Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA: Wakunga ni wadau muhimu wa afya ya uzazi duniani kote

A health worker in pink UNFPA uniform presents medical supplies from a woven basket to a mother holding her baby, in a clinic setting in DR Congo.
UNFPA DRC/Junior Mayindu Mkunga akisaidia kinamama na watoto wachanga katika Kituo cha Afya cha Turunga huko Goma.

UNFPA: Wakunga ni wadau muhimu wa afya ya uzazi duniani kote

Wanawake

Leo Mei 5 ni Siku ya Kimataifa ya Wakunga na kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA, idadi ya wakunga bado ni ndogo sana licha ya kuwa wao hutoa huduma muhimu za afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto mchanga duniani kote.

Shirika hilo limesema kuongezwa kwa wakunga milioni moja zaidi kungeleta mabadiliko makubwa katika huduma za afya na kuongeza nafasi ya kuishi kwa wanawake na watoto wachanga kila mahali.

Kwa mujibu wa UFPA wakunga sio tu wanahakikisha ujauzito salama na kuokoa maisha, bali pia hupunguza mimba zisizotarajiwa, utoaji mimba usio salama, maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na upasuaji usio wa lazima wakati wa kujifungua au Caesarean, hali inayochangia jamii kuwa na afya bora zaidi.

Katika nyakati za migogoro, mara nyingi wao ndio wahudumu wa kwanza kuwafikia wanawake wajawazito na watoto wachanga hata katika maeneo hatari au ya mbali limesema shirika hilo.

Hata hivyo, ukosefu wa uwekezaji pamoja na ubaguzi na vikwazo vya kijinsia vinaendelea kudhoofisha taaluma ya ukunga ambayo kwa kiasi kikubwa inaongozwa na wanawake, huku wakunga wengi wakikosa nafasi za uamuzi na uongozi.

Uwekezaji kwa wakunga ni uwekezaji katika maisha

Shirika hilo limeongeza kuwa uwekezaji kwa wakunga milioni moja zaidi ni njia yenye ufanisi mkubwa zaidi ya kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za ujauzito, kujifungua salama na huduma baada ya kujifungua.

Aidha limesema ongezeko la wakunga hao lingefanya mifumo ya afya kuwa nafuu zaidi na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto.

Taaluma ya ukunga inapaswa kulindwa kikamilifu katika bajeti za afya kitaifa na kimataifa.

UNFPA inasisitiza kuwa wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wakunga, ni wakati wa wakunga kuondoka pembezoni na kuwa kiini cha mifumo ya afya.