WHO yaadhimisha Siku ya Usafi wa Mikono Duniani 2026 kwa wito wa kuimarisha udhibiti wa maambukizi
WHO yaadhimisha Siku ya Usafi wa Mikono Duniani 2026 kwa wito wa kuimarisha udhibiti wa maambukizi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO limehimiza juhudi zaidi za kuhakikisha usafi wa mikono unazingatiwa katika huduma za afya, likisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza maambukizi.
Taarifa iliyotolewa na WHO kupitia kampeni yake ya kimataifa ya Okoa Maisha: Osha Mikono Yako(SAVE LIVES: Clean Your Hands), inaeleza kuwa maadhimisho ya Siku ya Usafi wa Mikono Duniani 2026 (WHHD 2026) yanalenga kuhamasisha umuhimu wa usafi wa mikono katika kudhibiti maambukizi ndani ya mifumo ya afya duniani.
Maadhimisho haya, yanayofanyika kila mwaka tangu 2009, mwaka huu yanaadhimisha miaka 18 ya kampeni hiyo, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Hatua huokoa maisha.”
Umuhimu wa usafi wa mikono waangaziwa
Kwa mujibu wa WHO, maambukizi mengi yanayotokea wakati wa utoaji wa huduma za afya yanaweza kuzuilika kwa urahisi kupitia usafi sahihi wa mikono.
Shirika hilo linaeleza kuwa hatua hiyo husaidia pia:
· Kupunguza gharama za huduma za afya
· Kupunguza mzigo wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa (AMR)
· Kuboresha ubora wa huduma kwa wagonjwa
Changamoto katika utekelezaji
Pamoja na umuhimu huo, WHO imebainisha kuwa bado kuna changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa hatua za usafi wa mikono, zikiwemo:
· Ukosefu wa maji na huduma za usafi wa mazingira (WASH)
· Miundombinu duni katika vituo vya afya
· Ukosefu wa rasilimali na mifumo madhubuti ya kudhibiti maambukizi
Changamoto hizi zinaathiri hasa nchi zenye rasilimali chache na kudhoofisha juhudi za kuhakikisha usalama wa wagonjwa na wahudumu wa afya.
Wito wa hatua za pamoja
Katika kukabiliana na hali hiyo, WHO imetoa wito kwa wadau wa afya duniani kuchukua hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na:
· Kuzingatia mbinu sahihi za usafi wa mikono kulingana na “Nyakati 5 Muhimu”
· Kuingiza usafi wa mikono katika mipango ya kitaifa ya kudhibiti maambukizi (IPC)
· Kufuatilia utekelezaji na kutoa mrejesho wa mara kwa mara
· Kuimarisha uwekezaji katika mifumo ya afya na miundombinu ya usafi
· Kuchukua hatua za kitaifa kuboresha mifumo ya IPC ifikapo mwaka 2030
Wito wa kuimarisha mifumo ya afya
WHO imehitimisha kwa kusisitiza kuwa usafi wa mikono ni hatua rahisi lakini yenye athari kubwa katika kuokoa maisha.
Shirika hilo limetoa wito kwa nchi wanachama na wadau kuimarisha mifumo ya afya, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za usafi, na kuendeleza juhudi za pamoja katika kudhibiti maambukizi duniani.