Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola ikisambaa DRC, Mkuu  wa WHO asihi sitisho la mapigano

Msichana mchanga aliyevaa sare ya shule anaosha mikono yake kwenye chombo cha maji nje ya shule moja nchini DR Congo, huku mwanamume aliyevaa koti la UNICEF na wanafunzi wengine wakitazama.
© UNICEF/Carmel Ndomba Mbikayi Msichana anasafisha mikono yake katika shule ya msingi huko Bunia wakati wa mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ebola ikisambaa DRC, Mkuu  wa WHO asihi sitisho la mapigano

Afya
  • Ni mgongano wa vita na magonjwa
  • Mapigano hasa Ituri yanavuruga mipango ya kudhibiti mlipuko
  • Ni vigumu kuhudumia wagonjwa huku mabomu yanalipuka
  • Kasi ya kusambaa Ebola inazidi kasi ya mwitikio

Pata ripoti ya punde zaidi kutoka WHO kuhusu Ebola hapa

Ongezeko la vurugu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, linakwamisha juhudi za kudhibiti mlipuko wa Ebola, hivyo tunasihi pande zinazohasimiana zisitishe mapigano.

Ni wito wa dharura wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus kwa makundi yaliyojihami eneo hilo ambako ndiko mlipuko wa 17 wa Ebola umeripotiwa na hadi sasa watu 105 wamethibitishwa kuambukizwa aina ya virusi vya Bundibugyo visivyo na tiba wala chanjo , na kati yao hao 10 wamepoteza maisha.

WHO ni shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, ambalo Mkuu wake huyo kupitia ukurasa wake wa X, zamani Twitter anasema anaonya kwamba kuongezeka kwa vurugu kunadhoofisha juhudi za kudhibiti mlipuko unaokua kwa kasi hususan jimboni Ituri ambako ndiko kitovu cha mlipuko wa sasa.

Tweet URL

Vita na ugonjwa vinashindana

Amesema kinachoendelea sasa ni mgongano wa kihistoria katiya magonjwa na mizozo akisema kwamba mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo “unazidi kasi ya mwitikio.”

Dkt. Tedros amekumbusha kuwa virusi vya Ebola vya Bundibugyo havina chanjo wala matibabu yaliyothibitishwa, hivyo “kukomesha maambukizi kunategemea kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa usaidizi wa kibinadamu.”

Hata hivyo wahudumu wa afya wanasema mapigano yanayoendelea kati ya makundi yenye silaha mashariki mwa DRC yamesababisha watu wengi kukimbia makazi yao, na kuwalazimu walio katika hatari ya kuambukizwa kuingia katika kambi za wakimbizi zenye msongamano mkubwa ambako virusi vinaweza kuenea haraka.

Maisha ya raia na wahudumu wa afya hatarini

 Kutokuwa na usalama pia kumevuruga mitandao ya ufuatiliaji na kufunga njia muhimu zinazotumiwa na timu za matibabu kufuatilia waliokutana na wagonjwa na kuwaweka waliothibitishwa kuambukizwa katika maeneo ya kutengwa.

“Wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele wanahatarisha maisha yao, huku mashambulizi dhidi ya vituo vya afya yakifanya kufuatilia wagonjwa na watu waliokutana nao kuwa karibu haiwezekani,” amesema Mkuu wa WHO.

“Hatuwezi kujenga imani ya jamii au kuwaweka wagonjwa katika maeneo ya kutengwa wakati mabomu yanaporushwa,” amesema akiongeza kuwa, “tunaomba mpatie kipaumbele uhai wa binadamu kuliko kitu kingine chochote.”

Ingawa hivyo video ya WHO nchini DRC iliyochapishwa ukurasa wa  X inaonesha wafanyakazi wakiendelea na ujenzi wa vituo vya matibabu dhidi ya Ebola huko Bunia, mji mkuu wa Ituri, ujenzi unaofanyika kwa usaidizi wa serikali ya Uingereza na Mfuko wa Gates.

Mfanyakazi wa afya katika suti nyeupe ya kinga, kinga ya uso, na glavu za bluu anasimama nje karibu na gari la bluu.
© WHO Mfanyakazi wa afya amevaa suti ya kinga wakati wa mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

WHO imeonya kwamba mlipuko huo unaendelea kusambaa kijiografia, huku kukiwa na ushahidi wa maambukizi yanayoendelea kuvuka mipaka.

Mlipuko wa sasa umejikita katika jimbo la Ituri na umeenea katika kanda 11 za afya, huku wagonjwa wakiritipotiwa pia jimboni Kivu Kaskazini — ikiwemo Butembo na Goma — pamoja na Kivu Kusini, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Maafisa wa afya wanasema virusi hivyo vya Bundibugyo ambavyo kwa mara ya kwanza viliripotiwa DRC mwaka 2007, vinaendelea kusambaa kupitia makundi ya kifamilia na vituo vya afya, huku maambukizi yakihusishwa na kuwahudumia wagonjwa, mikusanyiko ya kifamilia na taratibu zisizo salama za mazishi.