Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sauti ya Afrika imepuuzwa kwa muda mrefu, sasa ni wakati wa kupindua ukurasa: Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza kwenye jukwaa wakati wa sherehe za kuanzisha ujenzi wa Kituo Kipya cha Mkutano katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.
UN Nairobi/Abdikarim Haji Katibu Mkuu António Guterres akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuanzishwa kwa ujenzi wa kituo kipya cha mikutano katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.

Sauti ya Afrika imepuuzwa kwa muda mrefu, sasa ni wakati wa kupindua ukurasa: Guterres

Amani na Usalama

Akizungumza katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa mageuzi makubwa katika taasisi za kimataifa, akisema kuwa Afrika inaendelea kukabiliwa na “mfumo usio wa haki wa kimataifa” unaolikosesha bara hilo uwakilishi sawa na fursa za kiuchumi.

Guterres ameyasema hayo leo wakati wa mkutano wake na waandishi na kuongeza kuwa  uwezo mkubwa wa Afrika unakwamishwa na gharama kubwa za mikopo, upatikanaji mdogo wa fedha za mabadiliko ya tabianchi na kutoshirikishwa kikamilifu katika maamuzi ya kimataifa.

Afrika lazima iwe na sauti, uwakilishi na rasilimali zinazostahili watu wake,” amesema Guterres. “Hebu tuongee ukweli mageuzi hayawezi kusubiri.”

Amesema taasisi kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na taasisi za fedha za kimataifa bado zinaakisi hali ya dunia ya miaka mingi iliyopita, akisisitiza kuwa kukosekana kwa uwakilishi wa kudumu wa Afrika Baraza la Usalama ni dhuluma ya kihistoria inayopaswa kurekebishwa.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres na maafisa wamefuta ardhi katika sherehe ya ujenzi wa majengo mapya ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.
UN Nairobi/Julius Mwelu Katibu Mkuu António Guterres (katikati) pamoja na wakuu wengine wa ofisi wakati wa kuzinduliwa kwa majengo mapya ya ofisi katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi na kuanzishwa kwa jengo la mkutano.

Upanuzi wa ofisi Nairobi wadhihirisha nafasi ya Afrika ndani ya UN

Katibu Mkuu huyo ametoa kauli hizo muda mfupi baada ya kuzindua majengo mapya ya ofisi na kuweka jiwe la msingi la kituo kikubwa cha mikutano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika jijini Nairobi.

Ameelezea miradi hiyo kama ishara ya wazi ya kutambua nafasi ya Afrika katika ushirikiano wa kimataifa na diplomasia ya kimataifa.

Guterres almeipongeza Kenya kwa uongozi wake katika diplomasia, ujenzi wa amani, misaada ya kibinadamu na ulinzi wa mazingira, akiitaja nchi hiyo kuwa “mwenyeji mkarimu na mshirika wa kimkakati.”

“Nairobi ni moja ya vituo vya kijani vya Umoja wa Mataifa ni makao makuu pekee ya Umoja wa Mataifa barani Afrika,” amesema. Akiongeza kuwa “Umoja wa Mataifa lazima uwe karibu zaidi na watu unaowahudumia uunganishwe na hali zao halisi, na uwe na uwezo wa kuunga mkono suluhisho wanazojenga.”

UN yaonya juu ya migogoro inayoendelea barani Afrika

Guterres pia ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu migogoro inayoendelea nchini Sudan, Sudan Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Cngo DRC, na eneo la Sahel. Amesema raia ndio wanaoathirika zaidi kupitia vurugu, njaa na uhamaji wa lazima, hasa nchini Sudan ambako matumizi ya ndege zisizo na rubani au droni yamezidisha mashambulizi dhidi ya raia.

“Hakuna suluhisho la kijeshi kwa migogoro hii,” Guterres amesisitiza. “Amani ya kudumu inahitaji ujasiri, mazungumzo, taasisi zinazoaminika na ushirikiano wa kikanda na kimataifa unaoongozwa na Afrika na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.”

Picha ya pembe ya chini ya jengo la saruji la ghorofa nyingi lililoharibiwa sana huko Tehran, Iran. Mbele inaonyesha uharibifu mkubwa na saruji iliyo wazi, madirisha yaliyovunjika, na magofu yaliyotawanyika ardhini. Scaffolding inaonekana kwenye sakafu za juu.
© Mchangiaji Jengo katika Mashariki ya Tehran likionesha uharibifu uliosababishwa na bomu.

Mgogoro wa Iran watishia uchumi na uhakika wa chakula Afrika

Katibu Mkuu huyo pia ameonya kuwa mgogoro unaohusisha Iran tayari unaathiri uchumi wa Afrika kupitia usumbufu wa njia ya mlango bahari wa Hormuz.

Amebainisha kuwa karibu asilimia 13 ya uagizaji wa bidhaa wa Afrika, ikiwemo mafuta na mbolea, hupitia eneo hilo muhimu la usafirishaji.

“Nchi ambazo tayari zinakopa kwa gharama kubwa sasa zinalazimika kulipa zaidi kuagiza nishati au mbolea, kusafirisha bidhaa, kulisha watu na kulinda walio hatarini,” amesema.

Ameongeza kuwa bei ya mbolea ya urea imepanda zaidi ya asilimia 35 ndani ya mwezi mmoja wakati wa msimu muhimu wa kupanda, hali inayozidisha hatari ya ukosefu wa chakula.

UN yasisitiza ushirikiano imara zaidi na Afrika

Akihitimisha, taarifa yake kwa wanahabari Guterres amethibitisha dhamira ya Umoja wa Mataifa kuimarisha ushirikiano wake na Afrika na kuunga mkono suluhu zinazoongozwa na Waafrika.

Amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kusukuma mageuzi ya haki ya tabianchi, amani na uchumi yanayoiwezesha Afrika kupata uwakilishi na rasilimali sawa.

“Afrika inajua gharama ya dhuluma na nguvu ya mshikamano,” amesema. “Ndiyo maana Umoja wa Mataifa unaimarisha mizizi yake barani Afrika kusimama na Waafrika, kuunga mkono uongozi wa Afrika na kusaidia amani, maendeleo na haki ya tabianchi.”