Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukimya sio ridhaa ya ndoa za utotoni Afghanistan; kamati ya Umoja wa Mataifa yalaani

Mwanamke mwenye shati la bluu ameketi juu ya kofia ndani ya nyumba, akitazama nje ya dirisha katika chumba rahisi.
© UNICEF/Madhok Ndoa za utotoni ni mkakati wa maisha kiuchumi nchini Afghanistan huku familia zikiwaoza binti zao ili kupunguza mzigo wao wa kiuchumi.

Ukimya sio ridhaa ya ndoa za utotoni Afghanistan; kamati ya Umoja wa Mataifa yalaani

Haki za binadamu

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto, CRC, imelaani vikali utawala uliopo sasa nchini Afghanistan kufuatia uamuzi wao wa kupitisha sheria mpya inayoruhusu ndoa za utotoni na kuchukulia ukimya wa msichana kama ridhaa ya kuolewa. Amri hiyo namba 18 ya mwaka 2026, inatenganisha wasichana waliofikia umri wa kubalehe na kutumia mgawanyiko huo kuruhusu waolewe, jambo ambalo wataalamu hao wameagiza lifutwe mara moja.

Katika taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, nchini Uswisi, kamati hiyo imetaja kuwa huo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na kwenda kinyume kabisa na Mkataba wa Haki za Mtoto, ambapo wameeleza kuwa kubalehe hakuwezi kuchukuliwa kama kigezo cha binti kuwa mtu mzima au kuwa na uwezo wa kisheria wa kuolewa, kwani watoto kimsingi hawana uwezo wa kutoa ridhaa kamili na ya hiari.

Kamati hiyo pia, imekumbusha kuhusu msimamo wake wa pamoja na Kamati ya Kutokomeza Ubaguzi dhidi ya Wanawake unaoeleza kwamba, "Ndoa ya utotoni, ambapo angalau upande mmoja unakuwa na umri chini ya miaka 18, inajumuisha kitendo chenye madhara na ni aina ya ndoa ya kulazimishwa, ikizingatiwa kwamba watoto kwa asili yao hawana uwezo wa kutoa ridhaa kamili, ya hiari na yenye uelewa kuhusu ndoa." 

Madhara ya kuhalalisha ndoa za utotoni

Kamati hiyo, inayoundwa na wataalamu huru 18 wa haki za watoto, imeonya kuwa mfumo wowote wa kisheria unaohalalisha au kurahisisha ndoa za watoto unawanyima wasichana fursa zao za baadaye. 

"Ndoa ya utotoni haijumuishi tu kitendo chenye madhara bali ni ukiukaji mkubwa wa haki za msingi. Inawaweka wasichana katika hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili, unyonyaji, ujauzito wa mapema na wa kulazimishwa, kukatishwa masomo, na madhara ya muda mrefu ya kimwili na kisaikolojia," imeeleza kamati hiyo huku ikiongeza kuwa hatua hii inashusha utu wao na kuwanyang'anya uhuru wa kujiamulia mustakabali wao.

Wataalamu hao wameonesha wasiwasi mkubwa kwamba amri hii ni muendelezo wa mfululizo wa hatua za kibaguzi zinazochukuliwa na utawala huo, ikiwa ni pamoja na ule uamuzi wa kupiga marufuku wasichana kupata elimu ya sekondari na ya juu hali ambayo imezidisha umaskini na ukosefu wa usawa nchini humo, "Hatua hizi zimewanyima mamilioni ya wasichana wa Afghanistan haki zao za msingi, zimefanya ushiriki wao wa kijamii na kiuchumi wa baadaye kuwa dhaifu, na zimeongeza umaskini na ukosefu wa usawa kote nchini."

Wito wa kusitisha sheria zote kandamizi

Kamati imetoa wito kwa mamlaka zilizopo Afghanistan kusitisha mara moja taratibu zote zinazokiuka haki za watoto na kupiga marufuku kabisa ndoa za utotoni mara moja. Aidha, wameitaka serikali hiyo kurejesha haki zote za wasichana za kupata elimu, ulinzi, usawa, na kushiriki kikamilifu katika jamii, kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa ambayo nchi hiyo imesaini.