Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mama ni nguzo ya jamii na msingi wa haki za watoto

Mwanamke mweusi aliyevaa koti jekundu anaongea wakati wa mahojiano ya nje mbele ya alama ya Angelica's Home huko Kajiado, Kenya.
Habari za UN Mchungaji Jimono, Mwanzilishi wa Angelica Home na Alter of the Holy one Ministries.

Mama ni nguzo ya jamii na msingi wa haki za watoto

Wanawake

Je wajua nafasi ya mama katika jamii? Dunia ikiwa imeadhimisha siku ya mama Jumapili Mei 10, tunakupeleka kaunti ya Kajiado nchini Kenya ambako nafasi mama ya katika kusongesha haki za kijamii hususan za watoto wao imewekwa bayana.

“Hii ni siku yetu ya akina mama. Tujivunie…mimi namshukuru mama mmoja anayeishi kule Marekani anaitwa Liz, ambaye amenishikilia kama mama, na nawashukuru kinamama wote kwa ujumla.” Amesema Mchungaji Jimono, Mwanzilishi wa Angelica Home, ambacho ni kituo cha malezi na elimu kwa watoto yatima na wale waliokumbwa na dhuluma mbalimbali.

Bi. Jimono anasema iwe ni mama mzazi au mama mlezi, akinamama wote wakishikamana watoto wataweza kutimiza ndoto zao maana watoto ni wa akinamama..…

“Wamama tunaweza kufanya mambo makubwa sana. Tunaweza kusimamia watoto wetu, tunaweza kuwalinda watoto wetu maana watoto wanatutegemea sisi kinamama.”

Shuhuda mwingine wa kazi ya kinamama katika kituo hiki cha watoto ni Beverline Mulago ambaye ni mkazi wa hapa Kajiado, anasema watoto hao wamepata matumaini…

“Katika kituo hiki cha Angelika Foundation nimeona watoto wengi wamekumbatiwa, wale ambao walikuwa wameumizwa wakapona. Wengi walikuwa wamehangaika na hapa wakapata ni mahali pa tumaini. Ni mahali ambapo ukiingia hakika Maisha ya mtoto itabadilika, imebadilisha maisha ya watoto wengi na hata maisha ya jamii imebadilika.”

Mwanamke wa Kenya akiwa amevaa shufu ya rangi ya waridi na koti la manjano anaongea wakati wa mahojiano nje.
Michell Anyango kutoka Kajiado Kenya. Siku ya Mama

Je, kuna mama ambaye unampa shukrani kwa kuchangia Maisha yako? Michell Anyango anatoa shukrani kwa mama ambaye si mzazi wa mtoto wake lakini amesimamia gharama zake za elimu na mahitaji mengine...

“Nashukuru mama mmoja amenitoa mbali, ananisaidia kiuchumi na mtoto wangu saa hii yuko katika kidato cha nne, na ako na nidhamu.  Amesimamia mtoto shuleni kwa kila kitu ambacho mimi singeweza. Mungu ampe maisha marefu kwa sababu baba watoto alikufa, akanisaidia mpaka wa leo ananishika mkono. Nina furaha kwa sababu mimi mwenyewe wazazi wangu hawakuweza kunisomesha lakini nafurahia mtoto wangu, lakini mama huyu anajua hali ya mtoto wangu, ameweza kuendelea na masomo.”

Mchungaji Jimono anatamatisha akitoa wito kwa akinamama wote wasimame pamoja na washikamane kwa upendo..

“Dunia ni mwanamke maana anaitwa She. Bila shaka hizi mambo ndogo ndogo zitaisha, na wewe mama ambaye uko pale unafikiria mume amekuacha labda unajisikia kuwatupa au kuwaacha watoto wako, hapana, wewe ni mama mwenye nguvu. Wewe ni mama ambaye kila siku ana matumaini, na ujue nyuma yako kuna wamama wengine.”

Hakika tunawatakia kinamama wote furara na afya njema katika siku ya kinamama na siku zote za usoni!