Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Tanzania inajali usawa na haki kwa watu wote kupata huduma kwa usawa – Hamisi Masanja Malebo

Wanaume wawili wanakaa kwenye meza ya mviringo wakiwa na maikrofoni katika studio wakati wa mahojiano, wakiwa na nembo kubwa ya Umoja wa Mataifa inayoonekana kwenye skrini nyuma yao.
Habari za Umoja wa Mataifa/Flora Nducha Profesa Hamisi Masanja Malebo (kulia) kutoka Tanzania akizungumza na Feissal Kibet (kushoto) wa UN News Kiswahili kandoni mwa mkutano wa watu wa asili jijini New York, Marekani.

Serikali ya Tanzania inajali usawa na haki kwa watu wote kupata huduma kwa usawa – Hamisi Masanja Malebo

Tabianchi na mazingira

Siku tano zilizopita Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) limefunga pazia hapa katika makao ya Umoja wa Mataifa  jijini New York, Marekani  baada ya majadiliano ya takribani wiki mbili ya wadau kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu sera, mafanikio na kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kuhudumia wananchi wao ikiwemo jamii za watu wa asili. Kwa upande wa Tanzania, mmoja wa walioshiriki ni Katibu Mtendaji wa Tume ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO ya Taifa la Tanzania, Profesa Hamisi Masanja Malebo.

Feisal Kirwa wa idhaa hii alifanya mahojiano naye kwanza akitaka kufahamu Tanzania ina mikakati gani ya kuhakikisha watu wa asili wanajumuishwa katika huduma za afya kwa wote?

“Serikali ya Tanzania inajali sana usawa na haki kwa Watanzania wote kupata huduma bila ubaguzi. Huduma za jamii na afya zinatolewa kwa wote bila kujali kundi au asili ya mtu. Hakuna upendeleo, na hakuna kundi lenye haki zaidi ya lingine. Tanzania imeendelea kujenga taifa lenye mshikamano na usawa kwa wananchi wote.” Amesema Profesa Malebo.

Katika muktadha wa kimataifa, changamoto ya mabadiliko ya tabianchi imeendelea kuathiri jamii nyingi, hususan watu wa asili. Tanzania ina mikakati gani kukabiliana na hali hii?

Mwanamume mwenye suti ya kijivu na miwani ameketi mbele ya bendera ya rangi ya bluu ya Umoja wa Mataifa.
Habari za Umoja wa Mataifa/Flora Nducha Profesa Hamisi Masanja Malebo kutoka Tanzania wakati wa mazungumzo na Feissal Kibet wa UN News Kiswahili kandoni mwa mkutano wa watu wa asili jijini New York, Marekani.

“Ni kweli kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaathiri pia Tanzania kama zilivyo nchi nyingine. Serikali imeweka mikakati mbalimbali kulingana na mazingira wanayoishi wananchi wake. Kuna makundi yenye mahitaji maalum kama Wahadzabe, Wadatoga, Akie na Wasandawe ambao wanaishi katika mazingira ya asili. Endapo kutatokea upungufu wa chakula, serikali huwasaidia kwa kuwapelekea misaada." Amasema.

Anaongeza kuwa "Kwa upande wa wafugaji kama Wamasai na Wasukuma, ambao huathirika na ukame, serikali inahakikisha wanapata maeneo salama zaidi ya kuishi na kufuga. Aidha, kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi ya mafuriko, tayari wamepewa maelekezo na kusaidiwa kupata maeneo mbadala yaliyo salama zaidi, hususan maeneo ya miinuko ili kuepuka athari za mafuriko.”