Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya hatari na machafuko, wakunga wanasaidia wanawake wakimbizi Musenyi Burundi

Mwanasaidizi wa uzazi mwanamke mwenye mavazi ya bluu anamtunza mama aliyebeba mtoto wake mchanga ndani ya hema la matibabu huko Burundi.
© UNFPA Burundi/Alec Junior Rumbete Mkunga akiongea na mama katika zahanati inayoungwa mkono na UNFPA katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi katika Mkoa wa Burunga, Burundi.

Licha ya hatari na machafuko, wakunga wanasaidia wanawake wakimbizi Musenyi Burundi

Wahamiaji na Wakimbizi

Wangunga ni wadau muhimu katika kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa sama, kabla, wakati na baada ya kujifungua limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watun a Afya ya Uzazi UNFPA.

Katika kuadhimisha siku hii leo tunakupeleka MaziwaMakuu nchini Burundi kwenye makazi ya wakimbizi ya Musenyi kusikia mchango Mkubwa unaotolewa na wakunga kwa jamii hiyo ya wakimbizi.

“Nilipogundua kuwa nina ujauzito, niliogopa sana kwa sababu nilijua kujifungua kungekuwa hatari kwangu,” anasema Maombi Kijijwa mwenye umri wa miaka 36.

Mwaka mmoja kabla, Bi. Kijijwa, mume wake na watoto wao 13 walikimbia makazi yao Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, baada ya wanamgambo wenye silaha kuvamia usiku wa manane na kuwaua baadhi ya ndugu na marafiki zao.

Baada ya safari ya siku tatu kwa miguu, familia hiyo iliingia Burundi na kuhamishiwa katika eneo la wakimbizi la Musenyi.

Madaktari walikuwa wamewaonya wanandoa hao kuwa ujauzito mwingine ungekuwa na hatari kubwa. Miaka ya kupata mimba kwa vipindi vifupi ilikuwa imeathiri afya yake vibaya na kumweka katika hatari ya matatizo makubwa ya kiafya yanayoweza kuhatarisha maisha.

“Mwili wangu ulikuwa umechoka, na nilijua kwamba kama ningeendelea kupata watoto kwa namna hii, ningeweza kufa,” Bi. Kijijwa ameliiambia Shirika la UNFPA.

Nilikuwa nikisali nipate suluhisho la kutopata watoto zaidi. Nilijua kujifungua kungekuwa hatari kwangu – Bi. Kijijwa

Mwanamke anayebeba mtoto anapita karibu na hema la muda la matibabu katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi nchini Burundi, huku wafanyakazi wa UNFPA wakiwa wamesimama karibu.
© UNFPA/Alec Junior Rumbete Kliniki ya afya inayoungwa mkono na UNFPA katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi katika Mkoa wa Burunga, Burundi, inawasaidia angalau wanawake 15 kila wiki wakati wa kujifungua.

Upungufu wa wakunga

Wakunga wanaweza kutoa karibu huduma zote muhimu za afya ya uzazi, lakini kuna upungufu wa angalau wakunga milioni moja duniani, kwa mujibu wa UNFPA na  zaidi ya nusu ya pengo hilo likiwa Afrika, ambayo ina viwango vya juu zaidi vya vifo vya akina mama duniani

Nchini Burundi, kiwango cha vifo vya akina mama kimepungua katika kipindi cha miaka 30 iliyopita na ni cha chini ukilinganisha na nchi nyingi za ukanda huo, lakini bado kuna haja kubwa ya kuwekeza zaidi katika mafunzo ya ukunga na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wao.

Ilikuwa mwishoni mwa ujauzito wake ndipo Bi. Kijijwa alipokwenda kupata huduma ya dharura katika kliniki inayoungwa mkono na UNFPA katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi.

Mkunga Aline Niyonkuru alisema “Baadhi ya wanawake hufika tayari wakiwa kwenye uchungu wa kujifungua na wakiwa na matatizo kwa sababu bado hawajui kuwa wanapaswa kuja kliniki kwa uchunguzi wa mara kwa mara wa ujauzito. Lakini kupitia uelimishaji wa jamii tunaamini hali hii itaimarika.”

Huduma muhimu za dharura zinaendelea

Wiki chache baadaye, Bi. Kijijwa alipata uchungu wa kujifungua na wakunga waliopata mafunzo ya huduma za dharura kwa wajawazito na watoto wachanga walikuwa tayari kusaidia.

“Wakunga wetu wanahakikisha huduma zinapatikana saa 24 kwa wanawake wengi wajawazito wanaoishi hapa,” amesema Bi. Niyonkuru. “Pia tunawafundisha akina mama kuhusu uzazi wa mpango baada ya kujifungua, kwa sababu wanawake wengi hapa hupata mimba nyingi bila nafasi sahihi kati ya ujauzito mmoja na mwingine.”

Kwa wastani, kliniki hiyo hupokea takribani wanawake 15 kila wiki kwa ajili ya kujifungua. Baadhi yao hufika wakiwa na matatizo makubwa kama kutokwa damu nyingi, hali inayohitaji huduma ya haraka ya kitabibu.

Kwa msaada wa dawa, vifaa na mafunzo yaliyotolewa na UNFPA kwa ufadhili wa Serikali ya DRC, wakunga wanaweza kushughulikia dharura hizo za uzazi.

“Ilikuwa ni uchungu mgumu sana wa kujifungua, na nilikuwa nikiombea maisha yangu na ya mtoto wangu,” anasema Bi. Kijijwa. “Mkunga alinipa moyo nisukume taratibu, na hatimaye mtoto wangu akazaliwa. Ninafurahi kwamba sote tumeishi.”

Mtoto wake wa kiume alikuwa mtoto wa 100 kuzaliwa salama katika kliniki ya Musenyi ishara ya nafasi muhimu ya wakunga katika kuhakikisha huduma za afya ya uzazi kwa wanawake waliokimbia makazi yao na wanaoishi katika mazingira magumu.

Mzazi mwenye mavazi ya bluu anamshika mtoto mchanga wakati akitabasamu kwa wazazi katika hema katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi nchini Burundi.
© UNFPA/Alec Junior Rumbete Maombi Kijijwa na mumewe Mapenzi Salongo pamoja na mtoto wao mchanga katika kambi ya wakimbizi ya Musenyi.

Umuhimu wa uchaguzi wa njia za uzazi wa mpango

Baada ya kupata ushauri kutoka kwa wakunga wa kliniki hiyo, Bi. Kijijwa aliamua kutumia uzazi wa mpango ili kulinda afya yake na kuendelea kuwalea watoto wake.

Sasa ninazungumza na wanaume wengine na viongozi wa dini ili waelewe umuhimu wa kulinda afya ya wanawake – Bw. Salongo

Mume wake, Mapenzi Salongo, anasema kuwa imani za kitamaduni na kidini zilikuwa zimemfanya ashindwe kuelewa umuhimu wa kupanga uzazi dhana potofu ambayo imegharimu maisha ya wanawake wengi.

“Hapo zamani hatukuamini uzazi wa mpango,” anasema Bwana. Salongo. “Nilimpoteza hata dada yangu kutokana na kutokwa damu nyingi wakati wa kujifungua. Daktari alikuwa amemwonya kuwa ujauzito mwingine usingekuwa salama, lakini tulipuuza ushauri huo.”

Lakini baada ya kushuhudia hatari aliyokuwa nayo mke wake na huduma aliyopata, amebadilisha mtazamo wake.

“Sasa ninazungumza na wanaume wengine na viongozi wa dini ili waelewe umuhimu wa kulinda afya ya wanawake.”

Mwanamume mtaalamu wa uzazi anafanya ukaguzi wa sauti ya juu (ultrasound) kwa mwanamke mjamzito katika kliniki iliyopo kwenye kambi ya wakimbizi ya Musenyi nchini Burundi.
© UNFPA/Alec Junior Rumbete Mfanyakazi wa afya anayeungwa mkono na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) anafanya uchunguzi kwa mwanamke mjamzito.

Wahudumu muhimu wa mstari wa mbele

Mgogoro unaoendelea nchini DRC umewafanya makumi ya maelfu ya watu kukimbilia nchi jirani ya Burundi ambayo nayo tayari inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula na ongezeko la wakimbizi kutoka nchi nyingine pamoja na wanaorejea nyumbani.

Kama wahudumu hawa wa afya wasingekuwepo, huenda ningempoteza mke wangu – Bwana. Salongo

UNFPA pamoja na washirika wake wanakidhi mahitaji ya dharura ya zaidi ya wakimbizi 100,000 wanaoishi katika jamii zinazohifadhi wakimbizi katika maeneo ya Musenyi na Busuma.

Wahudumu wa afya wanasaidia kuhakikisha kujifungua salama pamoja na kutoa ushauri wa kitabibu, vipimo vya ultrasound kwa wajawazito na huduma nyingine muhimu za afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana.

Wakunga sio tu wanahakikisha ujauzito salama na kuokoa maisha, bali pia husaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa, maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na upasuaji wa kujifungua usio wa lazima wa Caesarean, jambo linalochangia kuwa na jamii zenye afya bora zaidi.

“Kama wahudumu hawa wa afya wasingekuwepo, huenda ningempoteza mke wangu,” anasema Bwana. Salongo. “Leo tuko pamoja na tunawalea watoto wetu, na kwa hilo tunashukuru sana.”