Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres aonya kuhusu kuongezeka kwa kauli za chuki katika zama za kidijitali

Mkono wa mwanamke ulioandikwa 'STOP CHUKI' kwenye kiganja cha mkono umeinuliwa mbele, huku picha ya mwanamke huyo ikiwa imefifia nyuma kwenye daraja.
© Adobe Stock/Flashizzle/Watu Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kauli za Chuki huadhimishwa kila mwaka tarehe 18 Juni.

Guterres aonya kuhusu kuongezeka kwa kauli za chuki katika zama za kidijitali

Haki za binadamu

Kauli za chuki zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa mshikamano wa jamii na amani duniani, na mara nyingi ndiyo hatua ya kwanza kuelekea vitendo vya ukatili, migogoro na hata uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres. 

Katika ujumbe wake kwa ajili ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kauli za Chuki, ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 18, Guterres amesema chuki hutumiwa kama nyenzo ya mgawanyiko inayolenga makundi mbalimbali, yakiwemo wanawake, wahamiaji, wakimbizi, watu wa jamii ya LGBTQIA+, watu wenye ulemavu na makundi mengine ya wachache, na mara nyingi kwa manufaa ya kisiasa.

“Kauli za chuki ndiyo hatua ya kwanza katika njia ya kuwanyima watu utu wao, njia ambayo mara nyingi hupelekea vurugu, migogoro na uhalifu wa kutisha,” amesema Guterres. 

Amesisitiza kuwa tatizo hilo limekuwa kubwa zaidi katika zama za kidijitali ambapo ujumbe wa chuki unaweza kusambaa kwa kasi isiyokuwa ya kawaida kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya mtandaoni.

Msichana mdogo amelala kitandani akiangalia simu yake ya mkononi katika chumba chenye mwanga hafifu.
© UNICEF/Karel Prinsloo Unyanyasaji mtandaoni unaweza kusababisha wasiwasi, msongo wa mawazo na hata kujiua kwa watoto.

Algoriti za mitandao ya kijamii zakosolewa

Katibu Mkuu huyo amesema maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili Mnemba (AI), yameongeza kasi ya kusambaa kwa taarifa za chuki na upotoshaji. Ameonya kuwa baadhi ya algoriti za majukwaa ya kidijitali zinachochea mgawanyiko kwa kuhamasisha maudhui yanayoibua hasira na migogoro kwa lengo la kuongeza ushiriki wa watumiaji.

Ameongeza kuwa “Algoriti nyingi sana zinasababisha hasira na mgawanyiko, zikihamasisha uongo ili kupendwa au ‘likes’ na kukuza vurugu ili kupata watazamaji zaidi,” amesema. Aidha, ameeleza kuwa kutokujulikana kwa watumiaji mtandaoni kunafanya iwe vigumu kuwawajibisha wanaosambaza kauli za chuki na ujumbe wa uchochezi.

Wito wa hatua madhubuti dhidi ya chuki

Pamoja na changamoto hizo, Guterres amesema kuna suluhu za vitendo zinazoweza kuvunja mzunguko huo hatari. 

Ametaja elimu inayowawezesha watu kutambua na kukataa kauli za chuki, msaada kwa waathirika wa unyanyasaji au wa ukatili wa mtandaoni na hatua madhubuti zaidi kutoka kwa serikali na kampuni za teknolojia.

Amesisitiza kuwa nchi zina wajibu wa kisheria chini ya sheria za kimataifa kupambana na uchochezi wa chuki na kukuza ushirikishwaji, kuheshimu tofauti za watu na kuimarisha mshikamano. 

Hata hivyo, ameonya kuwa uhuru wa kujieleza haupaswi kutumiwa kama kisingizio cha kusambaza ujumbe unaodhuru wengine.

Wasichana wanne wadogo wa Kihindi kutoka kituo cha watoto yatima huko Rajasthan, India, wamekusanyika pamoja wakitazama simu janja na kucheka.
© UNICEF/Srikanth Kolari Wanafunzi wa Kituo cha Yatima cha JR wakitazama vichekesho vya Bollywood kwenye simu janja.

UN yataka mazingira salama ya kidijitali

Katibu Mkuu amesema Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Kauli za Chuki pamoja na Kanuni za Kimataifa za Uadilifu wa Taarifa zinatoa mwongozo muhimu wa kujenga mazingira ya kidijitali yaliyo salama na yenye maadili.

Katika maadhimisho haya ya tano ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kali za Chuki, Guterres ametoa wito kwa watu, serikali na taasisi kote duniani kukataa ubaguzi wa aina zote na kushirikiana kujenga dunia inayozingatia haki za binadamu, utu na heshima kwa wote. 

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kuwa “Tukatae chuki katika aina zake zote na tushirikiane kujenga dunia inayojengwa juu ya haki za binadamu, utu na heshima,”