Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti mpya ya UN yafichua udhaifu wa mifumo ya kidijitali na kuonya hatari ya “janga la kidijitali”

Maandishi kwa lugha ya teknolojia au coding kwenye kompyuta.
Unsplash/Markus Spiske Maandishi kwa lugha ya teknolojia au coding kwenye kompyuta.

Ripoti mpya ya UN yafichua udhaifu wa mifumo ya kidijitali na kuonya hatari ya “janga la kidijitali”

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti mpya ya pamoja ya Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU), Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Maafa (UNDRR), na Sciences Po inaonya kuwa mifumo ya kidijitali ya dunia iliyounganishwa kwa karibu inazidi kuwa dhaifu na inaweza kusababisha mtikisiko mkubwa unaoweza kuibua kile wataalamu wanachokiita “janga la kidijitali.” 

Utafiti huo unachunguza hatari kama dhoruba za jua, kukatika kwa nyaya za chini ya bahari, hitilafu za satelaiti na hali mbaya ya hewa inayoweza kuvuruga mawasiliano duniani.

Miundombinu muhimu iko katika tishio kubwa

Ripoti hiyo yenye kichwa “Wakati mifumo ya kidijitali inashindwa: Hatari zilizojificha za dunia yetu ya kidijitali,” inaeleza jinsi hitilafu moja inavyoweza kuathiri sekta nyingi na kuvuka mipaka ya nchi, na kuathiri huduma za afya, fedha na uokoaji wa dharura. 

Inaonya kuwa joto kali linaweza kuzima vituo vya takwimu, huku matetemeko au kukatika kwa nyaya za baharini vikikata mawasiliano ya intaneti kwa wiki kadhaa.

Mashirika ya UN yaitaka dunia kuchukua hatua

Wataalamu kutoka nchi 12 wanasisitiza kuwa miundombinu ya kidijitali lazima ichukuliwe kama huduma muhimu za msingi. 

“Mnepo lazima ujengwe ndani ya DNA ya teknolojia tunazotegemea,” amesema Katibu Mkuu wa ITU Doreen Bogdan-Martin. 

Ameongeza kuwa “Lazima tubadilishe jinsi tunavyolinda mifumo inayounganisha na kuwawezesha wanadamu.”

Teknolojia ya habari 'imesonga mbele' zaidi ya miaka 30 iliyopita.
Unsplash/Markus Spiske Teknolojia ya habari 'imesonga mbele' zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Hatari za mlolongo wa kimataifa

Maafisa wa UNDRR wanaonya kuwa jamii za kisasa ziko katika hatari ya kushuhudia athari za mnyororo wa hitilafu. 

“Kadri jamii zetu zinavyozidi kutegemea teknolojia za kidijitali, usumbufu unaosababishwa na majanga unaweza kusambaa katika mifumo na mipaka ya nchi,” alisema Kamal Kishore, Mkuu wa UNDRR. 

Ameongeza kuwa “Miundombinu ya kidijitali lazima iwe miundombinu yenye mnepo.”

Udhaifu uliofichika katika dunia iliyounganishwa

Ripoti inaeleza kuwa ingawa teknolojia za kidijitali zimeleta mabadiliko makubwa duniani, utegemezi huo umepunguza uwezo wa kutumia mifumo mbadala kama ile ya zamani. 

Wataalamu wanaonya kuwa mifumo inaposhindwa, jamii nyingi zitakuwa na changamoto kubwa kwa kukosa mbadala wa nje ya mtandao.

Wito wa maandalizi ya pamoja duniani

Waandishi wa ripoti hiyo wanazitaka serikali na sekta binafsi kuchukua hatua mara moja, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mipango ya hatari, uratibu wa kimataifa kuhusu satelaiti na nyaya za mawasiliano, na kuongeza uhimilivu wa jamii. 

“Ripoti hii inaonesha jinsi utungaji sera unaotegemea ushahidi unavyoweza kutusaidia kujenga mnepo katika dunia inayozidi kuunganishwa,” amesema Arancha González wa Sciences Po, akitoa wito wa hatua za haraka za kuzuia mgogoro wa kidijitali wa baadaye.