Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Abiria mwingine athibitishwa kuwa na ugonjwa wa virusi vya Hanta

Picha ya mikroskopu ya chembe za Hantavirus zenye rangi ya kijani kwenye mandhari nyeupe.
© CDC Ugonjwa wa virusi vya Hanta (ugonjwa unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya HPS au yasiyo ya HPS) ni hali inayotakiwa kuripotiwa kitaifa.

Abiria mwingine athibitishwa kuwa na ugonjwa wa virusi vya Hanta

Afya

Imethibitishwa kuwa abiria mwingine aliyekuwa kwenye meli ya kitalii iliyohusishwa na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Hanta au Hantavirus ameambukizwa ugonjwa huo, ugonjwa ambao tayari umeua watu watatu waliokuwa ndani ya meli na kusababisha tahadhari ya kimataifa iliyoratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) la Umoja wa Mataifa. 

Duru za habari zinaeleza kuwa mtu huyo ni mwanaume na alikuwemo kwenye meli hiyo iliyopatiwa jina Hondius, ikipeperusha bendera ya Uholanzi. Kwa sasa anapatiwa matibabu katika hospitali moja mjini Zurich nchini Uswisi baada ya kurejea nchini humo na kujibu barua pepe kutoka kwa mwendeshaji wa meli hiyo.

Ufuatiliaji unaendelea na kusaidia waliomo kwenye meli

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO kupitia ukurasa wake wa X linasema kwa mujibu wa kanuni za kimataifa za afya za shirika hilo, WHO inashirikiana na nchi husika kusaidia ufuatiliaji wa mawasiliano wa kimataifa, ili kuhakikisha kuwa wale waliodhurika wanafuatiliwa na kwamba kuenea zaidi kwa ugonjwa kunazuiliwa.

WHO inasema hadi kufikia leo Jumatano, abiria watatu kati ya 147 waliokuwa ndani ya meli hiyo wamefariki dunia tangu ilipoanza safari yake kuvuka Bahari ya Atlantiki kutoka Argentina hadi ilipoegeshwa sasa karibu na pwani ya Cabo Verde.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia ukurasa wake wa X ameripoti kuwa abiria watatu wamehamishwa hivi punde kutoka kwenye meli hiyo na walikuwa njiani kuelekea Uholanzi kwa ajili ya matibabu.

Ingawa hivyo amerejelea kauli ya WHO kwamba kwa hatua ya sasa  hatari ya jumla kwa afya ya umma bado iko chini.

Ifahamu meli Hondius

Taarifa zilizo hadharani zinaonysha kuwa Hondius ilitengenezwa nchini Croatia na kuzinduliwa Juni 2018. Ina urefu wa takribani mita 108 na imesajiliwa chini ya nambari ya utambulisho wa meli 9818709 katika Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya bahari, IMO.

Meli hiyo ina uwezo wa kubeba abiria 196 na wafanyakazi 72; imepewa jina la mchapishaji wa ramani na mchongaji wa karne ya 17, Jodocus Hondius.

Safari yake ya kwanza mwaka 2019 ilianzia Vlissingen nchini Uholanzi hadi kisiwa cha volkeno cha Jan Mayen na Spitzbergen katika ncha ya dunia ya Aktiki.

Pengine maambukizi kabla ya kupanda melini

WHO inasema huenda waathiriwa waliambukizwa ugonjwa huo kabla ya kupanda meli na hadi sasa kuna maambukizi miongoni mwa watu wanane na kati yao wagonjwa watatu wamethibitishwa kwenye maabara kuwa na virusi vya Hanta vya Andes vinavyokumba zaidi nchi za kusini mwa Amerika.

Jana Jumanne, WHO ilisema kuwa mtu mmoja alikuwa katika chumba cha wagonjwa mahututi, nchini Afrika Kusini, ingawa hali yake ilikuwa “inaimarika”.

WHO imebainisha kuwa kazi ya kubaini virusi imehusisha Taasisi ya Kitaifa ya Magonjwa ya Kuambukiza nchini Afrika Kusini na Hospitali za Chuo Kikuu cha Geneva (HUG).

Taasisi ya Pasteur mjini Dakar, Senegal na Mamlaka ya Kitaifa ya Maabara na Taasisi za Afya ya Argentina pia zilitoa msaada mwingine muhimu.

Huduma kwa wagonjwa ni ‘kipaumbele cha juu’

WHO imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na nchi kuhakikisha kuwa wagonjwa, wale waliokaribiana nao, abiria na wafanyakazi wanapata taarifa na msaada wanaohitaji ili kubaki salama na kuzuia kuenea kwa ugonjwa.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne, WHO ilisema kuwa “kipaumbele cha juu zaidi” ni kuwaondoa abiria wawili wagonjwa waliobaki ndani ya meli “ili kuhakikisha wanapata huduma wanayohitaji”.

Mara tu meli itakapofika visiwa vya Canary, Dkt. Maria Van Kerkhove mamlaka za Hispania zitafanya uchunguzi kamili wa magonjwa  pamoja na usafishaji kamili wa meli, kabla ya kutathmini hatari kwa abiria waliobaki ndani.

Kama tahadhari, abiria wameombwa kubaki kwenye vyumba vyao wakati shughuli za usafishaji na hatua nyingine za afya ya umma zikiendelea.