UNICEF yaongoza kampeni kukomesha adhabu ya viboko shuleni nchini Tanzania
UNICEF yaongoza kampeni kukomesha adhabu ya viboko shuleni nchini Tanzania
Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu za Viboko huadhimishwa Aprili 30 ya kila mwaka, na mwaka huu katika maadhimisho ya siku hiyo wiki iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa haki za binadamu na elimu lilizindua kampeni iitwayo ‘No Collabo’ iliyolenga kukomesha adhabu ya viboko kwa mtindo ambao walimu zaidi ya mmoja humchapa mwanafunzi viboko kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa Waraka wa Elimu Na. 24 wa mwaka 2002 nchini Tanzania, adhabu ya viboko inaruhusiwa katika hali ya utovu mkubwa wa nidhamu kiasi cha kuivunjia shule heshima au makosa ya jinai, kwa kuzingatia vigezo maalum, ikiwemo umri wa mwanafunzi, hali yake ya afya na aina ya kosa. Aidha, waraka huo unaweka kikomo cha viboko visivyozidi vinne, kwa ruhusa ya maandishi kutoka kwa Mwalimu Mkuu.
Je, hali halisi ikoje?
Nimekutana na wazazi mbalimbali wallionipa maoni yao wa kwanza ni Bi. Gati Mgosi.
“Yaani sasa utaratibu unakosekana, mwalimu anapiga mpaka mgongoni, mikononi, yaani kama mimi mwanangu alikuja mpaka mikono hawezi kushika vitu, imevimba. Nilichukia nilienda mpaka kwa Afisa Elimu nikalalamika, nashukuru yule baba alinisikiliza tulienda ile changamoto ikaisha, lakini alimpiga mpaka akamchania shati ya shule. Yule ni mtoto wa kike na anampiga hadi mitama unadhalilisha kisa shilingi 200 ya masomo ya ziada,” .
Kisha, Bi. Prisca Stephano,ambaye anasema mbali na kutweza utu wa mtoto adhabu hizo zina madhara ya kisaikolojia.
“Zinamtengenezea mtoto madhara hata na akili ina hama na mtoto anapata woga shuleni, muda wote ana wasiwasi ‘nikifanya hivi watanipiga’ mwishowe mtoto anakataa shule.”
Matukio ya kujeruhiwa, ulemavu, na vifo si mageni, kutokana na adhabu hizo Karumuna Theonest, anatahadharisha.
“Vifo vipo vimekuwepo tumeviona lakini jambo lingine pia tumeona madhara ya kupata ulemavu” .
Mzazi mwingine, ni Bw. Murshid Sadick yeye anataka walimu wawajibishwe.
“Sasa basi, walimu wanaotoa adhabu hizo wanastahili kuwajibishwa, inatakiwa wawajibishwe kulingana na wanatoa adhabu ambazo sio sahihi. Mwanafunzi anainamishwa chini ya meza, mtu anapigwa na kiti au ubao, hiyo sio adhabu hayo ni mateso” .
Huko shule ya msingi Itumba, wilaya ya Momba, mkoani Songwe, nyanda za juu kusini mwa Tanzania, hali ni tofauti, mwalimu Joseph Swaga hutumia majukwaa ya mitandao ya kijamii kuonesha namna nyimbo na michezo ilivyo njia bora ya kujifunzia. Nini kilimsukuma? Anafunguka
“Mimi ni muumini sana wa nyimbo na michezo kwahiyo nikaona ni mbinu bora yakutumia kwa ajili ya kufundishia wanafunzi wangu. Wanaweza kufurahia masomo mbalimbali, pia wanakuwa na ukaribu zaidi na nwalimu na kumshirikisha kuhusu changamoto ambazo wanafunzi wanakumbana nazo, inawafanya wanapenda shule na mahudhurio yanaongezeka” .
Kampeni hiyo ya UNICEF imelenga kukomesha adhabu za kikatili kwa watoto na kuhimiza njia mbadala za malezi bora shuleni.