Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Niko hapa kuonesha mshikamano na watu wa DRC katika vita dhidi ya Ebola: Tedros

Mfanyakazi wa afya mwenye kanzu ya bluu na kinyago anatumia thermometer kumchunguza mtu kwenye mlango wa kituo cha matibabu cha muda katika Mkoa wa Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WHO/Joël Lumbala Mhudumu wa afya anampima joto mwanamume kwenye mlango wa kituo cha afya katika Mkoa wa Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Niko hapa kuonesha mshikamano na watu wa DRC katika vita dhidi ya Ebola: Tedros

Afya

Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amewasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC leo Ijumaa Ijumaa, taifa linalokabiliana na mlipuko mpya wa Ebola na kuwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Kinshasa kuwa yuko huko kuonesha jamii kwamba “hawako peke yao.”

Dkt. Tedros ameyasihi makundi mbalimbali yenye silaha yanayoendesha shughuli zao bila kuwajibika katika eneo la Mashariki lililoharibiwa na vita kutangaza usitishaji wa mapigano ili wahudumu wa afya waweze kuwafikia watu wanaohitaji msaada na kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

DRC iliijulisha WHO kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa sasa wa ugonjwa wa Ebola virusi vya Bundibugyo tarehe 15 Mei na kufikia Alhamisi, wiki hii wagonjwa 125 wamethibitishwa, ikiwa ni pamoja na vifo 17 katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.

Aidha, wagonjwa 906 washukiwa kuwa na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na zaidi ya vifo 223 vinaendelea kuchunguzwa na kuhakikiwa huku uwezo wa upimaji ukiboreshwa.

Nchini Uganda, kufikia Alhamisi wiki hii kulikuwa na wagonjwa saba waliothibitishwa, ikiwa ni pamoja na kifo kimoja. WHO ilisema kuwa kwa sasa hakuna ushahidi wa maambukizi ya ugonjwa huo katika jamii nchini humo.

Wafanyakazi wenye mavazi ya usalama wanapakia kontena kubwa kutoka kwenye lori hadi kwenye ndege kwenye uwanja wa ndege. Kontena hiyo ina logo ya Okapi Logistique.
© WHO / Joël Lumbala Usafirishaji wa vifaa muhimu vya matibabu kwa ajili ya kukabiliana na Ebola umefikishwa kwenye uwanja wa ndege wa Bunia katika jimbo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ni ugonjwa unaoupata ukimuhudumia mtu

Wiki mbili tangu kuzuka kwa mlipuko huu wa hivi karibuni wa Ebola unaoua, WHO linakadiria kuwa sasa kuna wagonjwa  906 wanaoshukiwa kuwa na Ebola DRC, ikiwa ni pamoja na vifo 223 vinavyoshukiwa.

Ugunduzi wa mapema na uhamasishaji wa jamii vinaendelea kuwa muhimu katika kuokoa maisha, huku matibabu na chanjo zinazowezekana zikiendelea kutathminiwa, shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa lilisema.

Tangu tarehe 15 Mei, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakisaidia DRC pamoja na nchi jirani ya Uganda kudhibiti mlipuko huo uliosababishwa na aina adimu ya virusi vya Ebola ya Bundibugyo, ambayo huenea kupitia mawasiliano ya karibu.

“Ni ugonjwa unaoupata unapomhudumia mtu, mume wako au mwenzi wako au mtoto wako au mama yako,” amesema Anaïs Legand, Afisa wa Kiufundi wa WHO alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo.

 “Unaambukizwa unapojaribu kumsaidia mtu mwenye dalili, na hili ni jambo la kusikitisha,” amesema, akieleza kuwa familia na marafiki lazima waelekezwe kutowagusa wapendwa wao wanaoanza kuugua.

Asilimia 30 hadi 50 ya uwezekano wa kufa

Bi. Legand amesisitiza umuhimu mkubwa wa kinga na kupata huduma mapema mbele ya ugonjwa huu hatari sana. Kwa kuzingatia milipuko iliyopita, kiwango cha vifo “kinakadiriwa kuwa kati ya asilimia 30 na 50,” amesema “ni kikubwa sana.”

Ingawa “watu watano kati ya 10 wana uwezekano wa kufa,” bado kuna mengi yanaweza kufanywa kusaidia wagonjwa kupona, kulingana na mtaalamu huyo wa WHO.

“Tunaweza kuongeza huduma bora za wagonjwa mahututi,” amesema. “Tunaweza kusaidia jamii kutambua dalili mapema ili kupata uchunguzi wa mapema, ili waweze kupokea kiwango cha huduma wanachohitaji.”

Uzoefu unaonesha kuwa milipuko ya Ebola inaweza kudhibitiwa tu pale jamii zinaposhirikishwa kikamilifu katika juhudi za kukabiliana nayo, Bi. Legand amesisitiza akitaja kisa cha hivi karibuni nchini DRC ambapo mgonjwa alipona kabisa na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Timu za afya za umma zilizovaa mavazi ya kinga zinashughulikia mlipuko wa Ebola kwenye mlango wa Hospitali ya Rwampara ya Urefu wa Kijamii katika Mkoa wa Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© WHO / Joël Lumbala Mhudumu wa afya anachunguza mwanamume kwenye mlango wa kituo cha afya katika Mkoa wa Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kazi ya uchunguzi inaendelea

WHO imekusanya wataalamu kupitia upya matibabu na chanjo zinazoweza kufanya kazi dhidi ya virusi hivyo, huku bidhaa kadhaa sasa zikibainishwa kwa tathmini zaidi.

Kwa wagonwa waliothibitishwa, dawa tatu zinazotarajiwa kutumika kwa matibabu zimepewa kipaumbele kwa majaribio ya kitabibu, Bi. Legand amefichua ambazo ni kingamwili za monokloni MBP 134 na maftivimab, pamoja na dawa ya kuzuia virusi remdesivir.

Kwa upande wa kinga, dawa ya kuzuia virusi ya kunywa iitwayo obeldesivir imepewa kipaumbele katika utafiti wa kitabibu kama hatua ya baada ya mtu kuathiriwa kwa wale waliowasiliana nawagonjwa waliothibitishwa.

Mtaalamu huyo wa WHO ameongeza kuwa chanjo mbili zinazotarajiwa zimetambuliwa kwa ajili ya tathmini mara dozi zitakapopatikana.

Shirika hilo linafanya kazi kwa karibu na serikali za DRC na Uganda huku wakati huo huo “likiongeza haraka uwezo wa huduma za matibabu.”

Changamoto zinazojitokeza

“Mlipuko huu unatokea katika mazingira magumu sana,” amesisitiza, akikumbusha kuwa katika jimbo lililoathirika la Ituri pekee, watu milioni 1.2 wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku migogoro inayoendelea na ukosefu wa chakula vikikwamisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo.

“Changamoto tuliyonayo uwanjani siyo ukosefu wa rasilimali,” Bi. Legand amesisitiza. “Ni suala la ufikiaji.”

Uwanja wa ndege wa Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, umefungwa, na ingawa serikali ya DRC imeruhusu safari za ndege za kibinadamu kuendelea, changamoto za kiutendaji bado zipo. “Siku moja nilipigiwa simu na timu yangu wakiniambia hakuna mafuta,” amesema mtaalamu huyo wa WHO.

Hakuna vizuizi vya safari kwa sasa

Ingawa WHO imeonesha kuwa watu kutoka maeneo yaliyoathirika ambao huenda wameathiriwa na Ebola hawapaswi kusafiri, shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa halipendekezi kwa sasa kuwekwa kwa vizuizi vyovyote vya usafiri au biashara dhidi ya DRC au Uganda kulingana na taarifa zilizopo sasa.