Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Mashambulizi hospitali Lebanon yaathiri wagonjwa walio tayari hatarini

Barabara moja huko Tebnine, kusini mwa Lebanon, imejaa mabomoko na takataka kutoka majengo yaliyoharibiwa na mapigano. Nyuma, Hospitali ya Serikali ya Tebnine inasimama na alama ya Msalaba Mwekundu; muundo wake na eneo linalozunguka linaonyesha dalili za uharibifu kutokana na mgogoro.
© UNICEF Barabara imejaa vifusi vya majengo yaliyoharibiwa vibaya na mapigano ya hivi karibuni karibu na hospitali huko Tebnine, kusini mwa Lebanon.

WHO: Mashambulizi hospitali Lebanon yaathiri wagonjwa walio tayari hatarini

Amani na Usalama

Mashambulizi dhidi ya hospitali katika mji wa Tyre kusini mwa Lebanon yamejeruhi makumi ya watu na kuongeza shinikizo kwa mfumo wa afya ambao tayari umeathiriwa na vita, limeonya leo Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO).

WHO, nchini Lebanon inafanyia uthibitisho taarifa za mashambulizi yaliyolenga hospitali katika mji wa Tyre jana Jumatatu, huku kukiwa na ongezeko la kutia wasiwasi la mashambulizi dhidi ya vituo vya afya nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka mamlaka za Lebanon, watu wasiopungua 86, wakiwemo wahudumu wa afya, wamejeruhiwa katika mashambulizi dhidi ya Hospitali ya Jabal Amel.

Mwakilishi wa WHO nchini Lebanon, Abdinasir Abubakar, amesema mashambulizi hayo yalisababisha uharibifu mkubwa katika idara ya dharura na chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Akizungumza kutoka mji mkuu wa Beirut leo Jumanne, Dkt. Abubakar amesema Hospitali ya Jabal Amel ni miongoni mwa hospitali chache ambazo bado zinaendelea kutoa huduma kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi ya afya yaongezeka

Katika kipindi cha miezi mitatu pekee, WHO imethibitisha karibu mashambulizi 190 dhidi ya sekta ya afya, yaliyosababisha vifo vya wahudumu wa afya 128 na kujeruhi wengine 332. Wiki moja iliyopita pekee ilishuhudia mashambulizi 11 dhidi ya huduma za afya.

Dkt. Abubakar ameongeza kuwa “Mashambulizi haya hayasababishi tu vifo na majeraha, bali pia yanawanyima watu huduma muhimu za afya wanazozihitaji.”

Eneo la Tyre limeathirika zaidi katika siku za karibuni kutokana na mapigano kati ya wapiganaji wa Hezbollah na Israel. 

Hospitali mbili kati ya tatu zilizopo katika eneo hilo, Jabal Amel na Hiram, zimeharibiwa, huku hospitali ya tatu ikilemewa na ongezeko kubwa la wagonjwa waliojeruhiwa.

Huduma muhimu za afya zatikiswa

WHO imesema upatikanaji wa huduma muhimu za afya umeathirika vibaya, hasa kusini mwa Lebanon, ambapo wagonjwa wanalazimika kusubiri hadi saa 48 kufikishwa katika hospitali za rufaa.

“Hospitali sita bado hazijaanza tena huduma za uzazi na kwa sasa zinatoa huduma za dharura pekee,” amesema Dkt. Abubakar. “Kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga, kuchelewa kupata huduma kunaweza kuwa tofauti kati ya maisha na kifo.”

Kawthar, mwenye umri wa miaka 14, mgonjwa katika hospitali moja huko Beirut, Lebanon, amekaa kwenye kiti cha magurudumu akionyesha vidonda vya shrapnel na majeraha ya uso yaliyopatikana wakati wa kuongezeka kwa vurugu huko Baalbeck mnamo Machi 5, 2026. Anapona majeraha yake chini ya mpango wa ACWA wa UNICEF.
© UNICEF/Fouad Choufany James Elder alikutana na Kawthar, mwenye umri wa miaka 14, ambaye alipata majeraha mengi, ikiwa ni pamoja na vidonda vya shrapeni kwenye uso, majeraha ya miguu, na jeraha la mapafu.

Wasiwasi wa magonjwa katika makazi ya wakimbizi

WHO pia imeelezea hali ngumu ya kiafya katika makazi ya muda yanayohifadhi takribani watu 130,000 waliokimbia mapigano. 

Idadi ya waliokimbia makazi yao inaendelea kuongezeka kufuatia maagizo mapya ya watu kuhama yaliyotolewa na Israel.

Kuongezeka kwa ghasia pamoja na onyo la mashambulizi ya Israel katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, vinavyoishi mamia ya maelfu ya raia, kumesababisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili hali hiyo siku ya Jumatatu.

WHO imekuwa ikifuatilia magonjwa ya kuambukiza katika makazi ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, na imebaini ongezeko la visa vya kuhara vinavyosababishwa na maji machafu.

“Tupo katika msimu wa joto na sasa hatari ya mlipuko wa kipindupindu inaweza kuongezeka,” ameonya Dkt. Abubakar.

Wanawake wakiweka vifaa vya usafi katika masanduku ya karatasi kwa ajili ya wanawake na wasichana waliohamishwa nchini Lebanon, mpango wa UN Women na Assabil NGO.
UN Wanawake Kupitia UN Women na Assabil NGO, kamati za wanawake katika maktaba za umma za Beirut na Barja zinasambaza vifaa muhimu vya usafi kwa watu zaidi ya 250 walioathiriwa na migogoro na wasichana, wakiendeleza heshima na uongozi wa mitaa.

Wito wa kulinda huduma za afya

WHO imesisitiza kuwa mahitaji ya kibinadamu yanaongezeka kwa kasi kuliko uwezo wa kuyashughulikia, na hivyo kuhitajika ufadhili endelevu kwa huduma muhimu za afya.

“Tunahitaji pia mashambulizi dhidi ya huduma za afya yakome na vituo vya afya vilindwe kikamilifu,” amesema Dkt. Abubakar, akirudia wito wa kusitishwa kwa mapigano na kupatikana kwa amani ya kudumu.

Tangu kuanza kwa awamu ya sasa ya mapigano kati ya Israel na wapiganaji wa Hezbollah tarehe 2 Machi, zaidi ya watu 3,400 wameuawa nchini Lebanon na karibu watu 10,400 wamejeruhiwa, wengi wao wakiwa raia.

Dkt. Abubakar amesema “Hii imekuwa baadhi ya miezi yenye vifo vingi zaidi nchini Lebanon tangu kuanza kwa mzozo mwezi Oktoba 2023,”.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyopatanishwa na Marekani kati ya Lebanon na Israel yalianza kutekelezwa tarehe 17 Aprili, lakini hayajawahi kuheshimiwa kikamilifu na pande zote mbili. 

Makubaliano hayo yameongezwa mara mbili, mara ya mwisho ikiwa tarehe 16 Mei kwa kipindi cha siku 45.

Wanawake na wasichana hawawezi kusubiri: UNFPA

Wanawake na wasichana nchini Lebanon wanaendelea kulipa gharama kubwa kutokana na ongezeko la mashambulizi na ufurushwaji wa watu licha ya kuwepo kwa usitishaji mapigano, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA). 

Mvutano ulioongezeka mjini Beirut na mashambulizi makali kusini mwa Lebanon umeacha familia nyingi zikiishi kwa hofu na kutokuwa na uhakika. Akizungumza kutoka Beirut kwa njia ya video, Mwakilishi wa UNFPA nchini humo, Anandita Philipose, amesema mashambulizi ya anga mwishoni mwa wiki yaliharibu kituo cha afya ya msingi kinachoungwa mkono na UNFPA pamoja na kituo salama cha wanawake na wasichana kusini mwa nchi, ambavyo ni miongoni mwa vituo vichache vilivyokuwa bado vinatoa huduma muhimu. 

Hospitali ya umma inayotoa huduma za uzazi pia iliharibiwa. Kati ya waliolazimika kuhama makazi yao ni takribani wanawake wajawazito 13,500, huku 1,500 wakitarajiwa kujifungua ndani ya siku 30 zijazo. Aidha, wanawake wapatao 1,500 bado wamekwama kusini mwa Lebanon bila huduma za uhakika za uzazi au maeneo salama ya kujifungulia.

UNFPA: ukosefu wa fedha unaweza kuzidisha mgogoro

UNFPA pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya katika makazi ya muda ya waliokimbia makazi yao, ambapo tathmini zimebaini msongamano mkubwa wa watu, mwanga hafifu, ukosefu wa faragha na miundombinu duni ya usafi. 

Hali hiyo inaongeza hatari ya ukatili wa kijinsia, hasa kwa wasichana balehe, wanawake wanaoongoza familia, wajawazito na watu wenye ulemavu. Shirika hilo linaendelea kutoa huduma za afya ya uzazi kupitia timu za mkononi, msaada wa kisaikolojia na huduma za ulinzi kwa kushirikiana na mamlaka za Lebanon na washirika wa ndani. 

Hata hivyo, Bi. Philipose ameonya kuwa bila ufadhili wa haraka na endelevu, madhara ya kibinadamu yataongezeka kwa kasi. Ombi la awali la dharura ya UNFPA imefadhiliwa kwa asilimia 30 pekee, na sasa shirika hilo linahitaji dola milioni 25 ili kuendelea na shughuli zake hadi Agosti. 

Ameonya kuwa kupunguzwa kwa shughuli hizo kunaweza kuwanyima zaidi ya wanawake 75,000 huduma muhimu za ulinzi dhidi ya ukatili wa kijinsia, usimamizi wa kesi na maeneo salama wakati ambapo wanazihitaji zaidi.