Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu yasaini Mkataba wa Nchi Mwenyeji na Somalia
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu yasaini Mkataba wa Nchi Mwenyeji na Somalia
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, pamoja na Waziri wa Familia na Maendeleo ya Haki za Binadamu wa Somalia, Khadiija Mohamed Al-Makhzoumi, hii leo Mei 06, 2026 wamesaini Mkataba wa kwanza wa Nchi Mwenyeji kati ya Umoja wa Mataifa na Somalia.
Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Kamishna Türk ameeleza kufurahishwa kwake na hatua hiyo muhimu, akisema mkataba huo utawezesha kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini humo.
“Ninaukaribisha kwa dhati mkataba huu, ambao utawezesha kuimarisha ushirikiano wetu na Somalia katika kulinda na kukuza haki za binadamu nchini humo,” alisema Türk, akitoa shukrani kwa serikali ya Somalia kwa “nia njema na ushirikiano wao.”
Mkataba huo wa Nchi Mwenyeji ni nini
Mkataba huu unaweka msingi mpana wa utekelezaji wa majukumu ya haki za binadamu nchini Somalia, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji, utoaji wa taarifa, msaada wa kiufundi na shughuli za kujenga uwezo.
Aidha, unatarajiwa kuwezesha kuanzishwa kwa ofisi ya haki za binadamu jijini Mogadishu, hatua ambayo itategemea upatikanaji wa rasilimali fedha.
Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu ameeleza matumaini yake kuwa mkataba huo utakuwa nguzo muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na taasisi zote za dola nchini Somalia, ili kukabiliana na changamoto za haki za binadamu zinazoikabili nchi hiyo na kuhakikisha haki za msingi zinaheshimiwa kwa kila mtu.
“Natumaini mkataba huu utakuwa msingi wa kuimarisha ushirikiano wetu na mihimili yote ya dola ya Somalia, katika kushughulikia changamoto za haki za binadamu zinazoikabili nchi hiyo na kukuza haki za msingi kwa kila mtu,” alisisitiza Kamishna Türk.