Mashambulizi dhidi ya huduma za afya kwenye migogoro yaongezeka miaka 10 baada ya Azimio 2286
Mashambulizi dhidi ya huduma za afya kwenye migogoro yaongezeka miaka 10 baada ya Azimio 2286
Mashirika ya kimataifa ya kibinadamu na afya yameonya kuwa hali ya usalama wa huduma za afya katika maeneo ya migogoro imeendelea kuzorota, licha ya juhudi za kimataifa zilizowekwa kulinda sekta hiyo.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo tarehe 4 Mei 2026 huko Geneva na viongozi wa Kamati ya Kimataifa ya Chama chaMsalaba Mwekundu (ICRC), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO, na Madaktari Wasio na Mipaka Médecins Sans Frontières (MSF), imeadhimisha miaka 10 tangu kupitishwa kwa Azimio 2286 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa huduma za afya katika maeneo yenye vita.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, badala ya hali kuimarika, mashambulizi dhidi ya hospitali, wahudumu wa afya, magari ya kubeba wagonjwa na wagonjwa yameendelea kuripotiwa mara kwa mara katika maeneo ya migogoro.
Hali ya ulinzi wa afya yazorota
Viongozi hao wamesema kuwa vitendo hivyo vinaonesha kukiukwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu pamoja na ukosefu wa dhamira ya kisiasa katika kuzitekeleza.
Wamesisitiza kuwa tatizo si udhaifu wa sheria zilizopo, bali ni kushindwa kwa pande husika kuziheshimu na kuzitekeleza kikamilifu.
Wito wa hatua madhubuti
Katika juhudi za kubadili hali hiyo, mashirika hayo yametoa wito kwa mataifa na pande zote zinazohusika katika migogoro kuchukua hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na:
· Kutekeleza kikamilifu sheria za kimataifa zinazolinda huduma za afya
· Kuingiza ulinzi wa huduma za afya katika mafunzo na miongozo ya kijeshi
· Kuimarisha sheria za kitaifa na mifumo ya utekelezaji
· Kutoa rasilimali na ufadhili wa kutosha kwa ajili ya utekelezaji
· Kushawishi washirika wao kuheshimu sheria za kimataifa
· Kuchunguza mashambulizi kwa uwazi na kuhakikisha uwajibikaji
· Kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya utekelezaji
Wito wa uongozi wa kisiasa
Mashirika hayo yamehitimisha kwa kusisitiza kuwa huduma za afya hazipaswi kamwe kuwa shabaha ya mashambulizi wakati wa vita.
Yametoa wito kwa viongozi wa dunia kuonesha uongozi thabiti wa kisiasa ili kulinda mifumo ya afya na kuhakikisha usalama wa wahudumu wa afya pamoja na wagonjwa katika mazingira ya migogoro.