Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaimarisha huduma za hospitali kwa watoto wenye utapiamlo mkali barani Afrika

Wataalamu wa afya wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) wenye kanzu nyeupe wanachunguza mtoto kwenye ubao wa kichwa cha kuzuia magonjwa wakati wa mafunzo katika hospitali.
© WHO Uganda - Kuboresha huduma za hospitali kwa matibabu ya utapiamlo mkali wa watoto.

WHO yaimarisha huduma za hospitali kwa watoto wenye utapiamlo mkali barani Afrika

Afya

Katika juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya utapiamlo mkali wa kupindukia kwa watoto barani Afrika, Ofisi ya Kanda ya Afrika ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, kwa kushirikiana na wizara za afya, hospitali washirika na kwa msaada wa Irish Aid, imeendesha mfululizo wa mafunzo maalum ya wakufunzi ili kuboresha huduma za hospitali kwa watoto wanaokabiliwa na utapiamlo mkali wa kupindukia wenye matatizo ya kiafya yanayoambatana nao.

Katika maeneo mengi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, utapiamlo bado unaendelea kuwa moja ya sababu kuu za vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano. Watoto wengi wanaolazwa hospitalini kutokana na hali hiyo hukabiliwa na changamoto kubwa za kiafya zinazohitaji huduma maalum, uangalizi wa karibu na wahudumu wenye ujuzi wa hali ya juu.

Kikundi cha wataalamu wa afya na wafanyakazi wa serikali wanapiga picha baada ya kikao cha mafunzo juu ya usimamizi wa utapiamlo mkali, kilichoandaliwa na Shirika la Afya Duniani na Irish Aid.
© WHO Uganda -Warsha wa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara iliyofanyika Kapmala nchini Uganda kwa ajili ya kuboresha huduma za hospitali kwa matibabu ya utapiamlo mkali wa watoto.

Kwa mujibu wa Makadirio ya Pamoja ya Utapiamlo kwa Watoto ya mwaka 2025 kutoka WHO, UNICEF na Benki ya Dunia, zaidi ya watoto milioni 12 duniani wanakabiliwa na utapiamlo mkali wa kupindukia, huku karibu watoto milioni 3 kati yao wakiwa barani Afrika. Hali hiyo imeongeza hitaji la haraka la kuimarisha uwezo wa wahudumu wa afya ili kuhakikisha watoto wanapata huduma bora, salama na zinazotegemea ushahidi wa kisayansi.

“Mafunzo haya yanaonesha umuhimu mkubwa wa kuhakikisha huduma bora za hospitali kwa watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo na yanashughulikia hitaji muhimu la kusaidia nchi kutumia taratibu sanifu na kuendelea kuboresha ubora wa huduma ili kuokoa maisha,” amesema Dkt. Eugénie Niane, Afisa wa Kiufundi wa Lishe na Usalama wa Chakula wa WHO Madagascar.

Mtaalamu wa afya aliyevaa koti jeusi anapendelea meza ya matunda na mboga kwa kikundi cha wanawake wa Afrika na watoto wao.
© WHO Uganda - Kuboresha huduma za hospitali kwa matibabu ya utapiamlo mkali wa watoto.

Mafunzo hayo yalikuwa sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo mapya ya WHO ya mwaka 2023 kuhusu kinga na usimamizi wa utapiamlo mkali wa kupindukia pamoja na uvimbe wa lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano. Yalitegemea moduli zilizoboreshwa za WHO za mwaka 2025 ambazo zimeandaliwa kwa kuzingatia ushahidi wa hivi karibuni wa kisayansi na uzoefu kutoka vituo vya afya barani Afrika.

Washiriki walipatiwa mafunzo ya kinadharia na vitendo yaliyohusisha tafiti za visa halisi, majaribio ya kuigiza mazingira ya hospitali, mazoezi ya uwezeshaji pamoja na mafunzo ya kliniki chini ya usimamizi wa wataalamu hospitalini. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uwezo wa kutathmini na kugundua matatizo yanayohusiana na utapiamlo mkali wa kupindukia, kuboresha lishe ya tiba na ufuatiliaji wa wagonjwa, pamoja na kuimarisha ushiriki wa walezi katika matibabu ya watoto wao.

“Mafunzo haya yametukumbusha jambo muhimu, Afrika ina utaalamu, ari na dhamira ya kubadilisha simulizi la uhai wa watoto barani humo,” amesema Dkt. Joy Odhiambo, Mtaalamu wa Afya ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya ya Kenya. Aliongeza kuwa kila mhudumu wa afya aliyeshiriki katika mpango huo sasa ni sehemu ya harakati kubwa za kulinda afya na mustakabali wa watoto wa Afrika.

Mtaalamu wa afya mwenye kanzu nyeupe anapima uzito wa mtoto mchanga kwenye kigawanyo cha hospitali, akiwa amezungukwa na wafanyakazi wengine wa afya na wagonjwa.
© WHO Uganda - Kuboresha huduma za hospitali kwa matibabu ya utapiamlo mkali wa watoto.

Mbali na kuwajengea uwezo wa kitabibu, washiriki waliandaliwa pia kuwa wakufunzi wa kitaifa watakaoweza kuendesha mafunzo hayo katika nchi zao. Hatua hiyo inalenga kusaidia nchi kuimarisha mifumo yao ya afya kwa njia endelevu na kuhakikisha huduma za lishe zinaendelea kuboreshwa hata baada ya mafunzo ya kikanda kukamilika.

Kwa mujibu wa Dkt. John Makengo Mafuila Adjukula, Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini katika Mpango wa Kitaifa wa Lishe wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ushirikiano wa kikanda umeanza kuzaa matunda muhimu.

“Sasa tumejiandaa vizuri kuendesha mafunzo kama haya katika nchi zetu na kuwa mabingwa katika vituo vya afya ili kuimarisha usimamizi wa watoto wanaosumbuliwa na utapiamlo mkali wa kupindukia wenye matatizo ya kiafya,” amesema.

Wataalamu wa afya wakimchunguza mtoto mchanga hospitalini.
© WHO Togo - Kuboresha huduma za hospitali kwa ajili ya magonjwa ya utapiamlo mkali wa watoto.

Mafunzo hayo yalifanyika kwa awamu mbili, kuanzia maandalizi ya mtandaoni yaliyofanyika kati ya tarehe 27 Aprili na 1 Mei 2026 yakihusisha nchi 12. Baadaye, vipindi vya ana kwa ana vilifanyika Kampala, Uganda kwa nchi zinazotumia Kiingereza ikiwemo Ethiopia, Kenya, Malawi, Nigeria, Sudan Kusini na Uganda, pamoja na Lomé mji mkuu wa Togo kwa nchi zinazotumia Kifaransa ikiwemo Burkina Faso, Madagascar, Niger, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Chad na Togo.

Nchi hizo, ambazo zimeathiriwa kwa kiwango kikubwa na utapiamlo wa watoto, zinaendelea kupata msaada wa WHO katika kurekebisha na kutekeleza taratibu za kitaifa zinazolingana na viwango vya kimataifa vya huduma za lishe.

Washiriki wengi walieleza kuwa kubadilishana uzoefu kati ya nchi mbalimbali kulikuwa moja ya mafanikio makubwa ya mafunzo hayo, kwani kulisaidia kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kujifunza mbinu mpya za kuboresha huduma kwa watoto hospitalini.

Kikundi cha wataalamu wa afya wenye vyeti katika kikao cha mafunzo huko Brazzaville, Kampala, na Lomé kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkoa wa WHO kwa Afrika.
© WHO Togo - Kuboresha huduma za hospitali kwa ajili ya magonjwa ya utapiamlo mkali wa watoto.

Mwisho wa mafunzo hayo, kila nchi iliandaa mpango wa utekelezaji wa kitaifa unaolenga kuendesha mafunzo ya ndani ya nchi, kuimarisha usimamizi wa kitabibu, kuboresha ubora wa huduma katika vitengo vya lishe na kuharakisha utekelezaji wa taratibu za kitaifa zinazolingana na mapendekezo ya WHO.

Kupitia juhudi hizi, WHO na washirika wake wanatarajia kusaidia kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vinavyotokana na utapiamlo mkali wa kupindukia miongoni mwa watoto barani Afrika na kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata nafasi ya kuishi na kukua katika afya bora.