WHO: Mlipuko wa hatari wa hantavirus kwenye meli ya watalii wachunguzwa
WHO: Mlipuko wa hatari wa hantavirus kwenye meli ya watalii wachunguzwa
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO) linasema mlipuko wa virusi vya hanta au hantavirus ulioibuka kwenye meli ya watalii katika Bahari ya Atlantiki unaweza kuhusisha maambukizi machache ya binadamu kwa binadamu, ingawa hali hiyo ni nadra.
WHO inasema baadhi ya abiria huenda waliambukizwa kabla ya kupanda meli hiyo, huku wengine huenda waliambukizwa wakati wa safari kupitia visiwa ambako kuna uwezekano wa kugusana na panya wanaobeba virusi hivyo.
Watu saba wameambukizwa, watatu wamefariki dunia
Kwa mujibu wa WHO Watu saba kati ya abiria na wahudumu 147 wameugua huku wengine wakifariki dunia.
Mkuu wa Kitengo cha WHO cha Maandalizi na Kinga dhidi ya Milipuko na Majanga ya Magonjwa Dkt. Maria Van Kerkhove, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba “Kufikia leo, watu saba kati ya abiria na wahudumu 147 wameripotiwa kuugua. Kwa masikitiko, watu watatu wamefariki dunia. Mgonjwa mmoja amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi nchini Afrika Kusini, ingawa tunaelewa kuwa hali yake inaendelea kuimarika, huku wagonjwa wawili wakiwa bado ndani ya meli na wanaandaliwa kuhamishiwa nchiniUholanzi kwa matibabu.”
Uhamisho wa wagonjwa na hatua za dharura zinaendelea
WHO inasema kipaumbele chake ni kuhamisha wagonjwa hao wawili kwenda Uholanzi kwa matibabu ya haraka.
Hakuna wagonjwa wengine wapya waliogunduliwa ndani ya meli, ingawa mtu mmoja aliyekuwa na homa kidogo sasa anaendelea vizuri.
Abiria wameagizwa kubaki ndani ya vyumba vyao wakati usafishaji na hatua za afya ya umma zinaendelea, huku timu za matibabu kutoka Cabo Verde zikitoa msaada.
Meli kuelekea visiwa vya Canary kwa uchunguzi zaidi
Meli hiyo inatarajiwa kuelekea Visiwa vya Canary, ambapo mamlaka za Hispania zitafanya uchunguzi kamili wa epidemiolojia na usafishaji wa meli hiyo, limesema shirika la WHO.
Dkt Maria Van Kerkhove, amesema mamlaka pia zitachunguza hatari kwa abiria kutoka mataifa zaidi ya 20 walioko ndani ya meli hiyo.
Chanzo kinahusishwa na panya
Virusi vya hantavirus kwa kawaida huenezwa kupitia kugusana na panya walioambukizwa au mkojo, kinyesi au mate yao. WHO inakadiria kuwa maelfu ya maambukizi hutokea kila mwaka duniani.
Maafisa wanaamini wagonjwa wa kwanza, mume na mke waliopanda meli kutoka Argentina, huenda waliambukizwa kabla ya safari kutokana na kipindi cha kuchukua dalili cha wiki 1 hadi 6.
Hata hivyo, WHO inasema maambukizi machache ya mtu kwa mtu hayawezi kutengwa, hasa kwa waliokuwa na mawasiliano ya karibu kama wanaoshiriki chumba, hali iliyowahi kuripotiwa kwa nadra katika milipuko ya virusi vinavyohusiana.
Hakuna tiba maalum, ya Hantavirus
Hakuna tiba maalum ya hantavirus. WHO inasema matibabu hulenga kusaidia dalili, hasa msaada wa kupumua, huku baadhi ya wagonjwa wakihitaji mashine za kusaidia kupumua au uangalizi wa hali ya juu hospitalini.
Dkt Van Kerkhove amewahimiza abiria kuwa watulivu, akisema WHO inashirikiana na waendeshaji wa meli na nchi za asili kuhakikisha huduma na kurudishwa kwao salama.
“Tunakusikia. Tunajua mnaogopa,” amesema, akiongeza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha abiria wanapata matibabu na kurudi nyumbani salama.