Watoto zaidi ya 20 waachiliwa kutoka kituo cha mafunzo ya kijeshi Sudan Kusini: UNMISS
Watoto zaidi ya 20 waachiliwa kutoka kituo cha mafunzo ya kijeshi Sudan Kusini: UNMISS
Zaidi ya wavulana 20 walio chini ya umri wa miaka 18 wameachiliwa kutoka kituo cha mafunzo ya kijeshi mjini Pariang kufuatia operesheni ya uhakiki iliyoongozwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa kushirikiana na wadau wengine.
Wavulana hao 21 wenye umri kati ya miaka 15 na 17 walidaiwa kuingizwa katika mzozo wa silaha baada ya taarifa kuibuka mapema mwaka huu zikidai kuwepo kwa usajili wa lazima wa vijana, wakiwemo watoto, katika eneo la utawala la Ruweng nchini Sudan Kusini.
Operesheni ya pamoja yabaini watoto kambini
Operesheni hiyo ya uhakiki ilifanyika katika kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Manjaba mjini Pariang ikihusisha UNMISS, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Kamati ya Kitaifa ya Mpango Kabambe wa Utekelezaji, Tume ya Kitaifa ya Kupokonya Silaha, Kuwarejesha na Kuwajumuisha Wapiganaji katika Jamii (NDDRC), pamoja na viongozi wa eneo hilo.
“Tulipopita katika gwaride na kufanya uhakiki, tulibaini kuwa watoto 21 walikuwa chini ya umri unaoruhusiwa,” amesema Mwenyekiti wa NDDRC, Anyuen Alier.
Wavulana hao walitoka maeneo ya Jonglei, Greater Pibor, Aweil na Warrap.
Umoja wa Mataifa wataka watoto warejee shuleni
Maafisa wa ulinzi wa watoto wamesisitiza kuwa nafasi ya watoto ni shuleni na si katika vikosi vya kijeshi.
Afisa wa Ulinzi wa Watoto wa UNMISS mjini Bentiu, Pamela Wadegu, amesema ujumbe huo unashirikiana kwa karibu na Vikosi vya Ulinzi vya Sudan Kusini (SSPDF) kuchunguza madai ya kuajiri watoto na kuhakikisha wanaachiliwa.
“Watoto wanapaswa kuwa shuleni majeshi si mahali pao,” amesema. “Tunataka watoto wa nchi hii wapate maisha bora zaidi, ndiyo maana tunashirikiana kuhakikisha wanaachiliwa na kupata nafasi ya pili ya kurejea katika masomo yao.”
Wavulana waeleza furaha baada ya kuachiliwa
Wavulana hao walikuwa wamepitia miezi kadhaa ya mafunzo ya kijeshi huku baadhi yao tayari wakijumuishwa kwenye orodha ya mishahara ya kijeshi.
Licha ya hofu ya awali, wengi wao walionesha furaha baada ya kuvua sare za kijeshi na kuondoka kambini.
“Nitafurahi sana kumuona mama yangu na dada zangu. Sijawaona kwa muda mrefu,” amesema mmoja wa wavulana hao baada ya kuachiliwa.
UNICEF yatoa huduma za ulinzi na urejeshwaji
UNICEF mjini Bentiu imewapokea wavulana wote 21 na kusema watapatiwa ushauri nasaha, msaada wa kisaikolojia pamoja na shughuli za burudani kabla ya kurejeshwa kwa familia zao.
“Tutaangalia ustawi wao hadi watakapounganishwa tena na familia zao kwa kuhakikisha wanapata msaada wa kisaikolojia, ushauri nasaha na kushiriki katika shughuli za burudani,” amesema Mkuu wa UNICEF Bentiu, Luel Ding.
Kuachiliwa huku kunafuatia operesheni kama hiyo iliyofanyika mwezi Aprili ambapo wapiganaji watoto 23 pia waliachiliwa kutoka mafunzo ya kijeshi mjini Malakal katika jimbo la Upper Nile.
UNMISS imesema itaendelea kushirikiana na mamlaka za kitaifa pamoja na wadau kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kumaliza ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto, ikiwemo uandikishaji wa watoto vitani kwa nguvu.