Vita Ukraine imeingia hatua hatari tuchukue hatua sasa – Guterres
Vita Ukraine imeingia hatua hatari tuchukue hatua sasa – Guterres
- Idadi ya vifo inaongezeka mwaka hadi mwaka
- Matumizi ya silaha nzito yatia hofu zaidi
- Maneno matupu hayatoshi hatua zahitajika
Mzozo wa Ukraine umeingia katika hatua mpya hatari kufuatia mashambulizi makubwa ya Urusi yaliyofanywa tarehe 23 na 24 mwezi huu na kuongezeka kwa vifo vya raia, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Baraza la Usalama lililokutana jijini New York, Marekani alasiri ya Alhamisi kujadili mzozo huo wa miaka minne na miezi mitatu sasa.
Akinukuu takwimu zilizothibitishwa na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, (PHCHR) Guterres amesema “zaidi ya raia 15,000 wameuawa nchini Ukraine tangu uvamizi mkubwa wa Urusi ulipoanza mwezi Februari 2022. Idadi hiyo inajumuisha takribani watoto 800.”
Guterres ameonya kuwa vifo vya raia katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2026 tayari vimezidi viwango vya kipindi kama hicho katika miaka ya 2025, 2024 na 2023, jambo linaloashiria kuzorota kwa mgogoro wa kibinadamu licha ya miaka ya juhudi za kidiplomasia za kimataifa.
Vifo pia nchini Urusi
Guterres pia amebainisha kuongezeka kwa taarifa za vifo vya raia ndani ya Urusi, wakiwemo watoto, huku mashambulizi ya kuvuka mipaka na mashambulizi yanayotumia ndege zisizo na rubani au droni yakiendelea kuongeza madhara ya kibinadamu ya mzozo huo.
Matumizi ya droni
Mkuu huyo wa UN ameelezea hali ya uwanja wa vita kuwa inazidi kuwa ya mbayá na kusababisha vifo licha ya mabadiliko madogo ya maeneo ya kijeshi huku matumizi ya droni yakizidi.
Miundombinu ya kiraia, hasa mifumo ya nishati ya Ukraine, inaendelea kuharibiwa kwa kiwango kikubwa. Wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu pia wameendelea kushambuliwa, huku ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu ukiendelea, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Mwelekeo wa sasa unatia hofu kubwa, diplomasia ichukue nafasi
Katika hotuba yake, Guterres ameonya kuwa mwelekeo wa sasa wa vita hivyo unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi yasiyotarajiwa.
“Hali ya sasa haiwezi kuendelea kwa njia endelevu. Pande zote zibadili mwelekeo mara moja. Mapigano yasitishwe mara moja bila masharti yoyote,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “kile kinachohitajika sasa ni kupunguza mvutano — mara moja na kwa kudumu. Mzunguko huu wa makuaji lazima usimame.”
Amezitaka Urusi na Ukraine kutumia njia za kidiplomasia na kuweka mazingira ya kile alichokiita “amani ya haki, ya kudumu na ya kina,” inayozingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Amehitimisha hotuba yake akisema, “chaguo ni wazi. Wajibu ni wazi. Wakati wa amani ni sasa.”