Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Virusi vya Hanta

Mwanateknolojia wa kike anayeveka koti nyeupe la maabara anafanya kazi kwenye bodi ya mzunguko katika maabara ya sayansi na teknolojia nchini Uganda, kama sehemu ya mpango wa Sekretarieti ya STI.
UNTB/Elçin Torlak Wanafunzi wakichunguza virusi na magonjwa mengine katika mafunzo kwenye maabara.

Virusi vya Hanta

Afya
  • Virusi vya Hanta ni kundi la virusi vinavyobebwa na panya na vinaweza kusababisha magonjwa makali kwa binadamu.
  • Maambukizi hutokea mara nyingi kwa kumgusa panya aliyeambukizwa au mkojo, kinyesi au mate yake.
  • Maambukizi yanaweza kusababisha aina mbalimbali za magonjwa, ikiwa ni pamoja na ugonjwa mkali na hata kifo.

Virusi vya Hanta ni nini

Chapisho la WHO linaainisha kuwa virusi vya Hanta ni virusi vya magonjwa ya kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, vinavyoishi kwa kawaida kwa panya na wakati mwingine huambukizwa kwa binadamu. 

Maambukizi kwa binadamu yanaweza kusababisha ugonjwa mkali na mara nyingi kifo, ingawa dalili hutofautiana kulingana na aina ya virusi na eneo la kijiografia.

Katika bara la Amerika, ugonjwa unaojulikana zaidi ni Ugonjwa wa virusi vya Hanta unaoshambuliwa kwa kasi mapafu na moyo, HCPS, Ulaya na Asia, ugonjwa unaojitokeza zaidi ni Homa ya kuvuja damu inayoambatana na kushindwa kwa figo HFRS, unaoathiri figo na mishipa ya damu.

Picha ya mikroskopu ya chembe za Hantavirus zenye rangi ya kijani kwenye mandhari nyeupe.
© CDC Ugonjwa wa virusi vya Hanta (ugonjwa unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya HPS au yasiyo ya HPS) ni hali inayotakiwa kuripotiwa kitaifa.

Hakuna tiba dhidi ya virisu vya Hanta

Hakuna tiba maalum ya kuponya virusi vya Hanta, lakini matibabu ya msaada wa kitabibu mapema ni muhimu ili kuongeza nafasi ya kupona. Kinga hutegemea kupunguza mawasiliano kati ya binadamu na panya.

Mzigo wa Ugonjwa

Maambukizi ya virusi vya Hanta si ya kawaida sana duniani, lakini yana kiwango kikubwa cha vifo:

  • Asia na Ulaya: chini ya 1% hadi 15%
  • Amerika: hadi 50%

Kila mwaka, inakadiriwa watu 10,000 hadi zaidi ya 100,000 huambukizwa duniani, wengi wao wakiwa Asia na Ulaya.

Maambukizi

Maambukizi hutokea kupitia:

  • Kugusa mkojo, kinyesi au mate ya panya walioambukizwa
  • Kung’atwa na panya (nadra)
  • Shughuli kama kusafisha maeneo yasiyo na hewa ya kutosha, kilimo, misitu, au kuishi maeneo yenye panya wengi

Maambukizi kutoka mtu hadi mtu yameripotiwa tu kwa virusi vya Andes, na hutokea kwa mawasiliano ya karibu na ya muda mrefu.

Dalili

Dalili huanza kati ya wiki 1 hadi 8 baada ya maambukizi:

  • Homa
  • Maumivu ya kichwa
  • Maumivu ya misuli
  • Kichefuchefu, kutapika au maumivu ya tumbo
HCPS inaweza kusababisha:
  • Kikohozi
  • Kupumua kwa shida
  • Maji kwenye mapafu
  • Mshtuko wa mwili
HFRS inaweza kusababisha:
  • Shinikizo la chini la damu
  • Kutokwa na damu
  • Kushindwa kwa figo
Meli kubwa nyeupe ya kusafiri inavuka bahari siku yenye mawingu.
© Unsplash/Yiran Ding Meli ya kitalii inavuka bahari.

Utambuzi wa ugonjwa

Utambuzi wa mapema wa maambukizi ya virusi vya Hanta  unaweza kuwa changamoto kwa sababu dalili za awali hufanana na magonjwa mengine yenye homa au ya mfumo wa upumuaji, kama vile mafua, coronavirus">COVID-19, nimonia ya virusi, leptospirosis, Homa ya Dengue na sepsis.

Hivyo, historia ya mgonjwa inapaswa kuchunguzwa kwa makini, kwa kuzingatia hasa uwezekano wa kuwasiliana na panya, hatari zinazohusiana na kazi na mazingira, historia ya safari, pamoja na mawasiliano na wagonjwa wanaojulikana katika maeneo yenye virusi vya Hanta.

Uthibitisho wa maabara hutegemea vipimo vya serolojia ili kubaini kingamwili maalum za virusi vya Hanta au ongezeko la viwango vyake, , pamoja na mbinu za kijenetiki .

Umakini wakati wa kupima sampuli

Sampuli zinazochukuliwa kutoka kwa wagonjwa ni hatari kwa usalama wa kibiolojia; hivyo, upimaji wa maabara kwa sampuli ambazo hazijapunguzwa nguvu unapaswa kufanyika katika mazingira yenye kiwango cha juu cha udhibiti wa kibaolojia.

Sampuli zote za kibiolojia ambazo hazijapunguzwa nguvu zinapaswa kufungashwa kwa kutumia mfumo wa vifungashio vitatu (triple packaging system) wakati wa kusafirishwa ndani ya nchi na kimataifa.

 Matibabu

Hakuna dawa maalum ya kuua virusi iliyosajiliwa wala chanjo kwa ajili ya maambukizi ya virusi vya Hanta.

Matibabu ni ya kusaidia na hulenga ufuatiliaji wa karibu wa hali ya mgonjwa pamoja na kudhibiti matatizo ya mfumo wa upumuaji, moyo na figo. Upatikanaji wa mapema wa huduma za wagonjwa mahututi (ICU), inapohitajika kitabibu, huongeza nafasi ya kupona, hasa kwa wagonjwa wenye ugonjwa wa hantavirus wa moyo na mapafu (HCPS).

Kinga na Udhibiti

Kuzuia maambukizi ya virusi vya Hanta kunategemea hasa kupunguza mawasiliano kati ya binadamu na panya. Hatua madhubuti ni pamoja na:

  • Kudumisha usafi wa nyumba na sehemu za kazi
  • Kuziba mianya inayoruhusu panya kuingia majengoni
  • Kuhifadhi chakula kwa usalama
  • Kutumia mbinu salama za kusafisha maeneo yaliyochafuliwa na panya
  • Kuepuka kufagia au kutumia mashine ya kuvuta vumbi kinyesi cha panya bila unyevunyevu
  • Kulowesha maeneo yaliyochafuliwa kabla ya kusafisha
  • Kuimarisha usafi wa mikono

Wakati wa milipuko au panaposhukiwa kuwepo kwa maambukizi, ni muhimu kutambua wagonjwa mapema na kuwatenga, kufuatilia waliokaribiana nao, na kutumia hatua za kawaida za kuzuia maambukizi ili kuzuia kuenea zaidi.

Udhibiti wa maambukizi katika vituo vya afya

Ushahidi uliopo unaonesha kuwa hatari ya maambukizi ya virusi vya Hanta katika mazingira ya huduma za afya, ikiwemo virusi vya Andes, ni ndogo sana ikiwa hatua sahihi za kuzuia na kudhibiti maambukizi zinazingatiwa. Katika vituo vya afya, tahadhari za kawaida zinapaswa kutumika kwa wagonjwa wote, ikiwa ni pamoja na usafi wa mikono na ushughulikiaji salama wa damu na majimaji ya mwili.

Mwitikio wa WHO

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO,  hushirikiana na nchi na wadau wake kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, uwezo wa maabara, mawasiliano ya hatari, ushirikishwaji wa jamii, utambuzi wa mapema, huduma kwa wagonjwa na mwitikio wa milipuko ya virusi vya Hanta.

Hii inajumuisha kuandaa na kusasisha miongozo inayotegemea ushahidi kuhusu uchunguzi, usimamizi wa wagonjwa, udhibiti wa maambukizi na ufuatiliaji wa waliokaribiana na wagonjwa.

WHO pia inahamasisha mbinu jumuishi ya One Health, inayozingatia uhusiano kati ya afya ya binadamu, wanyama (hasa panya) na mazingira, na kusaidia nchi kupitia upya ushahidi mpya ili kuhakikisha mapendekezo yanabaki kuwa ya kisasa.