inaeleza kuwa mashambulizi ya mabomu na risasi yanaendelea kuumiza raia katika Ukanda mzima wa Gaza, huku maeneo ya wakimbizi yakiwa katika hali mbaya sana kukiwa na ukosefu wa mwanga, nishati, na maji safi.

Said Bakroun, mwanaume kipofu huko Gaza, anasoma kutoka kwa kitabu cha Braille akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu.
Habari za UN Said Bakroun anatumia muda wake kusoma vitabu viwili alivyoacha—kwa Braille—baada ya maktaba yake kuungua kutokana na vita.

Kwa Saeed, changamoto kubwa zaidi ni usalama na jinsi ya kujiokoa dharura inapotokea.

“Wasiwasi pekee ni kupata mahali salama, kwa sababu mahali hapa pameporomoka. Kwa mfano, mashambulizi yanapotokea, mtu asiye na ulemavu anaweza kuondoka kwa urahisi na kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine. Lakini hali yangu ya afya hainiruhusu kufanya hivyo.”

Ikiwa ni siku chache baada ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wasioona na viziwi inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 27 Juni, hali ya Gaza inabaki kuwa mfano halisi wa changamoto wanazopitia walemavu. 

Video za mwisho zinaonesha taswira ya jumla ya mtaa anaoshi Saeed ukiwa umejaa vifusi na mahema, huku mzee huyu akionekana kwa mbali ndani ya mabaki ya nyumba yake akiendelea kushika kitabu chake cha maandishi ya nukta nundu, kilichonusurika kwenye moto, akitafuta hifadhi salama na huduma za msingi zitakazomwezesha japo kuishi.